2017-08-28 14:41:00

Kard.Braz De Aviz awaonya watawa kuwa makini na miungu ya kisasa


Shirikisho la Mashirika ya Watawa wa Kike Afrika ya Mashariki na Kati (ACWECA) , limefungua Mkutano wao wa 17 wa mwaka Jumapili, tarehe 27 Agosti 2017 na utakaofungwa tarehe 2 Septemba 2017 huko Makao makuu ya Sekretarieti ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Kurasini, Dar Es Salaam. Mkutano wao unaongozwa na kauli mbiu “Kuimarisha umoja wetu katika uinjilishaji wa kina mintarafu mazingira changamani ya nyakati hizi”. Mkutano huu umefunguliwa na Kardinali João Braz de Aviz,  Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa  la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume  akiwa pamoja na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Euzebius Nzigilwa akiwa pia ni msimamizi wa watawa Tanzania.

Katika ujumbe wa Baba Mtakatifu ulioletwa na Kardinali De Aviz, unasema; kwa fursa ya mkutano huo wanapaswa kujikita kwa undani kujenga urafiki na umoja kati yao ili kuweza kutoa zaidi ushuhuda wa kushiriki bega kwa bega katika utume wa Kanisa, kuunganika katika kutoa huduma kwa maskini wagonjwa na walio baguliwa. Baba Mtakatifu Francisko kwa ujumbe wake anamtakia mema na mafanikio Mwenyekiti wa Shirikisho la Mashirika ya watawa Sr Prisca Matenga na watawa wengine katika Mkatano huo wa 17 wa mwaka.

Sehemu ya Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko,anaamini kuwa Mkutano utakuwa ni fursa ya kugundua kwa upya utamu wa Injili, njia zipi mpya za kuweza kutokea, au hatua zipi mpya za ubunifu zilizo wazi pamoja na njia tofauti za kujieleza ikiwa ndiyo ishara fasaha na maneno yenye maana katika ulimwengu wa leo. Mwisho Baba Mtakatifu Francisko anawakabidhi washiriki wa Mkutano wa Shirikisho la Watawa chini ya  ulinzi wa mama Maria, Mama wa Kanisa, kwa furaha anawabariki na baraka za Kitume.

Naye Kardinali João Braz de Aviz, wakati wa kutoa mahubiri yake kwa washiriki 150 kutoka Shirikisho la Mashirika ya Kitawa wa Afrika Mashariki(ACWECA) amewaonya  watawa kuwa makini na miungu isiyoelezeka ya kisasa ambayo ni fedha. Fedha zina amuru kila kitu leo hii, pesa zina amrisha nguvu,fedha hufanya maskini, fedha hutengeneza kifo, inatengeza silaha na kujenga hofu. Hatutaki kutumikia fedha bali kumtumikia Mungu na kuweka fedha katika huduma ya Mungu,ndugu na kaka zetu; aidha kwa bahati mbaya baadhi ya watawa wameweka matumani katika akaunti za  benki badala ya kuweka akaunti kwa Mungu.Mambo haya yanajulikana kwani yameleta migogoro kati ya watawa na maaskofu.

Kardinali anauliza, inawezakanaje maaskofu na watawa kugombania suala la fedha?. Hilo siyo jambo zuri,na zinajulikana habari za ugonvi huo, kwa namna hiyo anawataka mabadiliko ya kweli.Halikadhalika amewashauri watawa kusikiliza zaidi kabla ya kunena na kujifunza kabla ya  kufundisha, ili na wengine wanao washirikisha waweze kuonesha mfano na kunufaika wao binafsi, kwa kufanya hivyo watakuwa na fursa ya  kuzungumza kile kitokacho rohoni.
Anawakumbusha  kwamba wamepokea kila kitu kwa uhuru kutoka kwa Mungu na kama ishara ya shukrani wanapaswa kumshukuru kwa baraka zake nyingi. Mungu alimtoa mwanae wa pekee kama dhabihu ya kuteketezwa kwa upendo wa binadamu na aliwaita waishi maisha yenye furaha kwa kufanya mapenzi yake. Amewahimiza watawa wa kike kufuata mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko ambaye mara zote anasema  kwamba watoke nje ya majumba yao kwenda kwa watu, kukaa na watu na kuangalia mateso na kuwa karibu nao. Na mwisho amesema ameshuhudia kuwa mafundisho ya Baba Mtakatifu  yamemsaidia yeye kuanza njia ya uongofu.

