2017-07-29 10:03:00

Uchaguzi mkuu nchini Kenya 2017: Sifa kuu za viongozi wanaotakiwa!


Demokrasia ni mfumo wa utawala unaozingatia kanuni, maadili pamoja na utendaji unaojali utu, heshima, ustawi na mafao ya wengi. Ili kukuza na kudumisha demokrasia ya kweli, wananchi wanapaswa kuwa makini katika mchakato mzima wa kupiga kura, ili serikali iliyoko au itakayoingia madarakani iweze kuwajibika kwa wananchi wake kwa kuzingatia haki msingi za binadamu na utawala wa sheria. Serikali ndiye mhusika mkuu katika kufanikisha dhana ya utawala bora. Misingi ya utawala bora inafumbatwa kwa namna ya pekee kabisa, katika chaguzi huru na za haki; mfumo huru wa mahakama na utawala wa sheria; uhuru wa mawazo na vyombo vya habari; mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma. Utawala bora daima unapania kuwekeza katika huduma muhimu za kijamii; kwa kuwashirikisha wananchi katika kutoa maoni na utekelezaji wake. Ni utawala unaojikita katika uwajibikaji, usawa na kazi ya ufanisi katika utekelezaji wake.

Homa ya uchaguzi mkuu nchini Kenya inaendelea kupanda na kushuka!Uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika hapo tarehe 8 Agosti 2017, hii ni siku ya kusuka au kunyoa! Familia ya Mungu nchini Kenya haina budi kujiandaa kikamilifu katika utekelezaji wa haki hii msingi itakayowawezesha wananchi kuchagua serikali ya watu inayotokana na ridhaa ya watu ili iweze kuwatumikia wananchi wa Kenya bila ubaguzi wa kidini, kikabila au kimajimbo! Wananchi wanataka serikali ya watu kwa ajili ya watu!

Ili kufanikisha azma hii, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya limetoa sifa za viongozi wanaoweza kuchaguliwa na wananchi ili kusaidia mchakato wa kuwaletea maendeleo endelevu! Wananchi wataweza kuchagua viongozi bora iwapo tu, watashiriki katika mchakato mzima wa uchaguzi na hatima yake ni kupokea matokeo kwa amani na utulivu! Hii inatokana na ukweli kwamba, chaguzi kadhaa nchini Kenya zimepelekea mpasuko wa kijamii ambao mara nyingi umetishia: umoja na mafungamano ya kijamii nchini Kenya.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linawataka wananchi kuwachagua viongozi wachamungu, waadilifu; watu wanaoheshimu na kudumisha haki msingi za binadamu! Kenya inawahitaji viongozi watakaosimama kulinda kutetea na kuendeleza utu wa binadamu, umoja, upendo na mshikamano kati ya wananchi wote wa Kenya; viongozi wanaosimama kidete kulinda na kutetea kanuni maadili, utu wema na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Kenya inahamu ya kuona viongozi wanaoheshimu utawala wa sheria, amani na utulivu; watu wanaotaka kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maendeleo, ustawi na mafao ya wengi; viongozi wanaowajibika mbele ya wananchi waliowapatia ridhaa ya kuwaongoza; viongozi wanaoweza kuwajibishwa na wananchi pale wanaposhindwa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa umma.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linakaza kusema, ukabila, udini, umajimbo au chama cha kisiasa ni mambo ambayo hayana mashiko wala mvuto kwa ustawi na maendeleo ya wananchi wa Kenya! Wananchi wanataka viongozi watakaochaguliwa wawe ni watu waliojipanga kusongesha mbele gurudumu la maendeleo ya wananchi wa Kenya katika ujumla wao; watu wanaojikita katika majadiliano ili kuomba kura na ridhaa ya kuwaoongoza Wakenya; viongozi wanaotaka maendeleo ya wengi.

Kwa upande mwingine, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linataka wananchi kutowachagua wala kuwapatia ridhaa ya kuwaongoza watu wenye uchu wa mali na madaraka wanaotumia: chuki, uhasama na mipasuko ya kijamii ili kujijenga kisiasa, tayari kuokota kura! Wasiwachague viongozi ambao wananuka damu ya watu; wanaopepeta mdomo kwa kueneza chuki; vitisho; viongozi wanaotaka kuwagawa watu, hatimaye kupata kura kwa ajili ya kula! Wala rushwa na mafisadi ni viongozi wanaopaswa kuogopwa kama ugonjwa wa “Ebola”. Viongozi wanaojinufaisha kwa kutumia mgongo wa maskini na wanyonge wanapaswa kuogopwa. Wananchi wasiwachague viongozi wanaotaka kujijenga kiuchumi ili kulinda masilahi yao binafsi. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasema, uchaguzi mkuu unafanyika kila baada ya miaka mitano, kumbe, kila mwananchi ajitahidi kuhakikisha kwamba anatumia vyema kura yake katika uchaguzi huu, kwani ngeli za muda yaani “ningejua” hazitakuwa tena na nafasi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.