2017-08-19 15:51:00

Furaha ya upendo ndani ya familia ni dira na mwongozo wa familia


Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia” umegawanyika katika sura tisa zenye utangulizi mfupi, kwa kuonesha mchango mkubwa uliotolewa na Mababa wa Sinodi ya familia, mchango ambao unapaswa kutunzwa kama amana na hazina ya Kanisa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, si majadiliano yote mintarafu Mafundisho tanzu ya Kanisa, maadili au shughuli za kichungaji yanapaswa kujadiliwa na  Khalifa wa Mtakatifu Petro, bali mambo mengine yanahitaji kupatiwa ufumbuzi makini kadiri ya mila, tamaduni na changamoto mahalia. Hii inatokana na ukweli kwamba,  mila na tamaduni za watu zinatofautiana, kumbe, hapa kuna haja ya kutamadunisha changamoto hizi ili ziweze kupatia ufumbuzi wa kudumu kadiri ya mwanga na tunu za kweli za Kiinjili.

Utamadunisho ni muhimu sana hata katika Mafundisho ambayo yamefafanuliwa na Mama Kanisa katika uzito wake, hapa hakuna sababu ya msingi ya kuwa na mwelekeo wa utandawazi. Baba Mtakatifu analitaka Kanisa kujinasua na wasi wasi wa mabadiliko na utekelezaji mkali wa sheria zinazoelea angani. Baba Mtakatifu anasema malumbano yanayojitokeza kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii na machapisho mbali mbali na hata wakati mwingine kati ya viongozi wa Kanisa yanafanyika kwa kutaka mabadiliko makubwa bila kuwa na tafakari ya kina ya kile wanachotaka kubadilisha au kwa kuwa na hitimisho kavu la masuala ya kitaalimungu.

Wosia huu ni matunda ya mwanga wa Neno la Mungu unaozingatia ukweli na changamoto za maisha ya ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo. Unatoa mwelekeo wa Yesu katika kukuza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kuzijengea familia uwezo wa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia. Ni waraka unaokazia upendo thabiti ndani ya familia; upendo unaogeuka na kuwa ni chemchemi na asili ya maisha. Baba Mtakatifu Francisko anatoa mapendekezo yanayopaswa kufanyiwa kazi katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji mintarafu utume wa maisha ya ndoa na familia. Anawataka wazazi na walezi kuimarisha elimu na makuzi ya watoto wao, ili waweze kuwajibika kikamilifu katika maisha yao. Ni wajibu wa Kanisa kuwasindikiza, kung’amua na kuwasaidia wanafamilia wanaolegalega katika maisha na wito wao. Baba Mtakatifu anachambua kwa kina na mapana tasaufi ya maisha ya ndoa na familia!

Familia ya Mungu ichukue muda kuendelea kuusoma na kuutafakari wosia huu kwa uvumilivu pasi na haraka; na pale inapowekezana kuangalia mada maalum kadiri ya mazingira ya watu husika! Huu ni mchakato wa utume wa familia unaofumbatwa katika uvumilivu, huruma na udumifu ili kuwasaidia wanandoa kutekeleza dhamana na maisha yao kadiri ya Mafundisho ya Kanisa mintarafu utume wa ndoa na familia. Huu ni ufafanuzi uliotolewa hivi karibuni na Padre Josè Guillermo Gutìèrrez Fernàndes, Afisa kutoka Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha wakati wa mkutano wa familia kimataifa uliofanyika huko mjini Madrid, Hispania, ulioandaliwa na Jumuiya ya Maisha ya Kikristo kwa ushirikiano na Taasisi ya Kipapa ya Familia, Chuo kikuu cha Comillas. Mkutano huu umewashirikisha mabingwa wa utume wa ndoa na familia kutoka katika nchi 30, walioongozwa na kauli mbiu “Tazama wanavyopendana”, jibu makini linalotolewa na watu wa ndoa na familia kwa changamoto zilizoibuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”.

