Tarehe 13 Agosti 2017 ilikuwa ni Siku ya Sala katika Peninsula ya Korea, siku
iliyo andaliwa na Baraza la Makanisa Ulimwenguni ambapo kwa mwaka huu wametoa kipaumbele
zaidi katika nchi ya Korea kutokana na hali ya mvutano wa kisiasa na kijeshi.
Shirika la habari la Osservatore Romano linaeleza kuwa, siku ya maombi imewekwa rasmi
Jumapili inayoekelea tarehe 15 ya mwezi Agosti , siku ambayo inakumbusha uhuru wa
nchi ya Korea kutoka Ukoloni wa Kijapani mwaka 1945, vilevile inakumbusha hata mgawanyiko
wa visiwa vya Korea katika sehemu mbili tofauti. Siku ya maombi ya sala ilikuwa imegawanyika
katika sehemu tofauti kwa mantiki ya hija ya haki na amani iliyoandaliwa na Baraza
hilo la Makanisa Duniani, ikiwa na kauli mbiu kutoka Barua ya Mtakatifu Paulo kwa
Waroma isemaayo “ kwa hiyo tuyazingatie daima mambo yenye kuleta amani na yanayotusaidia
kujengana” (Waroma 14, 19).
Katika suala la nchi ya Korea, pia upo wito wa Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa
duniani Olav Fykse Tveit ambaye anaona umuhimu wa kutafuta suluhisho la haraka ili
hatari ya migogoro hiyo iweze kupungua badala ya kuongezeka. Kwa namna hiyo anasisitizia
Jumuiya ya Kimataifa kuwa makini katika kuingilia kati ili kuweza kutoa ufumbuzi wa
mgogoro huo.
Ni zaidi sasa ya miaka 30 Baraza la Makanisa ulimwenguni imejikita katika kuongoza
mazungumzo na mikutano kati ya wakristo wa sehemu mbili za Korea. Mara kwa mara wamekuwa
na ugomvi wa maneno mengi ambayo yamezidisha mivutano na kusababisha hatari na migogoro
ya silaha na nguvu za nyuklia.
Sr Angela Rwezaula
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican
All the contents on this site are copyrighted ©. |