2017-08-08 12:10:00

Miaka 75 tangu alipofariki dunia Mt. Edith Stein: toba na wongofu!


Mama Kanisa tarehe 9 Agosti 2017 anaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 75 tangu Mtakatifu Theresa Benedetta wa Msalaba, maarufu kama Edith Stein, alipofariki dunia kwenye kambi ya mateso ya Auschwitz kunako mwaka 1942. Edith Therese Hedwig Stein alizaliwa kwenye familia ya Kiyahudi kunako tarehe 12 Oktoba 1891 huko Breslau. Kunako mwaka 1921 akaongokea dini ya Kikristo na tarehe 1 Januari 1922 akapewa Sakramenti ya Ubatizo. Mtakatifu Yohane Paulo II akamtangaza kuwa Mtakatifu hapo tarehe 11 Oktoba 1998. Na mwaka mmoja baadaye, yaani mwaka 1999, Mtakatifu Yohane Paulo II akamtangaza kuwa ni kati ya Wasimamizi wa Bara la Ulaya na mfano bora wa kuigwa katika maisha ya Kikristo bila kumezwa na malimwengu licha ya mafanikio makubwa ambayo Mwenyezi Mungu anaweza kumkirimia mja wake!

Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 75 tangu Mtakatifu Theresa Benedetta wa Msalaba, alipofariki dunia kwenye kambi ya mateso ya Auschwitz, Baraza la Maaskofu Katoliki Poland limeandika Waraka wa kichungaji, likiwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea wongofu wa Bara la Ulaya! Maaskofu wanasikitika kusema kwamba, Barani Ulaya kula sera na mbinu mkakati inayopania kufutilia mbali mizizi ya Ukristo Barani Ulaya. Matokeo yake ni kukumbatia utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini; kinyume kabisa cha Injili ya uhai.

Watu wamekengeuka kiasi hata cha kutaka kuhalalisha ndoa za watu wa jinsia moja, kinyume kabisa cha mpango wa Mungu katika maisha ya binadam. Mwelekeo huu unakwenda kinyume cha kanuni msingi za maisha ya binadamu; utu wema na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, msingi thabiti wa Injili ya familia. Kuna baadhi ya wanasiasa wanaotaka kufuta tofauti za kijinsia, kati ya bwana na bibi ili kuambata kile kinachodaiwa kuwa ni “Usawa wa kijinsia”.

Baraza la Maaskofu Katoliki Poland linakaza kusema, kutokana na sera na mikakati kama hii, watu wanataka kumfutilia mbali Mwenyezi Mungu katika: sera, mipango na mikakati yao ya maisha. Zote hizi ni dalili za ukanimungu Barani Ulaya; mambo ambayo yanaenezwa kwa kasi kabisa kwa njia ya misaada ya kiutu kwenye nchi maskini zaidi duniani. Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake binafsi “Spes aedificandi”, yaani “Matumaini yanayojenga”, aliyoichapisha hapo tarehe 1 Oktoba 1999, anamkumbuka kwa namna ya pekee kabisa Mtakatifu Edith Stein, aliyejitahidi kumwilisha ndani mwake mateso na madhulumu ya Wayahudi waliokuwa wanafanyiwa na utawala wa kinazi.

Barani Ulaya kumekuwepo pia na Serikali za mabavu ambazo zimechafua sura ya Bara la Ulaya katika miaka ya hivi karibuni. Yote haya ni matendo ya aibu. Lakini Edith Stein ndani mwake, alihisi uzito wa Msalaba wa Kristo Yesu, waliokuwa wanatishwa watu wake. Alihisi kushiriki kikamilifu katika mateso, dhuluma na nyanyaso zilizokuwa zinafanywa kwenye Kambi ya Mateso ya Auschwitz-Birkenau. Sauti ya kilio chake ikachanganyikana na ile sauti ya ndugu zake waliokuwa wanateswa vibaya kambini hapo. Lakini, hii ilikuwa ni sauti ya kilio cha Kristo anayewahakikishia wale wote wanaoteseka kwa ajili ya jina lake faraja ya kudumu. Baraza la Maaskofu Katoliki Poland linasikitika kusema kwamba, Bara la Ulaya linaanza kumeguka vipande vipande katika maisha ya kiroho; kwa kusahau kwa makusudi kabisa mizizi ya Kikristo na kuishi kana kwamba hakuna Mungu.

Edith Stein wanasema Maaskofu Katoliki Poland, ni alama ya ukinzani, inayoonesha ukuu wa binadamu na utakatifu wa maisha yake. Ni shuhuda makini  wa imani na matumaini ambaye alitumia karama na mapaji yake kwa ujasiri na ukweli wa kiakili kumtafuta Mwenyezi Mungu, ambaye leo hii anasukumizwa pembezoni mwa maisha ya watu. Maaskofu wanawaalika waamini kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, kwa kumwomba Mwenyezi Mungu neema na baraka ya kutubu na kumwongokea sanjari na kuonesha ujasiri wa kurejea misingi ya Kikristo ambayo ndiyo inayopaswa kuwa ni nguzo ya Bara la Ulaya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.