2017-08-03 15:06:00

Papa Francisko awashukuru wajumbe wa "Knights of Columbus"


Chama cha Kitume cha “Knights Of Columbus”, kilianzishwa na Padre Michael J. McGivney, kunako mwaka 1882, kimekuwa kikitoa mchango mkubwa kwa Kanisa Katoliki katika huduma kwa maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kikiongozwa na misingi ya mwanzilishi wake inayojikita katika: upendo, umoja na udugu.  Ni Chama cha kitume kinachoendelea kujitoa bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kuwa Jamii wanamoishi inakuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, kwa kuendelea kuunga mkono mikakati ya shughuli za kichungaji zinazofanywa na Mama Kanisa hasa katika kuimarisha imani, matumaini na mapendo pamoja na kudumisha tunu msingi za maisha ya kifamilia.

Kutokana na uwepo wake, waamini walei wameshirikishwa kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Wajumbe wa chama hiki kuanzia tarehe 1- 3 Agosti 2017 wanafanya mkutano wao wa 135 unaoongozwa na kauli mbiu “Kwa kuguswa na upendo na nguvu ya Mungu” iliyofunuliwa kwa njia ya Fumbo la Pasaka pamoja na Roho Mtakatifu kuwashukia wafuasi wa Kristo. Hii ndiyo hazina ya maisha ya upendo ambayo haiwezi kudanganya, na ujumbe ambao hauwezi kupotosha au kusikitisha, kwani unapenya ndani ya nyoyo za waamini ili kuwategemeza na kuwafanya kuwa bora zaidi.

Upendo na nguvu ya Mungu ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa unaofumbatwa katika mshikamano na ushuhuda wa upendo wa Mungu unaokuwa na kupanuka. Huu ni upendo ambayo umefunuliwa na Kristo Yesu kwa njia ya Fumbo la Msalaba, kielelezo cha ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko ulioandikwa kwa niaba yake ya Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Bwana Carl Anderson, Mkuu wa Chama hiki. Anasema: vita, ghasia na mipasuko ya kijamii inayoendelea sehemu mbali mbali za dunia ni kielelezo cha cha uchu wa mali na madaraka: kiuchumi, kisiasa au kijeshi, hali inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kukataa kishawishi cha utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani zao; kwa kujikita katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mashiko na mvuto, tayari kusaidia mchakato wa toba na wongofu wa ndani unaosadidia katika ujenzi wa amani sanjari na maboresho ya maisha ya watu. Baba Mtakatifu anawapongeza wajumbe wa chama hiki kwa kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha utakatifu wa maisha ya ndoa na familia; wema, utu wa mwanadamu na uzuri wa maisha; unaofumbatwa katika huduma makini inayotaka kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo sanjari na malezi na majiundo makini katika maisha ya ndoa na familia; dhamana ambayo inapaswa kutekelezwa kwa dhati kabisa na wazazi na walezi.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ni kwa njia ya tunu ya maisha ya kifamilia, watu wanaweza kuonja familia kubwa ya binadamu, ambamo watu wanapaswa kuishi katika umoja, upendo na mshikamano; kwa kusaidiana, kuheshimiana na kuthaminiana kwani kila mmoja wao ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia hazina budi kukuzwa na kudumisha na wote; kwa kuwajibika kulinda na kutunza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; kanuni maadili na utu wema; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anawashukuru kwa namna ya pekee wanachama hawa kwa sadaka na majitoleo yao kwa ajili ya huduma kwa Wakristo wanaoteseka huko Mashariki ya Kati, kutokana na ushuhuda wao kwa Kristo na Kanisa lake. Ni watu wanaouwawa kutokana na vitendo vya kigaidi, misimamo mikali ya kidini na kiimani; kiasi kwamba, wengi wao wamegeuka kuwa ni wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi hata katika nchi zao wenyewe. Msaada wao wa hali na mali ni kielelezo makini cha mshikamano wa upendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.