2017-08-21 08:59:00

Kardinali Pietro Parolin yuko nchini Russia kikazi! Mapambazuko mapya


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kuanzia  tarehe 20 hadi tarehe - 24 Agosti, 2017 anafanya safari ya kikazi nchini Russia ili kutangaza Injili ya amani, matumaini, ili kusaidia ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu katika umoja, upendo na mshikamano wa dhati!  Ni mwaliko wa kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kisiasa kati ya Vatican na Russia; majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa la Kiorthodox na Russia na Kanisa Katoliki, hasa baada ya viongozi wakuu wa Makanisa haya kukutana na kuzungumza mjini Avana Cuba, kunako mwaka 2016.

Kardinali Pietro Parolin katika mahojiano maalum na Wakala wa Habari kutoka Russia, Tass kabla ya kuanza safari yake kuelekea Russia anasema, hii ni changamoto ya kuendeleza pia majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi, ili kujenga na kudumisha mazingira ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Ni hamu ya Baba Mtakatifu Francisko kuonesha umoja na mshikamano wa dhati na familia ya Mungu ambayo imekumbwa kwa miaka mingi na madhulumu, ili kuendeleza majadiliano ya kiekumene kama chachu ya maendeleo endelevu ya binadamu:kiroho na kimwili! Ni majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika sala na maisha ya kiroho; katika ushuhuda wa damu na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kwa namna ya pekee, majadiliano ya kiekumene kati ya waamini wa Kanisa la Kiorthodox la Russia na Kanisa Katoliki, yameota mizizi katika Ibada na heshima kwa Mtakatifu Nicholaus wa Bari, ambaye kwa muda wa miezi miwili, waamini mbali mbali waliweza kusali na kutoa heshima zao kwa Mtakatifu Nicholaus wa Bari, ambaye anaheshimika kama Baba wa majadiliano ya kiekumene! Changamoto ya mmong’onyoko wa tunu msingi za kimaadili na utu wema ni mwaliko kwa Makanisa mbali mbali kushirikiana na kushikamana, ili kwa pamoja kuweza kusimama kidete kutangaza na kushuhudia tunu msingi za kimaadili na utu wema, urithi na amana kubwa kutoka katika Makanisa haya.

Kardinali Parolin anasema, vitendo vya kigaidi ni uhalifu dhidi ya binadamu, ni hatari kwa umoja, mshikamano na mafungamano ya kidini, kijamii na kisiasa. Ni  changamoto inayopaswa kushughulikiwa kwa uangalifu mkubwa, ili kudhibiti athari zake katika maisha na mali za watu. Jambo la msingi ni kuendelea kuwekeza katika elimu na majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu na kamwe wasikubali kuwa ni vyombo vya chuki, uhasama na ghasia kati ya watu. Ni dhamana inayopania kufunda na kukomaza dhamiri za watu ili kutambua jema la kufuata na baya linalopaswa kuepukika. Vatican katika miaka ya hivi karibuni, imeendelea kuwekeza katika majadiliano ya kidini na kitamaduni katika ngazi mbali mbali; kwa kujikita katika huduma makini za kijamii na kiutu kama kielelezo cha mshikamano wa upendo na ukarimu kwa watu wa mataifa, licha ya tofauti zao msingi za kiimani! Kuhusu dhamana na nafasi ya Rais Donald Trump wa Marekani, Kardinali Parolin anakaza kusema, kama mmoja wa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa anao wajibu wa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kukabiliana na changamoto mamboleo zinazoiandama Jumuiya ya Kimataifa, hasa katika utekelezaji wa sera na mikakati inayopania kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo kwa sasa zinaendelea kuwatumbukiza watu wengi katika umaskini wa hali na kipato! Ushirikiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa hayana budi kusimikwa katika majadiliano yanayofumbatwa kimsingi katika ukweli na uwazi; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kamwe, vitisho vya mashambulizi ya kivita na matumizi ya silaha za kinyuklia au kikemikali ni mambo ambayo hayana tija katika mchakato wa kutafuta: haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Matatizo na changamoto za Jumuiya ya Kimataifa hazina budi kutafutiwa suluhu ya kudumu kwa njia ya majadiliano yanayofumbatwa katika amani. Baba Mtakatifu Francisko anawataka wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu na wala wasitumbukie katika kishawishi cha kutaka kutumia nguvu kama suluhu ya matatizo na changamoto za Jumuiya ya Kimataifa. Wawe ni wajenzi wa amani na kamwe wasielemewe na utaifa na masilahi yasiyokuwa na tija wala mashiko kwa Jumuiya ya Kimataifa!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, Vatican imekuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na machafuko ya kisiasa nchini Venezuela, ili kuhakikisha kwamba, suluhu ya amani ya kudumu inapatikana, ili kukuza na kudumisha demokrasia licha ya matatizo changamani yanayoikumba Venezuela kwa wakati huu. Majadiliano katika ukweli, haki, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi, ndio jibu muafaka katika kukabiliana na mpasuko wa kisiasa nchini Venezuela. Viongozi wa Serikali na wale wa upinzani, hawana budi kuonesha ujasiri wa kumaliza tofauti zao kwa njia kukutana na kuzungumza ana kwa ana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wote wa Venezuela. Ili kuweza kukutana, lazima waaminiane na kuthaminiana kama ndugu; kwa kuepuka vurugu na ghasia; kwa kuzingatia: haki, sheria, kanuni demokrasia na Katiba ya nchi.

Kardinali Parolin anasikitika kusema kwamba, kwa sasa Venezuela inakabiliwa na hali ngumu ya maisha, kwani wananchi wengi wametumbukia katika umaskini wa hali na kipato; wanakabiliwa na hali ngumu sana ya maisha kutokana na ukosefu wa mahitaji msingi kama vile: chakula, tiba na makazi; kiasi kwamba, wengi wao wanalazimika sasa kukimbilia katika nchi za jirani ili kutafuta: hifadhi, uhakika na usalama wa maisha yao! Kardinali Parolin, anazitaka nchi jirani na marafiki wa Venezuela kushikikamana ili hatimaye, kuweza kupata suluhu ya mgogoro na mpasuko wa kisiasa nchini humo unaotishia amani, usalama na mafungamano ya kijamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.