2017-08-09 13:48:00

Mtafuteni Mwenyezi Mungu, ili aweze kuwaokoa katika shida zenu!


Ndugu yangu mpendwa, mtu mmoja aitwaye R. H. Benson anasema; ni katika ukimya tunamfahamu Mungu na katika fumbo anajionesha. Katika dominika iliyopita tulikumbushwa haja ya kwenda kwa Bwana na kumwomba atupe chakula na tukaona Bwana anatuagiza sisi tuwape chakula wenye njaa. Na tafakari yetu ikawa;  je wewe unayo mikate mingapi na samaki wangapi?  Dhamira inayotungoza leo hii inatupa changamoto ya kumtambua Mungu anayeokoa.

Katika somo la kwanza tunaona Nabii Eliya akiwa amechoshwa na mambo yaliyo kinyume yafanywayo na watu wake – anaendelea kumwomba Mungu aondoe roho yake. Lakini Mwenyezi Mungu ana mipango mingine naye. Anampeleka kwenye mlima ambao miaka 400 kabla yake alifunga agano na Musa. Somo hili la kwanza laelezea mang’amuzi yake katika mlima huu. Yeye alidhani kuwa ujio wa Mungu huambatana na mambo makubwa, ya ajabu n.k. Kumbe Mungu anafika katika upepo mwanana. Baada ya ujio huu wa Mungu, Eliya anang’amua kwa namna nyingine kuwa Mungu yupo. Baada ya tukio hili, Nabii  anarudi kati ya watu wake na kuendelea kutoa ushuhuda wa Mugu katika kukamilisha utume wake wa kinabii. Tukio hili la Eliya ni changamoto kubwa kwetu wakristo na twaweza tena kujiuliza Je, chanzo cha imani yetu ni nini? Tunatafuta imani yetu wapi au katika mazingira yapi?  Na hii ndiyo changamoto iliyo wazi mbele yetu. Tunamwona Yesu katika mahangaiko yetu ya kiimani? Tunamwita? Tukiitika bado tunabaki tumesimama imara? Ndiyo changamoto ya Liturujia yetu ya leo; kumtafuta Mungu – Ee Bwana tuokoe.

Katika Injili tunasikia habari ya Yesu kutembea juu ya maji.  Yesu aliwaaga wanafunzi wake waende mbele na baadaye atawafuata. Njiani wanapata shida ila mara Yesu anaonekana kati yao ili kuwaokoa. Katika fundisho hili la imani, ambapo Yesu anatembea juu ya maji, ni angalisho kwetu sisi, hasa tunaposhawishiwa na kutaka kuondoa jicho letu katika kumtazama Bwana na kuvutwa na heka heka za ulimwengu huu.

Mtume Petro anasema, Bwana kama ni wewe niite nije uliko – mstari wa 28 na 29 Yesu anamwamuru aje kwake. Yaonekana Yesu anatoa amri isiyowezekana kibinadamu. Hakika katika sheria za kisayansi haiwezekani na Petro mwenyewe aliyekuwa mvuvi anajua wazi kuwa si rahisi kutembea juu ya maji. Kinachoonekana hapa ni kuwa amri yo yote ile ya Yesu inatupatia nguvu ya kutenda. Kama mwanadamu, Petro anazidiwa na ule upepo na anaanza kuzama – mstari 30, lakini mara Bwana anafikana kumwokoa ingawa anamkemea. Imani kwa Kristo inamwokoa. Alijua fika kwamba haiwezekani ila anatii amri ya Bwana na anaokoka yeye na wale aliokuwa nao. Katika  2Kor. 5:7 tunasoma kuwa;  maana twaenenda kwa imani na si kwa kuona. Na neno hili litualike leo kutafakari vizuri ufuasi wetu.

Ndugu zangu, bado hata leo katika dunia yetu, mawimbi yako mengi. Hata sisi tunaoamini tunajikuta katika mahangaiko hayo. Tupo katika ulimwengu wenye mantiki yake na wakati huo huo tunae Yesu anayetuita. Kwa upande mmoja tunao ulimwengu wenye mivuto na mitindo mbalimbali ya maisha na upande mwingine tunaye Mungu anayetaka sisi tuutawale ulimwengu. Kwa anayemwamini Mungu ana haja ya kumwita Mungu – ‘Ee Bwana Tuokoe’. Lakini ni wangapi katika fujo hizo za dunia au katika kiburi cha maendeleo ya mwanadamu wanaweza kuona uwepo wa Mungu?  Nabii Eliya alitegemea Mungu aonekane katika mambo makubwa lakini ikawa kinyume chake.

Wengi wetu, kama si wote, tunajua wazi jinsi neno moja zuri linavyokuwa ni faraja tosha kwa mwenye kuhitaji. Kama Kristo alivyotoa neno moja – njoo, usiogope na dhoruba ikaacha, nasi basi kama Kristo leo tunapata changamoto hiyo hiyo hasa tunapotumwa kuwa wapashanaji wema wa habari njema ya Kristo kwa ajili ya wokovu wetu na watu wake Mungu. Ujasiri wa kina Nabii Eliya na Mtume Petro utuwajibishe leo ili tuweze kutenda na kuenenda katika njia zake Bwana bila wasiwasi na mashaka yo yote. Neno la Mungu katika Injili ya Yoh. 6:44,  hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka, nami nitamfufua siku ya mwisho litutie nguvu na kutuimarisha. Sisi tumeshakombolewa tayari na wajibu wetu ni kuishi huo ukombozi huku tukitambua kuwa Bwana atakuja siku ya mwisho kwa ajili ya hukumu.

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.