2017-08-22 11:16:00

Tunzeni mazingira kuepuka maafa kwa watu na mali zao!


Baba Mtakatifu Francisko  katika Waraka wake wa kichungaji “Laudato si” yaani  “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” anasema, hii ni sehemu ya mchakato wa kupambana na umaskini, magonjwa, vita na kinzani za kijamii, ili hatimaye, kujenga na kudumisha furaha, amani na utulivu. Uharibifu wa mazingira unahitaji wongofu wa kiekolojia unaobadili mfumo mzima wa maisha ya binadamu kwani hii ni dhamana ya kijamii, kimaadili na kidini sanjari na matumizi bora zaidi ya utajiri na rasilimali ya dunia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Baba Mtakatifu anazungumzia juu ya ustawi na maendeleo ya mwanadamu kwa nyakati hizi na kwa siku zijazo, kwa kutambua kwamba, dunia ni nyumba ya wote, inayopaswa kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa. Madhara yanayotokana na uchafuzi wa mazingira, tayari yanaonesha athari zake kwa kizazi cha sasa na kile kijacho. Kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya kimataifa kutambua athari zinazotokana na uharibifu wa mazingira katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu, tayari kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha mazingira bora.

Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko ni ujumbe wa matumaini unaopaswa kumwilishwa katika sera, mikakati na vipaumbele vya Jumuiya ya Kimataifa, mwanadamu akipewa kipaumbele cha kwanza. Hii inatokana na ukweli kwamba, binadamu na mazingira ni sawa na chanda na pete; ni mambo ambayo kamwe hayawezi kutenganishwa. Athari za mabadiliko ya tabianchi ni matokeo ya uharibifu wa mazingira unaofanywa na binadamu mwenyewe. Hapa utamaduni na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu, ni chanzo kikuu cha uharibifu wa mazingira.

Familia ya Mungu nchini Sierra Leone bado inaomboleza vifo vya watoto wake zaidi ya 500 waliofikwa na maafa makubwa baada ya kuporomokewa na udongo huko Freetown na wengine wengi kujikuta hawana tena makazi baada ya nyumba zao kukumbwa na maporomoko au kufunikwa na kifusi hivi karibuni. Padre Gerardo Caglioni, mmisionari kutoka Sierra Leone akizungumzia kuhusu maafa haya anasema, Kanisa liliwekeza sana nchini Sierra Leone baada ya kupigwa rufuku kwa biashara ya utumwa duniani. Freetown ukawa ni mji wa matumaini na kitovu cha elimu, ustawi na maendeleo.

Lakini, katika kipindi cha miaka 40, kumekuwepo na uharibifu mkubwa sana wa mazingira kiasi ambacho kimepelekea maafa makubwa kwa watu na mali zao. Maafa haya kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na shughuli za binadamu, kwani watu wameamua kujenga bila kufuata sheria, kanuni na taratibu na matokeo yake ni athari kubwa iliyojitokeza hivi karibuni. Watu wamefyeka sana misitu kwa ajili ya kuchoma mkaa na kukata kuni kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. Leo hii, Freetown, imegeuka kuwa ni jangwa!  Maafa haya ni changamoto kwa familia ya Mungu nchini Sierra Leone, kujipanga tena na kuanza kujikita katika sera na mikakati ya maboresho na utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Idara ya mipango miji ijipange tena upya, hifadhi ya takataka ngumu ipewe msukumo wa pekee pamoja na kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na mifereji ya majitaka ili kuimarisha ulinzi na usalama wa maisha ya raia na mali zao. Serikali iwe mstari wa mbele kuwahamasisha raia wake kulinda na kutunza mazingira. Waswahili wanasema ni heri kuzuia kuliko kuponya! Utunzaji bora wa mazingira ni dhamana, wajibu na changamoto ya: kimaadili, kijamii na kisiasa na kwamba, kila mtu anawajibu wa kulinda na kutunza mazingira.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.