2017-08-02 14:19:00

Vijana ni jeuri na matumaini ya Kanisa!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi, Jumatano tarehe 2 Agosti, 2017 kuhusu Sakramenti ya Ubatizo kama Mlango wa Matumaini, wakati akizungumza na mahujaji kutoka nchini Poland, amekumbushia hija yake ya kitume, mwaka mmoja uliopita, aliposhiriki kwa kishindo maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani sanjari ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kumwezesha kukutana na kuserebuka na vijana wa kizazi kipya katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Ameonja na kugundua ari na mwamko wa vijana katika maisha ya imani; ameshuhudia jinsi ambavyo Roho Mtakatifu alivyotenda miongoni mwa vijana na jinsi ambavyo anaendelea kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo. Baba Mtakatifu anawashukuru vijana wa kizazi kipya kwa ari na mwamko wa matumaini waliyo nayo!

Baba Mtakatifu amemkumbuka kwa namna ya pekee kabisa Kardinali Franciszek Macharski, ambaye, tarehe 2 Agosti 2016 alifariki dunia. Huyu ni kiongozi mashuhuri sana, aliyejipambanua kama mchungaji mwema, aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya watu wake; akajenga matumaini na kujiaminisha kwa Kristo Yesu, chemchemi ya huruma ya Baba wa milele. Mwishoni, amewataka mahujaji na waamini wote katika ujumla wao kujishikamanisha na Kristo Yesu pamoja na Injili yake. Sherehe ya Kung’ara Bwana, Jumapili ijayo, iwasaidie waamini kuwa na matumaini pamoja na kuendelea kujiaminisha mikononi mwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.