2017-08-30 16:33:00

Mambo msingi ya kuzingatiwa katika utunzaji bora wa mazingira!


Karidnali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini anasema kwamba, Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, Laudato si ni waraka unaotoa mwelekeo wa ustaarabu mpya wa maisha unaojikita katika Mafundisho Jamii kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: Mwenyezi Mungu muumba wa mbingu na nchi; binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; mazingira na kazi ya uumbaji ambayo mwanadamu amekabidhiwa ili kuilinda, kuitunza na kuiendeleza.

Baba Mtakatifu Francisko katika waraka huu anapembua kwa kina kuhusu ekolojia ya binadamu na ekolojia ya mazingira; mambo ambayo ni sawa na chanda na pete, yanakwenda pamoja kwani yanategemeana na kukamilishana. Huu ni mwaliko wa kuitafakari dunia mintarafu jicho la Mungu, ili kuitunza dunia, iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi; kwa kupyaisha mahusiano kati ya mfumo wa maisha ya binadamu na mazingira.

Inasikitisha kuona kwamba, shughuli nyingi zinazofanywa na binadamu zimechangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira, kumbe, hapa kuna haja ya kuwa na uwiano bora zaidi ili kazi ya uumbaji iweze kuleta mafao kwa binadamu, kwa leo na kwa jili ya vijana wa kizazi kipya. Kwa mwamini mazingira ni jambo takatifu linalonesha mahusiano makubwa kati ya Mungu na viumbe wake. Kumbe, maendeleo ya sayansi na teknolojia yasaidie kuboresha mazingira na kamwe yasiwe ni chanzo cha uharibifu wa mazingira na matokeo yake ni athari za mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha umaskini na majanga kwa watu na mali zao sehemu mbali mbali za dunia. Hapa kuna umuhimu wa kuwa na mwelekeo mpya katika kufikiri, kutenda na kuishi ili kupambana na kinzani za kimazingira na kijamii zinazoendelea kumwandama mwanadamu.

Jumuiya ya Kimataifa isimame kidete kupambana na umaskini, kwa kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Ili kufanikisha changamoto hizi, kuna haja ya kuwa na sera na mikakati makini ya shughuli za kiuchumi zinazotoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi.

Baba Mtakatifu Francisko anaihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kuanzisha mchakato wa majadiliano yanayojikita katika ukweli na uwazi kwa kuguswa na mateso na mahangaiko ya wengine, tayari kujenga na kudumisha utandawazi unaofumbata mshikamano unaoongozwa na kanuni auni! Kardinali  Tauran anasema, kadiri ya mawazo ya mwandishi Henri Tinco kutoka Ufaransa, Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko unaweza kufupishwa na kuwekwa kama Amri kumi za utunzaji bora wa mazingira.

Mosi ni kuondokana na utandawazi usiojali kwani mazingira ni nyumba ya wote. Pili, pambana kufa na kupona dhidi ya uchafuzi wa mazingira kwa kutumia nishati rafiki, uzalishaji na mfumo bora zaidi wa maisha. Tatu, jitahidi kutunza vyanzo vya maji, kwani maji safi na salama ni haki msingi ya binadamu. Nne, toa kipaumbele cha kwanza kwa maskini kwa kupambana na ubaguzi na utengano wa kijamii, ili wote waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maisha.

Tano, pambana kiume na sera pamoja na mikakati ya maendeleo inayojikita katika kutafuta faida kubwa kwa hasara ya maisha, utu na heshima ya binadamu. Sita, jikite katika kanuni maadili na utu wema kwa kuheshimu na kutunza mazingira. Saba, kumbuka kwamba, mazingira ni kwa ajili ya wote kwa matumizi ya watu wa kizazi hiki na kile kinachokuja baadaye. Nane, ondokana na ubinafsi, jitahidi kuunga mkono juhudi za kilimo cha kisasa kisicho sababisha uharibifu wa mazingira na saidia mchakato wa watu wengi kupata maji safi na salama.

Tisa, anza kufanya marekebisho ya mtindo na mfumo wa maisha yako, ili kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Kumi na mwisho, jitahidi kuwa na furaha na kiasi katika maisha kwa kuheshimu na kutunza hata kile kidogo ulichonacho na kumshukuru Mungu kwa wema na ukarimu wake katika maisha yako. Jumuiya ya Kimataifa ijenge utamaduni wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa kulinda na kutunza mazingira, nyumba ya wote. Baba Mtakatifu analeta changamoto hizi kwa njia ya kawaida inayomfikirisha mtu, ili hatimaye, aweze kufanya maamuzi magumu katika mtindo wa maisha yake, ili kuishi vyema na vizuri zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.