2017-08-28 14:03:00

Papa Francisko kutembelea Myanmar na Bangaladesh 27 Nov -2 Des. 2017


Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko uliotolewa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Myanmar  na Bangaladesh pamoja na Serikali zao, kutembelea katika nchi hizi mbili kuanzia tarehe 27 Novemba hadi tarehe 2 Desemba 2017. Katika hija hii ya kitume, Baba Mtakatifu akiwa nchini Myanmar atatembelea miji ya Yangon na Nay Pyi Taw. Akiwa nchini Bangaladesh, Baba Mtakatifu atatembelea mji wa Dhaka. Ratiba elekezi ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko huko Myanmar na Bangaladesh, inatarajiwa kutolewa wakati wowote kuanzia sasa!

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Myanmar kuanzia tarehe 27- 30 Novemba 2017 inaongozwa na kauli mbiu “Upendo na Amani”. Hii inatokana na ukweli kwamba, Amani ya Kikristo inafumbatwa katika Upendo na hakuna amani pasi na upendo. Upendo ni kati ya fadhila ambazo zinapewa kipaumbele cha kwanza na familia ya Mungu nchini Myanmar. Upendo utasaidia mchakato wa kukuza na kudumisha amani, dhamana ambayo Baba Mtakatifu anapenda kuitekeleza wakati wa hija yake ya kitume nchini humo kama Mjumbe wa Amani!

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Bangaladesh itakuwa ni kuanzia tarehe 30 Novemba hadi tarehe 2 Desemba 2017.  Hija hii inaongozwa na kauli mbiu Utulivu na Amani; mambo msingi yanayopaswa kuchuchumiliwa na waamini wa dini mbali mbali nchini Bangaladesh; nchi ambayo ina historia, tamaduni, urithi na mapokeo yake. Amani ni kichocheo muhimu sana cha maendeleo endelevu ya binadamu.

Baba Mtakatifu anakwenda nchini Bangaladesh kama mjumbe wa utulivu na amani; anataka kuwaonjesha uwepo na upendo wa Mungu watu wa familia ya Mungu nchini Bangaladesh sanjari na kuwahimiza kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, kwani uharibifu wa mazingira umekuwa ni chanzo kikuu cha maafa kwa watu na mali zao nchini humo. Baba Mtakatifu anataka kuwatia shime, ili hata katika shida na mahangaiko yao, waendelee kuwa ni watu matumaini. Vatican ilikuwa ni nchi ya kwanza kutambua uhuru wa Bangaladesh kunako mwaka 1971. Taarifa hii imetolewa na Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican. 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.