2017-07-31 11:19:00

Waziri Mkuu: Tanzania siyo lango la kupitishia dawa za kulevya!


Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Tanzania siyo lango la kupitishia dawa za kulevya kwenda nchi za nje hivyo ameagiza ulinzi uimarishwe katika mipaka yote. Amesema kuna tabia ya baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu kutumia Tanzania kama njia ya kupitisha dawa za kulevya kwa ajili ya kupeleka nchi za Afrika ya Kusini, Malawi na Zambia. Alitoa kauli hiyo Jumamosi, Julai 29, 2017 alipozungumza na watumishi wa kituo cha forodha cha Kasumulu kilicho katika mpaka wa Tanzania na Malawi wilayani Kyela. Waziri Mkuu alisema ili kuhakikisha jambo hilo linadhibitiwa ni vema ukaguzi wa watu wanaopita kwenye maeneo hayo pamoja na mizigo ukaimarishwa. “Endeleeni kufanya upekuzi wa kina wa magari, watu na mizigo yote yote katika mipaka yetu. Tanzania siyo lango la kupitishia dawa za kulevya na Serikali haitakubaliana na jambo hilo.”

Pia aliwataka viongozi hao kuhakikisha biashara zote za magendo zinazifanyika mipakani, zikiwemo za kubadilisha fedha zinadhibitiwa kwa kuwa zinaikosesha Serikali mapato. Alisema ni vema yakawepo maduka ya kubadilishia fedha katika maeneo hayo ili kudhibiti biashara hiyo ambayo kwa sasa inafanywa kimagendo huku Serikali ikikosa kodi. “Biashara za magendo zidhibitiwe katika maeneo haya na yaanzishwe maduka ya kubadilishia fedha ili biashara hiyo ifanyike kihalali. Pia imarisheni vyanzo vya mapato.”

Pia Waziri Mkuu aliwataka Maofisa wa Uhamiaji katika mikoa hiyo ya mipakani kuhakikisha wanadhibiti uingiaji holela wa raia wa kigeni kwa lengo la kuimarisha ulinzi nchini. Waziri Mkuu alisema katika baadhi ya maeneo kwa sasa zimeanza kuonekana silaha ambazo hapo awali hazikuwepo na ndizo zinazosadikiwa kutumika katika matukio ya kihalifu.

Awali, Bw. Taniel Magwaza ambaye ni Afisa Mfawidhi wa Uhamiaji alisema watahakikisha wanafanya kazi kwa weledi katika kupambana na biashara za magendo kwenye mpaka huo. Alisema mbali na kupambana na biashara za magendo pia watadhibiti uingiaji wa wahamiaji haramu kwa kushirikiana na watumishi idara zote waliopo katika mpaka huo wa Kasumulu. Bw. Magwaza alisema katika doria zilizofanywa mwaka 2016/2017 jumla ya wahamiaji haramu 87 walikamatwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. Alisema wahamiaji hao walitokea nchi za Malawi (30), Ethiopia (47), Burundi (6) Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) (4), ambapo baadhi walirudishwa makwao na wengine walifungwa katika Gereza la mkoa wa Mbeya.

Waziri Mkuu wa Tanzania azindua meli mbili zilizotengenezwa na mtanzania: Aonya zisitumike kuvushia wahamiaji haramu na dawa za kulevya

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua meli mbili za mizigo za Mv Njombe na Mv Ruvuma zitakazotumika katika kusafirishia mizigo kwenye ziwa Nyasa na kuonya kwamba zisitumike kama eneo la kuvushia wahamiaji haramu na dawa za kulevya. Amesema kukamilika kwa ujenzi wa meli hizo zilizogharimu sh. bilioni 11.253 ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Dkt. John Magufuli alizozitoa katika ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 kwa lengo la kutatua changamoto ya usafiri wa abiria na mizigo katika ziwa Nyasa. Amesema ni jambo la faraja na la kujivunia kwa Serikali na wananchi kwa pamoja kushuhudia meli zilizotengenezwa na Mtanzania, zikiwa zimekamilika tayari kwa kuanza kazi ya kuwahudumia wananchi, ambapo awali suala hilo lilikuwa likifanywa na raia wa kigeni.

Waziri Mkuu amezindua meli hizo zilizojengwa na kampuni ya Kitanzania ya M/S Songoro Marine Transport Jumamosi, Julai 29, 2017) katika bandari ya Kiwira wilayani Kyela akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mbeya.  Amesisitiza kwamba meli hizo zitumike katika kukuza uchumi wa wananchi kwa kusafirisha mizigo na biashara halali kati ya nchi za Tanzania na Malawi na zisitumike kama eneo la kuingiza wahamiaji haramu pamoja na dawa za kulevya nchini.

Waziri Mkuu amewataka wananchi wa maeneo hayo kuwa walinzi na kuhakikisha meli hizo zifanya shughuli halali za kiuchumi ambazo zitawaletea tija wao na Taifa kwa ujumla na kamwe wasikubali zikatumika kama kichaka cha uhalifu. “Changamoto ya usafiri wa mizigo katika ziwa Nyasa itakuwa historia kwani meli hizi zitarahisisha usafiri na kupanua wigo wa biashara kati ya Tanzania nan chi za Malawi na Msumbiji, hivyo tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli kwa kutoa ahadi hii ambayo leo utekelezaji wake umekamilika.”

Awali,Naibu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Karim Mataka alisema ujenzi wa meli hizo ulianza Juni 2015 zina uwezo wa kubeba tani 1,000 za mizigo kwa kila moja. Mhandisi huyo alisema mbali na kukamilika kwa mradi huo pia TPA imeingia mkataba na kampuni ya M/S Songoro Marine Transport Ltd kwa ajili ya ujenzi wa meli ya abiria yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 300 za mizigo. Mradi huo ambao upo katika hatua za mwisho kamilika utagharimu sh. bilioni 9.12.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.