2017-07-28 15:16:00

Watakatifu ni wasindikizaji wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene!


Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo pamoja na ujumbe wake, Alhamisi, tarehe 27 Julai 2017 wakiwa mjini St. Petersburg, Russia kwa ajili ya kushiriki katika mapokezi ya Masalia ya Mtakatifu Nicola wa Bari, wamekutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Kanisa la Kiorthodox , Moscow na Russia katika ujumla wake. Wametembelea Kanisa kuu Mtakatifu Aleksandr Nevskij, mahali ambapo masalia ya Mtakatifu Nicolas wa Bari yalitunzwa kwa heshima kubwa. Baadaye Kardinali Koch, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Catharina.

Katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa Wakristo kujenga mahusiano ya karibu na Mwenyezi Mungu, kama ilivyokuwa kwa Musa kwani daima, Mwenyezi Mungu anataka kukutana, kutembea na kuishi kati pamoja na watu wake. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, daima wanakuwa katika hali ya utakatifu wa maisha, kwa kufuata na kutekeleza kwa dhati unabii unaotolewa na Manabii wa Mungu kama ilivyokuwa kwa Waisraeli wakati wa Musa. Ili kuweza kuzungumza na Mwenyezi Mungu ana kwa ana, kuna haja ya kujitakasa, tayari kuwa ni chombo cha kutangaza na kushuhudia ukweli kama kielelezo makini cha imani tendaji.

Watakatifu na wafiadini ni vielelezo na mifano bora ya kuigwa katika maisha na maombezi yao. Wanaonesha dira na mwongozo wa kufuata katika maisha kama wafuasi wa Kristo Yesu. Kwa mifano na maombezi yao, wanawasaidia waamini katika mchakato wa kuwa watakatifu, kama kielelezo cha kutangaza na kushuhudia: ukuu, uweza na utakatifu wa Mungu. Kwa kuwaheshimu watakatifu, waamini wanamtukuza na kumwabudu Mwenyezi Mungu katika utakatifu wake, ambao umemwezesha kuwatembelea na kuwatakatifuza waja wake. Watakatifu ni mng’ao wa utukufu wa Mungu.

Ibada ya kuheshimu masalia ya Mtakatifu Nicolas wa Bari inayotekelezwa na Wakristo ambao bado wamegawanyika ni changamoto ya kumwomba asaidie kuganga na kuponya kashfa ya utengano kati ya Wakristo wa Makanisa ya Mashariki na Magharibi. Kwa waamini wa Makanisa haya mawili kuendelea kuonesha Ibada kwa watakatifu hawa ni kielelezo cha utashi wa watu wa Mungu kutaka kuungana tena. Masalalia haya ambayo yamerejeshwa tena kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Nicolas wa Bari, Jimbo kuu la Bari-Bintonto, Italia, Ijumaa, tarehe 28 Julai, 2017 iendelee kuwa ni changamoto kwa Wakristo kusali kwa ajili ya kuombea umoja wa Wakristo, kwa njia ya maombezi ya watakatifu wa Mungu.

Kardinali Kurt Koch amehitimisha mahubiri yake kwa kusema kwamba, watakatifu ambao tayari wameungana huko mbinguni ni waombezi wakuu na wanandani katika hija ya majadiliano ya kiekumene; wanaoweza kusaidia mchakato wa kuwaunganisha Wakristo; dhamana na wajibu wa waamini kujitakasa na kujitakatifuza mbele ya Mungu, ili kweli siku moja, Mwenyezi Mungu aweze kuwatembelea, wakati wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, kielelezo cha Mlima Mtakatifu; ambacho, kilele chake kilitumika kama mahali pa Musa kukutana na kuzungumza na Mwenyezi Mungu uso kwa uso; ili kuwashirikisha uwepo wake mwanana na endelevu; unaofumbatwa katika utakatifu wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.