Padre Josè Guillermo Gutìèrrez Fernàndes ametumia fursa hii kupembua kwa kina na mapana utume wa maisha ya ndoa na familia katika maisha ya Kanisa; changamoto zilizoko kwa sasa, sera na mikakati inayopewa kipaumbele cha kwanza na Mama Kanisa mintarafu matunda ya Sinodi za Maaskofu kuhusu familia zilizoadhimishwa kunako mwaka 2014 na Mwaka 2015. Amebainisha changamoto za kisiasa, kijiografia na kitamaduni mintarafu utandawazi, mambo yanayolitaka Kanisa kuwa karibu sana na waamini kama Msamaria mwema; Mama mwenye huruma na mapendo, anayefundisha, anayeganga na kutaka kuponya madonda yanayowaandama watoto wake katika uhalisia wa maisha!

Changamoto ya kwanza ni kuporomoka kwa Injili ya matumaini miongoni mwa waamini sanjari na upendo wa Kikristo mintarafu kweli na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Hali hii inawapelekea vijana wa kizazi kipya, kushindwa kufanya maamuzi machungu katika maisha yao, kwa kuwajibika kikamilifu katika maisha ya ndoa na familia, hadi pale Mwenyezi Mungu atakapowaita waja wake, kwenye maisha ya uzima wa milele. Kuna matatizo na changamoto za kanuni maadili na utu wema; uwepo wa utamaduni wa kifo na mwelekeo tenge wa tendo la ndoa unaogeuzwa kuwa ni fursa ya kukidhi tamaa za mwili badala ya kuwa kweli ni kielelezo cha utimilifu wa upendo kati ya bwana na bibi.

Dhamana na utume wa familia katika nchi nyingi duniani, haupewi msukumo unaostahili na matokeo yake, familia imekuwa kama “mpira wa danadana”. Elimu makini kwa watoto ni dhamana ambayo kwa sasa inaondolewa kutoka kwa wazazi na walezi na matokeo yake ni mwelekeo tenge wa usawa wa kijinsia unaotaka kufuta tofauti kati ya mwanaume na mwanamke. Kimsingi, wazazi wanapaswa kuwa ni walezi na warithishaji wa imani, maadili na utu wema kwa watoto wao, lakini utume huu sasa unafanywa na baadhi ya taasisi pamoja na vyombo vya mawasiliano ya jamii.

Kumbe, Wosia wa kitume “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia” umekuja kwa wakati wake, ili kusaidia kujibu changamoto hizi zinazowaandama waamini katika utume wa ndoa na familia.  Viongozi wanaosimamia na kutekeleza shughuli za kichungaji kwa ajili ya ndoa na familia, wanapaswa kutambua fika changamoto hizi, ili kuweza kujizatiti kikamilifu, kwa kujivika fadhila ya uvumilivu na udumifu katika utekelezaji wa sera na mikakati ya maisha ya ndoa na familia. Baba Mtakatifu analitaka Kanisa kuwa na sera na mikakati inayotekelezeka na wala si mambo yanayoelea kwenye ombwe! Wawe makini kwa utu na heshima ya binadamu; wasaidie  kuelimisha umuhimu wa uhuru unaowajibisha, ili kuwasaidia wahusika kukomaa katika imani, maadili na utu wema. Wanandoa wasaidiwe kutambua ukweli kuhusu maisha yao; uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu kwa mwanadamu. Wawaoneshe wanandoa ambao katika uvumilivu na udumifu wao, hadi leo hii wamekuwa ni mfano bora wa kuigwa.

Majiundo makini ya awali na endelevu anasema Padre Josè Guillermo Gutìèrrez Fernàndes, ni muhimu sana kwa wanandoa ambao wanapaswa kuishi maisha yao yote katika kifungo cha upendo usiogawanyika hata kidogo! Wanandoa watambue dhamana na wajibu wao, ili kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari ndani ya familia, ili kujenga umoja na mshikamano ndani ya Kanisa, ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa watu wa nyakati hizi. Utakatifu wa maisha ya wanandoa ni changamoto endelevu katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji. Maandalizi ya wanandoa watarajiwa, dhamana na wajibu wa Kanisa kuwasindikiza wanandoa wapya; malezi na majiundo makini ya maisha ya ndoa na familia; utume kwa wazee ni kati ya changamoto ambazo Mama Kanisa anapaswa kuzivalia njuga kama sehemu ya mchakato wa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.