2017-08-14 08:22:00

Papa Francisko: Imani si njia ya mkato katika maisha!


Yesu Kristo baada ya kuwalisha watu elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili, alijitenga na wafuasi wake, akaenda kusali faraghani baadaye akajidhihirisha kwa mitume wake, akitembea kwa miguu juu ya maji! Petro anamwomba ruksa ili aweze kuungana naye, lakini kwa bahati mbaya, akaingiwa na shaka kwa sababu ya imani haba na hapo akaanza kuzama na huo ukawa ni mwisho wa muujiza! Miujiza iliyotendwa na Kristo Yesu ilipania kuimarisha imani ya watu wake! Ni tukio lenye alama zinazoweza kuwa ni msaada mkubwa kwa mwamini binafsi au jumuiya ya waamini katika ujumla wake.

Hiki ni kipimo cha imani ya kweli kwa Kristo na Kanisa lake. Chombo kinachozungumziwa na Mwinjili Mathayo katika Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya XIX ni maisha ya kila mwamini yanayofumbatwa ndani ya Kanisa. Mawimbi mazito na upepo mkali ni matatizo na changamoto ambazo zinawaandama waamini binafsi na Kanisa katika ujumla wake. Ukelele wa Petro mtume, ni kilio na hamu ya waamini kusikia na kuhisi uwepo wa Kristo Yesu katika maisha yao. Ni wasi wasi, woga na mashaka yanayowaandama waamini katika safari ya maisha yao hapa duniani.

Wakati ule, Petro mtume alitaka kuonja uwepo wa Kristo katika maisha yake na wala si tu kusikia maneno yake! Alitaka kuwa na uhakika wa usalama wa maisha yake, kama wanavyofanya baadhi ya watu kwa kupiga ramli kwa waganga wa kienyeji au kusoma utabiri wa nyota! Kwa mwamini anapofikia hatua hii ni kuanza kuzama kama risasi ndani ya maji! Hiki ni kielelezo makini cha imani haba kama “kiatu cha raba”. Injili ya Jumapili hii, inawaonesha waamini kwamba, imani kwa Kristo Yesu na Neno lake, haliwapatii maisha rahisi, kama “maji kwa glasi” wala kuwaondoa katika mataizo, magumu na changamoto za maisha. Lakini, imani inawahakikishia waamini uwepo endelevu wa Kristo Yesu, unaowawezesha kusonga mbele katika mapambano ya maisha kwa kujiamini hata kama njia inaonekana kuwa na giza totoro! Imani si njia ya mkato katika shida na magumu ya maisha, bali ni msaada makini unaotoa maana halisi ya maisha!

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 13 Agosti 2017. Mfano ulitolewa na Mwinjili Mathayo ni hali halisi ya maisha na utume wa Kanisa kwa nyakati zote. Kanisa ni chombo ambacho kinatembea na katika safari yake, lazima kitakumbana na mawimbi mazito pamoja na upepo mkali, unaotishia usalama wake kiasi hata cha kutaka kukizamisha. Kanisa linaokolewa si kwa nguvu, jeuri wala ujasiri na ubora wa waamini wake, bali uhakika wa usalama unaofumbatwa katika imani kwa Kristo Yesu na Neno lake linalookoa.

Katika mwelekeo huu, waamini watambue kwamba, wako salama salimini, licha ya dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu. Waamini wawe na ujasiri wa kupiga magoti na kumsujudia Kristo kwa kusema, “hakika wewe ni Mwana wa Mungu” kama walivyothubutu kusema wale mitume, walipoyaona matendo makuu yaliyotendwa na Kristo. Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Bikira Maria awasaidie kuwa na imani thabiti kwa Kristo na Kanisa lake, ili kuweza kukabiliana na changamoto za maisha pamoja na kuendelea kukaa ndani ya Kanisa, kwa kukataa vishawishi vinavyoweza kuwatumbukiza katika sera na mitindo ya maisha inayoweza kuwaangamiza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.