2017-07-31 08:59:00

Papa Francisko: Biashara ya binadamu na utumwa mamboleo ni uhalifu!


Baba Mtakatifu Francisko, mara tu baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 30 Julai 2017 amekumbushia kwamba, hii ilikuwa ni Siku ya Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu Duniani, iliyoanzishwa na Umoja wa Mataifa ili kusaidia juhudi za kimataifa za kugaribisha athari za biashara hii katika maisha na utu wa binadamu. Kila mwaka kuna mamilioni ya watu wanaotumbukizwa katika mifumo ya utumwa mamboleo, hususan katika kazi za suluba, utalii wa ngono na biashara haramu ya viungo vya binadamu. Kashfa hii imeanza kuzoeleka kati ya watu, kiasi kwamba, inaonekana kuwa ni jambo la kawaida katika maisha. Lakini, huu ni ukatili dhidi ya utu na heshima ya binadamu.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwaalika wadau mbali mbali kujizatiti katika mapambano ya utumwa mamboleo na mifumo yake yote. Baba Mtakatifu amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kumwomba Bikira Maria ili aweze kuwasaidia waathirika wa biashara haramu ya binadamu na asaidie mchakato wa toba na wongofu wa ndani, wale wote wanaojihusisha na biashara hii haramu!

Hivi karibuni, Askofu mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, wakati akichangia hoja kuhusu mjadala wa biashara haramu ya binadamu katika maeneo yenye vita, kazi za suluba, utumwa mamboleo pamoja na mifumo yake alisema, biashara haramu ya binadamu na viungo vyake sanjari na mifumo yote ya utumwa mamboleo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu; ni kashfa kubwa katika ulimwengu mamboleo na ni uvunjaji wa haki msingi za binadamu unaojionesha katika kiwango cha kimataifa kiasi hata cha kugusa sekta ya utalii duniani.

Amewaambia wajumbe wa Baraza kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba, chanzo kikuu kinachopelekea mafuriko ya biashara haramu ya binadamu pamoja na mifumo ya utumwa mamboleo ni umaskini wa hali na kipato; ni dalili za kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema. Watu wanaotumbukizwa kwenye utumwa mamboleo ni wale wanaokabiliwa pamoja na mambo mengine na baa la ujinga, ukosefu wa fursa za ajira au majanga asilia yanayowafanya kutafuta kwa udi na uvumba: hifadhi, usalama na matamanio ya maisha bora zaidi.

Katika ujumbe wake kwa Siku ya Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu Duniani kwa mwaka 2017, Bwana Yury Fedotov, Mkurugenzi mtendaji wa UNODC “United Nations Office on Drugs and Crime”, yaani “Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia dawa na uhalifu, iliyoanzishwa kunako mwaka 1997 ili kukabiliana na changamoto mamboleo za: rushwa, uhalifu na ugaidi wa kimataifa anasema, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kushikamana katika kuwalinda na kuwahudumia waathirika wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.

Anasema, kuna uhusiano mkubwa kati ya vita, ghasia, biashara haramu ya binadamu pamoja na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Makundi ya wahalifu wa kimataifa wameendelea kupandikiza mbegu ya chuki na uhasama kati ya watu na hivyo kusababisha vita, ghasia na mipasuko ya kisiasa hali ambayo inapelekea makundi makubwa ya watu kuzihama na kuzikimbia nchi zao wenyewe.

Wakati huo huo, Shirika la Kimataifa la Wahamiaji, IOM, linasema, wahamiaji wanakabiliwa na changamoto mbali mbali katika maisha yao. Ni watu wanaotaka kuboresha maisha yao: kiuchumi, kijamii na kisiasa. Wao ni sehemu ya sura mpya ya mchakato wa wimbi kubwa la utandawazi duniani; ni watu wenye: matumaini, ujasiri na ushupavu kiasi kwamba, wanaweza kutumika kama mashuhuda na vyombo ya amani kwa kutangaza na kushuhudia kwamba, binadamu wote wanaunda familia moja kubwa ya binadamu.

Shirika la Kimataifa la Wahamiaji linafafanua kwamba, biashara haramu ya binadamu inaendelea kushamiri sana duniani kutokana na wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi. Biashara hii Barani Afrika inakadiriwa kufikia kiasi cha dola za kimarekani milioni 400 kwa mwaka. Ni fedha inayolipwa kwa wafanyabiashara haramu kwa njia ya gharama za usafiri jangwani na baharini sanjari na kazi za suluba ughaibuni. Hawa ni watu kutoka: Somalia, Sudan ya Kusini, Eritrea, Mali. Senegal, Gambia, Chad, Niger na Nigeria na wengine ni wale wanaotoka Bangaladesh.

Huu ni ushahidi tosha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa bado haijafanikiwa kudhibiti kwa ukamilifu biashara haramu ya binadamu pamoja na utumwa mamboleo. Rais Sergio Mattarella wa Italia anasema, ni jambo lisilokubalika kuwapatia ufunguo wa matumaini ya wahamiaji Barani Ulaya mikononi mwa wafanyabiashara haramu ya binadamu. Hatima ya wahanga wa biashara haramu ya binadamu ni kifo. Uhalifu dhidi ya ubinadamu unaweza kuvaliwa njuga kwa kuwekeza zaidi katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, unaofumbatwa katika ushirikiano wa kimataifa.

Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kudhibiti biashara haramu ya silaha inayoendelea kusababisha machafuko katika maeneo mengi ya dunia, ili kujipatia faida inayonuka damu ya watu wasiokuwa na hatia. Jitihada hizi hazina budi kwenda sanjari na kuwasaka na hatimaye, kuwatia mikononi mwa sheria wale wote wanaojihusisha na mtandao wa biashara haramu ya binadamu katika hatua mbali mbali. Umefika wakati wa kusikiliza na kujibu kwa vitendo kilio cha watu wasiokuwa na hatia, wanaotumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo anasema Rais Sergio Mattarella wa Italia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.