2017-08-19 15:20:00

Maandalizi ya Siku ya Familia Duniani kwa Mwaka 2018 yapamba moto!


Maadhimisho ya Siku ya 9 ya Familia Duniani kwa mwaka 2018 yatafanyika Jimbo kuu la Dublin, Ireland kuanzia tarehe 21 – 26 Agosti 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Injili ya Familia: Furaha ya Ulimwengu”. Viongozi wakuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland wamewasilisha matumaini na matarajio ya familia ya Mungu nchini Ireland wakati wa maadhimisho haya. Hii itakuwa ni fursa kwa wanafamilia kushiriki katika semina na katekesi makini kuhusu tunu msingi za Injili ya familia; watashiriki katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, chemchemi ya upendo wa Mungu kwa familia ya binadamu na kwamba, watashiriki katika shughuli mbali mbali za kifamilia sanjari na kufanya maandamano kama ushuhuda wa Injili ya familia, ambayo ni Habari Njema kwa Watu wa Mataifa!

Askofu mkuu Diarmuid Martin wa Jimbo kuu la Dublin, Ireland akiwa ameandamana na Padre Timothy Bartlett, Katibu mkuu wa Maadhimisho ya Siku ya 9 ya Familia Duniani, anasema, tarehe 21 Agosti 2017, Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland linazindua mchakato wa maadhimisho haya kwa njia ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Sala, Majadiliano na burudani kwani familia bado inaendelea kuwa ni msingi wa Habari Njema kwa watu mamboleo. Hii itakuwa ni nafasi ya kuweza kupembua kwa kina na mapana changamoto pevu katika maisha na utume wa familia. Umuhimu wa simu za viganjani na madhara yake katika maisha ya ndoa na familia.

Ibada ya Misa Takatifu itaongozwa na Askofu mkuu Diarmuid Martin anayependa kukazia umuhimu wa furaha na changamoto katika utume na maisha ya ndoa na familia. Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika maisha ya ndoa kuna nyakati ambazo wanandoa wanarushiana sahani zinazopishana hewani utadhani ni mbayuwayu! Lakini pia kuna nyakati za furaha za kula kuku kwa mrija! Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ni kielelezo na mfano bora wa kuigwa na wanafamilia. Picha ya Familia itatembezwa kwenye majimbo yote nchini Ireland.  “Tuzungumze kuhusu familia! Tuwe sehemu ya familia” ni kauli mbiu inayofanyiwa kazi katika maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani kwa Mwaka 2018, Jimbo kuu la Dublin.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland linawaalika wanandoa kushiriki kikamilifu katika maandalizi na hatimaye maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani ili kupembua kwa kina na mapana: uzuri, utakatifu, changamoto, matatizo pamoja na matumaini ya Injili ya familia kwa sasa na kwa siku za usoni! Lengo ni kuhakikisha kwamba Injili ya familia inaendelea kuwa ni sababu ya furaha kwa ulimwengu.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutoa mwongozo makini ambao unapaswa kufuatwa kama sehemu ya tafakari ya Wosia wa Kitume, "Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia” wakati huu, Kanisa linapojiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya. Swali la msingi hapa ni kujiuliza ikiwa kama Injili inaendelea kuwa ni sababu ya furaha kwa ulimwengu? Je, Familia bado inaendelea kuwa ni Habari Njema kwa ulimwengu mamboleo? Baba Mtakatifu anakiri kwa kusema kwamba, ni kweli familia inaendelea kuwa ni sababu ya furaha na Habari Njema kwa walimwengu, kwani uhakika huu unafumbatwa katika mpango wa Mungu kwa mwanadamu; upendo ambao unapaswa kupewa jibu la “Ndiyo” na viumbe vyote kwani hiki ni kiini cha moyo wa binadamu.

Hii ni “Ndiyo” inayowaunganisha bwana na bibi tayari kushiriki katika mchakato wa kuhudumia uhai katika hatua zake zote! Hii ni “Ndiyo” ya Mungu inayodhihirisha ile dhamana yake kwa binadamu aliyejeruhiwa, anayetendewa vibaya na kutawaliwa na ukosefu wa upendo. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Familia kimsingi ni “Ndiyo” ya upendo wa Mungu. Upendo ni chimbuko ambalo linaiwezesha familia kushuhudia sanjari na kuzalisha upendo wa Mungu duniani. Bila upendo huu, si rahisi sana kuweza kuishi kama watoto wa Mungu, watu wa ndoa, wazazi na kama ndugu.

Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kuhimiza umuhimu wa familia kuishi kwa kujikita katika upendo kwa ajili ya upendo na ndani ya upendo wenyewe. Hii ina maana kwamba wanandoa wanapaswa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusameheana, kuvumiliana na kuheshimiana. Baba Mtakatifu anawaalika wanafamilia kumwilisha ndani mwao maneno makuu matatu: “Hodi, samahani na asante”. Mama Kanisa kila wakati anapata mang’amuzi ya udhaifu wa binadamu, ndiyo maana watu wote, familia pamoja na viongozi wa Kanisa wanapaswa kujenga unyenyekevu uliopyaishwa, unaotamani kufundwa vyema; kuelimishwa ili uweze kuelimisha; kusaidiwa ili uweze kusaidia; kusindikiza, kung’amua na kuwaingiza na kuwashirikisha watu wote wenye mapenzi mema.

Unaweza pia kujitaabisha kwa kujitafutia habari zaidi kwa kutumia mtandao ulioandaliwa kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani kwa Mwaka 2018 kwa anuani ifuatayo: worldmeeting2018.ie. Maandalizi haya yanafanywa kwa ushirikiano kati ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha ambalo liko chini ya uongozi wa Kardinali Kevin Farrell anayesaidiwa na Monsinyo Carlos Simòn Vazques, Mwakilishi wa Idara ya familia na maisha ndani ya Baraza hili la Kipapa. Viongozi hawa hivi karibuni, wametembelea nchini Ireland na kujionea wenyewe jinsi ambavyo maandalizi yanaendelea kufanyika. Wameangalia kwa kina na mapana, katekesi ya Injili ya familia inayopaswa kufanyiwa kazi wakati wa maadhimisho haya. Wajumbe wa Utume wa familia nchini Ireland wameshiriki kikamilifu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.