2017-08-14 11:28:00

Tamko la Leuca linapania kujenga umoja, ushirikiano na udugu!


Vijana zaidi ya 250 kutoka sehemu mbali mbali za dunia, lakini wengi wao wakiwa ni wale wanaotoka: Albania, Italia, Nigeria, Senegal, Siria, Tunisia na Uturuki kuanzia tarehe 13 hadi tarehe 14 Agosti 2017 wamekuwa wakishiriki katika mkutano wa kimataifa unaozijumuisha Nchi ambazo zinapakana na Bahari ya Mediterannia kwa kuongozwa na kauli mbiu “Mediterrania: Bandari ya Udugu”. Huu ni mkutano ambao umeandaliwa na Jimbo Katoliki la Ugento- Santa Maria di Leuca, lililoko nchini Italia kwa kushirikiana na taasisi pamoja na vyama mbali mbali vya kitume, ili kukuza na kudumisha utamaduni wa ukarimu na mshikamano ili kuendeleza amani na udugu kati ya watu!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Askofu Vito Angiuli wa Jimbo Katoliki la Ugento- Santa Maria di Leuca anamshukuru na kumpongeza pamoja na kuzitia shime Jumuiya za Wakristo katika maeneo ya Mediterrania, vijana wa kizazi kipya pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuthamini uwepo wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kama fursa ya kukua na kukomaa kiutu; kwa kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana na kujadiliana na kwamba, ni wakati muafaka wa kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo.

Baba Mtakatifu anawataka wadau mbali mbali kuendelea kutembea katika njia hii ya ukarimu, upendo na mshikamano, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Anawaombea wote ulinzi na tunza ya Bikira Maria, washiriki wote wa mkutano huu wa kimataifa unaopania pamoja na mambo mengine, kutoa “Tamko la Leuca”.

Waandaaji wa mkutano huu wanasema, vijana wanayo ndoto na matamanio halali ya maisha bora zaidi yanayowasukuma kuelekea “Mediterrania: Bandari ya Udugu”. Mkutano huu ni fursa ya kuangalia na kusoma alama za nyakati, ili kusaidia mchakato wa upatanisho wa kiutu, utakaowawezesha watu kuwajibika kikamilifu katika maisha kwa kukuza na kudumisha udugu unaoelnga kuvunjilia mbali kuta za utengano kati ya watu wa Mataifa. Wanapania kujenga madaraja ya umoja, mshikamano na upendo; kwa kukuza, kudumisha na kuthamini umoja unaofumbatwa katika utofauti, ambao kimsingi ni utajiri mkubwa katika maisha ya watu wa Mataifa. Kwa njia hii, watu wanaweza kujenga msingi mpya wa urafiki kati yao!

Washiriki wa mkutano huu wanatamka wazi kwamba mchango wao unaoibuliwa kutoka katika udugu na ujirani wao kwenye Bahari ya Mediterrania unawasukuma na kuwahamasisha kujenga msingi wa mshikamano, ili kuigeuza Bahari ya Mediterrania ambayo leo hii umegeuka kuwa ni “kaburi lisilo na alama kwa wakimbizi na wahamiaji” ili hatimaye, Bahari ya Mediterrania iweze kuwa ni mlango wa matumaini kwa watu kushirikishana: bidhaa na miradi yao; mawazo, karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu, ili kujenga dunia inayosimikwa katika: haki, umoja na udugu!

Washiriki wa mkutano huu wanataka kuimarisha kadiri ya uwezo wao udugu na ushirikiano ili ardhi na kazi ya mikono ya wanadamu; utajiri na rasilimali za dunia hii; ustawi na maendeleo yaweze kutoa mwelekeo mpya unaojikita katika amani kwa watu wote. Vijana wa kizazi kipya wanataka sauti yao isikike kwa viongozi wa Serikali zao, ili waweze kuwa na ujasiri wa kuvunjilia mbali kuta za utengano zinazosababisha hofu na wasi wasi usiokuwa na mashiko. Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa waweze kujizatiti kikamilifu kukuza na kudumisha ushirikiano na mshikamano, ili kusaidia mchakato wa kuwashirikisha wahamiaji na wakimbizi katika maisha ya wenyeji wao. Wawe na ushupavu wa kuondoa ukosefu wa haki msingi ndani ya jamii kwa kujikita katika maendeleo endelevu ya binadamu, chemchemi ya furaha na amani ya kweli!

Washiriki wa mkutano huu wanatamka wazi kwamba, udugu ni matunda ya huruma inayosimikwa katika mchakato wa kuondokana na mawazo finyu kwamba, watu wanatafuta unafuu wa maisha tu na kuanza kujikita katika msamaha na furaha ya kweli inayofumbatwa katika upendo, kielelezo makini cha maendeleo endelevu ya utu na heshima ya binadamu; mambo msingi kwa watu wote. Kutokana na changamoto hii, wajumbe wa mkutano huu wanawataka viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa, watu maarufu na mashuhuri kujenga na kudumisha madaraja ya kuwakutanisha watu. Kujizatiti katika kupiga rufuku na hatimaye, kukomesha biashara ya silaha duniani na badala yake, kuwekeza katika miundo mbinu itakayosaidia kukuza na kudumisha maendeleo endelevu ya binadamu, kiini cha amani ya kweli. Wawe na ujasiri wa kuwaruhusu vijana kuondoka na kwenda kwenye “Bandari ya Udugu” ili kusafiri na kuyaendea mapambazuko ya matumaini kwa siku za mbeleni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.