2017-08-05 16:19:00

Siku kuu ya Kung'ara Bwana: Kifo cha Papa Paulo VI & Waraka wa Kitume


Liturujia ya Siku kuu ya Kung’ara Bwana inasimulia jinsi ambavyo Kristo Yesu alivyowachukua mitume wake watatu yaani: Petro, Yakobo na Yohane wakajitenga na hapo akang’ara sura mbele yao, kiasi cha kuwafunulia ukuu, utukufu na utakatifu wake ambao walipaswa kuupokea kwa njia ya imani, mahubiri pamoja na miujiza mbali mbali aliyotenda katika maisha yake. Tukio la kung’ara kwa Yesu linasindikizwa na uwepo wa Musa na Eliya waliokuwa wanazungumza na Yesu, kielelezo cha utimilifu wa Sheria na Unabii.

Mwanga angavu uliokuwa kiini cha tukio hili ni kielelezo cha mwanga unaopaswa kuangaza akili na mioyo ya Mitume wa Yesu, ili waweze kumfahamu Bwana wao. Ni mwanga unaoangaza Fumbo la maisha ya Yesu na hivyo, kufunua maisha na utume wake wote unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Katika maadhimisho ya Sherehe ya Kung’ara Bwana, Kanisa kwa mwaka huu, linafanya kumbu kumbu ya miaka 39 tangu Mwenyeheri Paulo VI alipofariki dunia tarehe 6 Agosti 1978 akiwa kwenye Ikulu ndogo ya Castel Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma na kuzikwa tarehe 12 Agosti 1978 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Itakumbukwa kwamba, alitangazwa kuwa Mwenyeheri hapo tarehe 19 Oktoba 2014 na Baba Mtakatifu Francisko. Kanisa pia linakumbuka miaka XXIV tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapisha Waraka wa kitume “Mng’ao wa Ukweli” yaani “Veritatis Splendor” uliochapishwa kunako tarehe 6 Agosti 1993. Ni Waraka unaojikita katika mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu maadili na utu wema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.