2017-07-31 08:15:00

Papa Francisko: Wekezeni katika Ufalme wa Mungu na Kristo Yesu!


Mwinjili Mathayo amefanikiwa kukusanya mifano saba ya Yesu katika Sura ile ya 13, ambayo inahitimishwa na mifano kuhusu ufalme wa Mungu, unaofananishwa na hazina iliyofichika, lulu yenye thamani kubwa na wavu uliotupwa baharini. Lakini mifano miwili ya kwanza inachukua uzito wa pekee kwani inawahusisha wadau wakuu, kufanya maamuzi mazito katika maisha yao, ili kupata ile hazina iliyofichika na lulu yenye thamani kubwa. Wahusika hawa waliamua kuwekeza katika mchakato wa kutafuta hicho ambacho wamekigundua kuwa kina thamani kubwa sana maisha mwao, bila kuogopa hatari ambazo wangeweza kukutana nazo mbeleni!

Haya ni maamuzi mazito yanayofumbatwa katika utafiti wenye kina na sadaka ya maisha. Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 30 Julai 2017 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kimsingi Ufalme wa Mungu umetolewa kwa ajili ya watu wote, lakini unahitaji mtu kujihusisha kikamilifu ili kuweza kuupata na wala hapa si “maji kwa glasi” anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Watu hawana budi kujishughulisha, kutembea na kufanya tafiti za kina, huku moyo ukiwaka shahuku ya kutaka kuifikia hazina iliyofichika, yaani Ufalme wa Mungu ambao umemwilishwa kwa njia ya Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu anasema, Yesu ndiye ile hazina iliyofichika na ndiye ile lulu yenye thamani kubwa, kwa mwamini anayemgundua katika maisha yake, anaweza kupata mageuzi makubwa katika maisha yake, kwa kuyapatia maana kubwa zaidi. Yule mkulima na mfanya biashara waligundua kwamba, mbele yao walikuwa na nafasi adhimu, ambayo hawakutana waiachilie hivi hivi ndiyo maana wakaamua kuuza vyote walivyokuwa navyo, ili hatimaye, waweze kuwekeza katika kununua hazina iliyofichika na lulu yenye thamani kubwa!

Hii ni sadaka kubwa inayowataka kufanya maamuzi ya kina kwa kutoa kipaumbele cha kwanza na cha pekee kabisa, kwa mambo yenye thamani kubwa katika maisha. Waamini wanapofanikiwa kukutana na Kristo Yesu katika maisha yao anasema Baba Mtakatifu Francisko, wanapaswa kutoa sadaka kwa mambo mengi, kwa kumpatia Kristo Yesu, kipaumbele cha kwanza katika maisha. Ikumbukwe kwamba, mfuasi wa Yesu ni yule ambaye amebahatika kupata mambo msingi katika maisha yake, ikiwa ni pamoja na utimilifu wa furaha inayotolewa na Yesu peke yake katika maisha ya binadamu. Hiyo ndiyo ile furaha ya wagonjwa waliogangwa na kutibiwa na Yesu;  wadhambi waliosamehemewa na kupatanishwa na Mungu pamoja na jirani zao; au yule mwizi aliyetubu na kufunguliwa mlango wa Paradisi. Baba Mtakatifu anasema, furaha ya Injili inaujaza moyo wa mwamini maisha tele, kwa wale wanaobahatika kukutana na Kristo Yesu katika maisha yao; wale watu wanaothubutu kumwachia Kristo Yesu nafasi katika maisha yao, ili aweze kuwaokoa na lindi la dhambi na mauti; hofu, wasi wasi na utupu wa moyo pamoja na upweke hasi unaoweza kumtumbukiza mtu katika “sonona ya maisha ya kiroho”.

Kwa njia pamoja na Yesu, daima furaha inapyaishwa katika maisha ya waamini. Kumbe, waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanahamasishwa na Baba Mtakatifu Francisko kutafakari kwa kina na mapana ile furaha ya mkulima na mfanyabiashara wanaozungumziwa katika Injili ya Jumapili ya XVII ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa. Hii ndiyo furaha kwa kila mwamini anapogundua uwepo na faraja ya Kristo Yesu katika maisha yake. Huu ni uwepo unaoleta mabadiliko katika moyo na kuwawezesha waamini kufungua nyoyo zao kwa ajili ya kuwakirimia jirani zao, hasa wale maskini na wahitaji zaidi katika maisha. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Bikira Maria, awasaidie ili kila mmoja wao aweze kushuhudia kwa maneno, lakini kwa njia ya matendo ya kila siku ile furaha ya kupata ile hazina ya Ufalme wa Mungu, ambao ni upendo wa Baba wa milele aliowazawadia waja wake kwa njia ya Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.