2017-07-31 10:05:00

31 Julai 2017 Siku ya Mashahidi na Wafiadini wa Makanisa ya Mashariki


Yesu aliwaambia mitume wake kwamba, anawatuma kama kondoo kati ya mbwamwitu, hivyo walipaswa kuwa na busara kama nyoka na wapole kama hua, kwani huko duniani, watakiona cha mtema kuni! Kutakuwa na kinzani na wengi watawachukia kwa sababu ya jina lake. Lakini, aliwakumbusha kwamba, wale watakaovumilia hadi mwisho, hao ndio watakaookoka. Matumaini ya Kikristo ni nguvu ya mashuhuda na waungama imani. Yesu alipowachagua na kuwatuma wafuasi wake, hakuwahakikishia mafanikio ya chapuchapu kama maji kwa glasi!

Kristo Yesu, aliwaonya na kuwaambia kwamba, utangazaji, ushuhuda na ujenzi wa Ufalme wa Mungu una magumu na changamoto zake; kwani watachukiwa kwa sababu ya jina lake. Hili ni jambo la kushangaza sana kwani Wakristo wanapenda kwa asili, lakini daima wanachukiwa sana. Imani thabiti inashuhudiwa katika mazingira kinzani na hatarishi! Kutokana na mwelekeo huu, Kanisa la Wamaroniti, kuanzia sasa, kila mwaka ifikapo tarehe 31 Julai, wanaadhimisha Siku ya Mashahidi wa Imani kwa Makanisa ya Mashariki.

Huu ni mwendelezo wa maadhimisho ya Mwaka wa Mashahidi wa Imani na Wafiadini unaoadhimishwa na Kanisa la Wamaroniti, mwaka uliotangazwa na Patriaki B├Ęchara Boutros Rai, mapema mwaka 2017 na hatimaye, kuidhinishwa na Serikali ya Rais Michel Aoun wa Lebanon. Ni kipindi cha kusali, kutafakari na kusikiliza shuhuda za maisha ya wafiadini ambao wanazidi kuongezeka kila kukicha kutokana na dhuluma, nyanyaso na vitendo vya kigaidi! Mwaka wa Mashahidi wa Imani na Wafiadini utafungwa rasmi tarehe 2 Machi 2018.

Siku hii ni matunda ya mageuzi ya Kiliturujia yaliyofanywa katika maadhimisho ya Sinodi ya Kanisa la Wamaroniti hivi karibuni. Maaskofu walikumbuka: mateso, mahangaiko na ushuhuda wa imani thabiti ulioneshwa na wafiadini pamoja na mashuhuda wa imani kutokana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii huko Mashariki ya Kati. Maadhimisho ya Mwaka huu, ni fursa na mwaliko kwa waamini kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; ili hatimaye, upendo, amani, mshikamano na umoja kati ya watu, viweze kutawala akili na nyoyo za watu dhidi ya vita, chuki, ubaguzi na hali ya kutaka kulipizana kisasi. Ni mwaka unaopania kufutilia mbali woga na wasi wasi usiokuwa na mashiko katika maisha na vipaumbele vya watu, licha ya dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo huko Mashariki ya Kati; ambao wengi wao walilazimika kuyakimbia makazi yao ili kusalimisha maisha yao. Maadhimisho haya yamekwenda pia sanjari na maadhimisho ya Siku ya Vijana nchini Lebanoni, yaliyofanyika kuanzia tarehe 13-23 Julai 2017 kwa kuwashirikisha vijana kutoka ndani na nje ya Lebanoni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.