2017-08-21 10:18:00

Hija ya Kitume ya Papa Francisko nchini Perù: Umoja na matumaini


Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 18 – 21 Januari 2018 anatarajia kufanya hija ya kitume nchini Perù kwa kutembelea miji ya Lima, Puerto Maldonado na Trujillo, baada ya kutua na kutembelea nchini Chile kuanzia tarehe 15 hadi tarehe 18 Januari 2018. “Umoja wa Matumaini” ndiyo kauli mbiu inayoongoza hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Perù. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa njia ya video mapema mwezi Agosti, 2017 aliitaka familia ya Mungu nchini Perù kushikamana katika umoja wa matumaini.

Kardinali Juan Luis Cipriani Thorne, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Lima, nchini Perù anafafanua kwamba, hii ndiyo changamoto ambayo Baba Mtakatifu Francisko anataka ifanyiwe kazi na familia ya Mungu nchini Perù kama sehemu ya maandalizi ya hija yake ya kitume nchini humo! Itakumbukwa kwamba, hii ni ziara ya tatu kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro kutembelea nchini Perù. Kwa mara ya kwanza, Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea nchini Perù kunako mwaka 1985 na kurejea tena nchini humo kunako mwaka 1988 wakati wa maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu.

Baada ya miaka thelathini, Baba Mtakatifu Francisko anatembelea tena Perù ili kuwaimaarisha ndugu zake katika imani na matumaini kwa Mwenyezi Mungu aliye asili ya wema wote. Baba Mtakatifu anataka kuleta mwamko mpya wa ari na maisha ya kimisionari miongoni mwa watu wa Mungu nchini Perù, changamoto ni kwa watu kushikamana katika matumaini; kwa kujenga na kudumisha ujirani mwema unaofumbatwa katika maisha ya sala, mambo msingi yanayofafanuliwa kwenye nembo ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Perù. Nembo hii inakazia sala, masifu na furaha kwa watu wa Mungu kutokana na ujio wa Baba Mtakatifu Francisko nchini mwao.

Baraza la Maaskofu Katoliki Perù linasisitiza kwamba, kwa sasa bado ratiba elekezi inaendelea kuboreshwa kati ya Vatican viongozi wa Kanisa na Serikali ya Perù. Lakini, kwa hakika Baba Mtakatifu Francisko atatembelea na kuzungumza na wananchi wa Puerto Maldonado, wazawa asilia wa eneo hili, ambao watakuwa na bahati ya kukutana na Khalifa wa Mtakatifu Petro katika eneo la msitu wa Amazzonia, changamoto kwa familia ya Mungu kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Taarifa zinaonesha kwamba mji wa Trujillo ni kati ya miji mikubwa nchini Perù inayoandamwa mara kwa mara na athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa kukumbwa na mafuriko yanayosababisha maafa makubwa kwa maisha ya watu na mali zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.