2017-08-02 14:35:00

Papa Francisko: Wanamichezo wawe ni vyombo vya wema na amani duniani!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 2 Agosti 2017 amekutana na kuzungumza na Timu ya Mpira wa miguu ya Borussia kutoka Monchengladbach iliyo mtembelea rasmi mjini Vatican na kuikaribisha kwa mikono miwili. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuishuruku timu hii ambayo imejenga mahusiano mazuri na Shirikisho la Michezo la Wafanyakazi wa Vatican. Pande hizi mbili zimekuwa kizichuana mjini Roma na huko Monchengladbach. Jambo la kutia moyo anasema Baba Mtakatifu ni kuona kwamba, timu hizi zimeendelea kujikita katika utu na heshima ya binadamu; timu ambazo zinasaidia kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kifamilia.

Inafurahisha kuona jinsi ambavyo familia nyingi zinahamasika kwenda kutaza mchezo wa mpira wa miguu wakati timu ya Borussia kutoka Monchengladbach inapojimwaga uringoni. Anawapongeza kwa kubainisha mbinu mkakati wa michezo na elimu kwa ajili ya vijana wa kizazi kipya, hasa zaidi wale vijana wanaotoka katika familia maskini zaidi. Baba Mtakatifu anawahimiza kuendelea kuwekeza katika michezo, ili kweli waweze kuwa ni wanamichezo wa wema na amani, mambo msingi ambayo kwa sasa yanahitajika ulimwenguni! Baba Mtakatifu amewaweka wanamichezo wote hawa chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu na hatimaye, kuwapatia baraka zake za kitume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.