2017-07-28 15:33:00

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Barani Asia yaanza kutimua vumbi!


Maadhimisho ya Siku ya 7 ya Vijana Barani Asia, yalitangazwa mara tu baada ya Baba Mtakatifu Francisko kuhitimisha hija yake ya kitume nchini Korea kunako mwaka 2014. Maadhimisho haya kwa Mwaka 2017 yanaongozwa na kauli mbiu “Furaha ya vijana wa Bara la Asia: Kuishi Injili katika wingi wa makabila ya Bara la Asia”. Maadhimisho haya yanafunguliwa rasmi, Jumapili tarehe 30 Julai 2017 na yatafungwa kwa kishindo tarehe 6 Agosti 2017, wakati Mama Kanisa atakapokuwa anaadhimisha Sherehe ya Kung’ara kwa Bwana, inayopania kuwaimarisha mitume, ili kuweza kukabiliana na Kashfa ya Fumbo la Msalaba!

Maadhimisho yamegawanyika katika awamu kuu tatu: awamu ya kwanza ni mkusanyiko wa vijana unaofanyika katika majimbo kumi na moja, yanayounda Kanisa Katoliki nchini Indonesia. Huko vijana wanashirikishana uzoefu na mang’amuzi ya maisha yao ya ujana, kwa kutambua kwamba, ujana ni mali, lakini yote ni tisa, kumi ni fainali uzeeni!  Tarehe 2 - 6 Agosti 2017 vijana wote watakusanyika Jimboni Yogyakarta na hio ndiyo itakayokuwa ni siku ya uzinduzi rasmi wa maadhimisho ya Siku ya Saba ya Vijana Barani Asia. Hiki ni kipindi cha siku tano zinazosheheni: Katekesi, Sala, Liturujia na Ibada ya Misa Takatifu.

Ni muda muafaka kwa vijana Barani Asia kuserebuka katika Kristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha na utume wa vijana katika tofauti zao za msingi, lakini wote wanafungamanishwa na imani moja kwa Kristo na Kanisa lake. Awamu ya tatu, ni majiundo makini yatakayotolewa kwa walezi wa utume wa vijana Barani Asia, ili kuwasaidia na kuwasindikiza vijana katika maisha na utume wao! Maadhimisho haya yatafanyika kuanzia tarehe 6-9 Julai 2017.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia linasema, hizi ni baadhi ya mbinu mkakati wa mchakato wa uinjilishaji Barani Asia. Tema zinazochambuliwa na kupembuliwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Saba ya Vijana Barani Asia. Siku ya kwanza wanajadili kuhusu: Umoja wa vijana wakristo katika wingi wa makabila Barani Asia. Umuhimu wa kuthamini na kusherehekea utofauti wao; kwa kuwa wamoja katika utofauti; kusherehekea Umoja wao na siku ya tano watapembua kuhusu: kuishi na kushirikishana furaha ya Injili. Huu ni muda pia wa kujenga na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene miongoni mwa vijana Barani Asia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.