2017-08-02 14:47:00

Frank Habineza Mgombea urais na Kagame Rais wa sasa wa Rwanda


Zimesalia siku mbili za uchaguzi Mkuu  wa rais nchini Rwanda  na vyama tisa vinashiriki na rais Paul Kagame wa chama cha RPF. Chama cha Green Party cha Frank Habineza ndicho chama pekee halisi cha upinzani. Uchanguzi Mkuu nchini Rwanda unatarajiwa kufanyika tarehe 4 Agosti 2017. Bwana Frank Habineza amejitosa kugombea  kiti  cha  urais  kwa  mara  ya kwanza  baada  ya  miaka  minane  ya  mapambano ili  kuweza kukiandikisha chama chake na kupata nafasi ya  kuingizwa  katika makaratasi  ya  kupigia  kura. Frank Habineza  ni mwanaharakati  wa  kulinda  mazingira anayewania  kuwa  rais  wa Rwanda na    mwenye  umri  wa miaka  40. Ni  kiongozi wa  chama  cha  Green Party ambaye  amekabiliana  na vitisho vya kuuwawa na pia ameshuhudia wanao muunga mkono wakipigwa, wakifungwa jela na  kulazimishwa  kuikimbia nchini  hiyo na  kwenda  kuishi  uhamishoni wakati  akijaribu  kuingia katika uwanja  wa  kisiasa  nchini  Rwanda  ambao  una udhibiti mkubwa.

Bwanan Habineza akiongea na Shirika la habari la Ufaransa la AFP katika  mahojiano  kwenye  ofisi yake katika  mji  mkuu  Kigali, ambako  walinzi  wake wana  ulizni mkali, amesema imekuwa ni safari ngumu na pia safari ya hatari. Historia fupi ya maisha yake ni kwamba, alizaliwa  uhamishoni  nchini Uganda baba  yake  akiwa  ni  Mhutu na  mama  yake  Mtutsi, alirejea  nchini Rwanda na  kusomea masuala  ya  utawala. Pia  alianza  kuwa mwanaharakati  wa  asasi za  kijamii , akifanya  kampeni  ya  ulinzi  wa  mazingira. Habineza  alikuwa  mwanachama  wa  chama  utawala  cha Rwandan Patriotic Front RPF lakini  akajitoa  na  kujiunga  na  siasa za  upinzani  mwaka 2009 ili  kuweza  kuwa  na  chama  mbadala kwa  chama  tawala  ambacho kinatawala  kwas asa.

Katika kampeni za uchaguzi  Rais  Paul Kagame  amekuwa  akishutumiwa  kwa  kuzuwia  uhuru wa  kutoa  mawazo  na  kuzuia  vyama  vya  upinzani. Mbali  na chama  cha  Habineza  cha  Green Party, hata hivyo vyama  vyote vya upinzani  vilivyosajiliwa  vinamuunga  mkono  Kagame. Akiendelea na mahojiano hayo  amesema walipo anzisha  chama  walipigwa katika  baadhi  ya  mikutano  yao na  watu  ambao  walikuwa  na  silaha, watu waliwekwa maabusu,walifungwa,wengine walikimbilia  uhamishoni. Chama  chake  kilizuiliwa  usajili  kabla  ya  uchaguzi  wa  mwaka 2010, na  muda mfupi  kabla  ya uchaguzi  mwili  wa  makamu  wa rais  wa  chama  cha  Green  Andre  Rwisereka  ulipatikana  ukiwa umeharibika  kabisa. Habineza , ambaye  anasema binafsi  pia  alipokea  vitisho vya kuuwawa  na aliamua kukimbilia nchi ya  Sweden mwezi  mmoja  baadaye   familia  yake  hatimaye ilipata  uraia.

Historia ya mpanzani wa Rais Kagame inaendelea: mwaka  2012  aliamua  kurejea  nchini  Rwanda. Amesema kumuacha  mkewe na  watoto ikiwa  ni pamoja  na  mtoto  wake wa  kiume  wa   mwaka  mmoja, ilikuwa  kitu  kigumu  sana  ambacho amewahi  kufanya. Lakini Chama  chake  hatimaye kilifanikiwa  kusajiliwa  mwaka  2013, mwezi  mmoja  tu  kabla  ya  uchaguzi  wa  bunge, ambapo Habineza aliamua  kutoshiriki  kutokana  na  ukosefu wa muda  wa matayarisho. Mwaka  2015 alikuwa  mgombea  pekee  kushiriki  katika  kura  ya maoni  ya  mageuzi  ya  katiba  inayomruhusu Kagame  kuwania muhula  wa  tatu madarakani. Habineza  alirejesha  uraia  wa Sweden  ili  kuweza kushiriki  katika  uchaguzi  wa  mwaka  huu 2017 na  ameendelea kukabiliana  na  vikwazo  chungu nzima katika kila  hatua. Mwaka  2016  aliotolewa  kutoka  katika  jengo  la  ofisi  yake  na nyumbani  kwake  bila  kupewa taarifa, aidha  katika kufanya  kampeni  imekuwa  taabu  kwake.

Je atafanikiwa kupata ushindi wa kuwa rais wa Rwanda ?

Sr Angela Rwezaula
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.