2017-07-28 14:06:00

Papa Francisko amkumbuka Marehemu Padre Jacques Hamel!


Baba Mtakatifu Francisko tarehe 26 Julai 2017 amemkumbuka kwa namna ya pekee kabisa Padre Jacques Hamel, ambaye pamoja na mashuhuda wengi wa imani wa nyakati hizi, wamepoteza maisha yao kwa ajili ya huduma kwa jirani zao. Huu ni ujumbe wa Baba Mtakatifu uliotundikwa kwenye mtandao wa “Instagram”, kama kumbu kumbu ya mwaka mmoja tangu Padre Hamel alipouwawa kikatili nchini Ufaransa wakati akiadhimisha Ibada ya Misa Takatifu Kwa njia hii, Baba Mtakatifu ameungana na waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufanya kumbu kumbu hii, ambayo imeadhimishwa kwa namna ya pekee Jimbo kuu la Rouen na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa waamini na watu wenye mapenzi mema walioongozwa na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa. 

Katika maadhimisho hayo, kilichojiri zaidi ni urafiki na majadiliano ya kidini. Ibada ya Misa Takatifu imeongozwa na Askofu mkuu Dominique Lebrun, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Rouen, ambalo tayari limeanza mchakato wa ngazi ya kijimbo ili kumtangaza Padre Jacques Hamel, kuwa ni mtumishi wa Mungu na hatimaye, Mwenyeheri. Huyu ni Padre ambaye katika maisha yake ameonesha fadhila ya: uaminifu, udumifu na ukarimu kwa kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani zake. Matunda yanayoonekana baada ya kifo chake mwaka mmoja uliopita ni: urafiki, majadiliano ya kidini, amani na utulivu; upendo na mshikamano. Ni Padre ambaye aliuwawa wakati akiadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu; chemchemi ya upendo na ukarimu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.