Ujumbe kutoka kwa Mwenyekiti wa Amecea Kardinali Berhaneyesus Demerew  Souraphiel

Katika Ujumbe kutoka kwa Mwenyekiti wa Amecea Kardinali  Berhaneyesus Demerew  Souraphiel katika tukio la Mkutano wa 17 wa mwaka, uliosomwa na Katibu Mkuu wa Amecea Padre Ferdinando Lugonzo , Kardinali anawasifu watawa. Ujumbe unasema jinsi gani wanavyoelewa na kutambua mchango mkubwa wa mafundisho na elimu kwa watoto na vijana  wanao utoa watawa ili kupunguza uchungu na mateso ya watu wengi hasa wanaoishi  katika vijiji pia  katika mchango wa kuhamasisha thamani ya Injili inayojikita kwa walio wengi.Ujumbe  pia unawasifu watawa kama mitume wasiochoka kusali na kujitoa kwa ajili ya Kanisa.

Kardinali Berhaneyesus ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Addis Ababa nchini Ethiopia amewambia watawa ni jinsi gani wao kama mitume wa kuendeleza ujumbe wa kuhubiri na kutoa  ushuhuda wa Bwana wetu Yesu kristo unavyohitaji mshikamano na umuhimu wa kuijilisha. Kwa miaka mingi sasa katika kanda  kuna ushuhuda wa mgawanyiko mkubwa, vita na mateso, kwa njia hiyo ni lazima watawa wote, wake kwa waume pamoja katika utume wao kuwa mstari wa mbele wa kuishi kwa mshikamano wa kweli ili sala zao kwa Bwana ziwe timilifu kama asemavyo Yesu, ili wote aliyo mpatia wawe wake na ulimwengu utambue kuwa ametumwa na yeye.

Salam Kutoka Baraza la Maaskofu Tanzania

Na Askofu Renatus Mkwenda aliwakilisha Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania kwa kuwakaribisha wote kwa niaba yake na amesoma hotuba ya Askofu Tarcisius Ngalalekumutwa, Rais wa Baraza la Maaskofu wa Tanzania. Katika hotuba hiyo  anapongeza Shirikisho wa Mashirika ya watawa wa kike wa Afrika ya Mashariki na Kati kuchagua Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wao wa 17 wa Mwaka. Kuchagua mkutano wa 17 wa mwaka kufanyika nchini Tanzania, umekuwa ni baraka kwa nchi; aidha watawa wa kike ni tunu ya Kanisa na ulimwengu. Maana kujitoa kwao kwa Mungu, watawa wanakumbatia ulimwengu kama upendo wa mama katika moyo wa mashirika ya watawa na vyama vya kitume.

Mkutano huo unaunganisha washiriki 150 kutoka katika nchi tisa ambazo ni Eritrea, Ethiopia, Kenya, Malawi, Sudan, Sudan ya Kusini, Tanzania, Uganda na Zambia. Vilevile washiriki wengine kutoka wakuu wa mashirika ya nchi mbalimbalimbali kama vile wafadhili wa ACWECA kutoka Baraza la maaskofu wa Marekani , Umoja wa wakuu wa mashirika ya kitawa wa kimataifa, wawakilishi kutoka Baraza la watawa wa kike wa Nigeria na wawakilishi kutoka Zimbabwe.

Angela Rwezaula
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 








All the contents on this site are copyrighted ©.