2017-08-17 15:19:00

Jumuiya ya Mt.Egidio yawasaidia wazee na wahitaji wakati wa kiangazi


Kama kawaida ya Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kuwakumbuka wale  wahitaji, hasa kipindi cha kiangazi wakati Kanisa linaadhimisha Sikukuu ya Kupalizwa Mbinguni mama Maria, hata mwaka huu tarehe 13 Agosti katika kituo cha meza ya Maskini Mjini Roma, wameandaa chakula cha mchana kwa ajili ya maskini wote wa mji ,tendo hilo pia limerudiwa tarehe 16 na 17 Agosti  katika kituo hicho. Mpango huo ni mmojawapo kati ya  mipango miwili ya Jumuiya ya Mtakatifu Egidio iliyoanzishwa kwa dharua ya kiangazi kuwawezesha wahitaji hasa wazee wasio kuwa na watu na maskini wengi kujumuika kwa pamoja.Pamoja na hayo Jumuiya zote za Mtakatifu Egidio nchini Italia nazo zinajikita katika njia ya mshikamano kwa wale wote wenye kuhitaji. Na hiyo ni pamoja na vituo vingine katika ulimwengu mahali ambapo jumuiya hizo zipo kama sehemu ya karama yao. Katika kituo cha Meza ya mshikamano iliyopo Dandola Roma pia wanajishughulisha na maandalizi ya chakula kwa ajili ya kuwasambazia watu wanao lala katika vituo vya Treni na vituo vinginevyo katika mji kwa maana ni wengi wasio kuwa na mahali pa kulala.

Taarifa pia inaeleza kuwa kwa bahati nzuri kipindi hiki cha kiangazi kimefurika  wasamaria wengi kutoka pande zote nchini Italia, ili kutumia muda wao wakati huu wa likizo kujitolea mjini Roma na sehemu nyingine za Jumuiya zao ambapo wanakutana na maskini ili kuwapa mshikamano wao na ukaribu.Shughuli hii ya kuwasaidia watu wasio kuwa na makazi inazidi kuongezeka mara dufu kwa wa umakini na ukaribu wa kirafiki wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kwa ajili ya wazee wanaobaki peke yao katika majumba na hata  katika kituo chao cha kutunza wazee kwa mwaka mzima.
Jumuiya ya Mtakatifu Egidio pia wanayo Programu itwayo “Wazee hoyee , inayojihusisha na wazee wenye umri zaidi ya miaka 80, progamu hii inafanya kazi zaidi  hasa kipindi cha kiangazi ambacho watu wengi wanakimbia mijini kwenda likizo na kuwaacha wazee peke yao.

Na zaidi katikati ya mwezi Agosti  wanajitahidi kutoa mshikamano, urafiki na wahamiaji na wakimbizi ambao wamefika kwa njia ya mikondo ya kibinadamu na familia za Waroma. Taarifa inasema ni lazima kufanya sikukuu ambayo inafukuza upweke na kuonesha sura nzuri ya nchi ya Italia ambayo haisahu kamwe maskini.

Sr Amgela Rwezaula

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 








All the contents on this site are copyrighted ©.