2017-07-29 09:36:00

Hazina iliyofichika ni: Ufalme wa Mungu na Kristo Yesu!


Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika kipindi cha Liturujia ya Neno la Mungu, tunapoendelea kutafakari kuhusu Ufalme wa Mungu ambao uko mbele yetu, lakini ni hazina ambayo imefichika, kama ambavyo Kristo mwenyewe anatujuza katika Injili ya Jumapili ya XVII ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa. Ufalme huu, umesogezwa karibu sana na Neno wa Mungu aliyemwilishwa na kukaa kati yetu kwake Yeye Bikira Maria. Ni ufalme ambao umetangazwa na kushuhudiwa na Kristo Yesu kwa njia ya maisha, lakini zaidi kwa njia ya Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake. Ni ufalme unaobubujika na kuimarishwa kwa njia ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Ufalme wa Mungu ni Kristo mwenyewe, hazina iliyofichika, inayohitaji uwekezaji wa hali ya juu kabisa, ili kuweza kuipata!

Kwa majuma kadhaa sasa, Mama Kanisa katika hekima na busara yake, ametusaidia kutafakari juu ya Ufalme wa Mungu, kwa kuangalia muundo wake kama ulivyofafanuliwa na Kristo Mwenyewe kwa mfano wa ngano safi na magugu; utakatifu wa maisha na uwepo wa dhambi, kazi inayofanywa na Shetani. Kanisa ni kielelezo makini cha Ufalme wa Mungu, linalowakusanya, wadhambi wanaopaswa kutubu na kumwongokea Mungu na watakatifu walioshinda magumu kwa msaada wa neema na baraka ya Mungu.

Yesu amepembua dhana na wajibu wa Ufalme wa Mungu unaoenezwa kwa njia ya toba na wongofu wa ndani; kwa ushuhuda wenye mvuto na mashiko, unaoyachachua malimwengu kwa harufu ya huruma, upendo na mshikamano. Ameelezea jinsi ambavyo Ufalme huu unaweza kukua na kukomaa licha ya timbwiri timbwiri na vikwazo dhidi ya Ufalme huu, kwa mfano wa mpanzi na mbegu zilivyoangukia katika nyoyo za watu! Ufalme wa Mungu anasema Yesu ni sawa na mbegu ya haradali ni ndogo kuliko mbegu zote duniani, lakini inapokuwa na kukomaa inakuwa ni mti mkubwa wenye kutoa hifadhi kwa viumbe vyote. Ukuaji wa Ufalme wa Mungu wanasema waswahili ni sawa na “mti wa mbuyu, ambao ulianza kama mchicha, lakini ukikomaa, hauwezi kuukumbatia”!

Katika Injili, Yesu anaendelea kufafanua dhana ya Ufalme wa Mungu, ambao ni sawa na hazina iliyofichika, sawa na dhahabu, iliyofichama kwenye tumbo la ardhi, ili kuweza kuipata lazima utafute mtaji na vitendea kazi vya nguvu. Mtaji huu katika maisha ya kiroho ni: Sala, Sakramenti za Kanisa; Toba na Wongofu wa ndani sanjari na matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo makini cha imani tendaji. Ili kuipata hazina hiyo iliyofichika, Yesu anasema, kuna haja ya kuwa na maamuzi magumu, maamuzi machungu kama yale yaliyotolewa na Mkulima pamoja na mfanyabiashara anayesimuliwa kwenye Injili ya leo!

Tumesema, kwa njia ya Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, Yesu mwenyewe ameanzisha Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki na amani; upendo na mshikamano. Huu ndio ukweli wa Fumbo la maisha ya Mungu yanayomwilishwa katika Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, ambamo: imani, matumaini na mapendo, hukua na hatimaye, kukomaa na kuzaa matunda yanayokusudiwa yaani furaha na maisha ya uzima wa milele, pale Kristo Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho. Waswahili wanasema, hakika inalipa kuwekeza katika Ufalme wa Mungu; kwa kujisadaka na kujitoa bila ya kujibakiza! Ikiwa kama mkono, jicho au mguu wako unakuwa ni kikwazo cha kuingia katika Ufalme wa Mungu, Yesu anasema, ukate na kuung’oa. Haya ni mambo mazito yanayohitaji uzito unaostahili!

Ndugu yangu msikilizaji wa Radio Vatican, Ufalme wa Mungu ni hazina ya wokovu wa binadamu, ni maisha ya furaha na uzima wa milele. Hii ni hazina ambayo imetulia tuli kama maji mtungini, haina makeke kama ”ngoma ya mdundiko” ikipita mtaani, hapo ni patashika nguo kuchanika! Ni hazina inayohitaji sadaka na majitoleo endelevu, kwani thamani yake inahifadhiwa katika sakafu ya moyo wa mwanadamu, hadi siku ile Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, atakapomkaribisha mja wake kuingia kwenye Ufalme wake, kwani wao kwa hakika wamebarikiwa! Sharti kuu hapa ni kujikana mwenyewe na kuubeba vyema Msalaba wako wa maisha. Yesu anasema, nenda ukauze vyote ulivyo navyo, kisha njoo unifuate!

Ni jibu la swali la "udaku" lililoulizwa na kijana mmoja mtanashati aliyetaka kufahamu afanye nini ili aweze kuurithi Ufalme wa mbinguni! Kijana akatokomea, hadi Mwinjili Mathayo anamaliza kuandika Injili yake, kijana hakuonekana tena! Hekina na busara ilitakiwa ili kuweza kufanya maamuzi mazito, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu, ambaye ni Hazina na Ufalme wa Mungu. Tunahitaji busara na hekima ili kuchagua mambo msingi katika maisha, kama alivyofanya Mfalme Sulemani, akaomba hekima na Mwenyezi Mungu akamkirimia: fahari, mali na maisha marefu kama jua! Aliomba hekima, ili aweze kuwa hakimu, kwa kuwahukumu watu kwa haki. Hekima ni fadhila ya kimaadili! Tumwombe Mwenyezi Mungu atujalie hekima na busara ya kuwekeza katika maisha, ili hatimaye, tuweze kuipata hazina iliyofichika, yaani Kristo Yes una Ufalme wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.