2017-07-28 14:55:00

Diplomasia ya Kanisa inajikita katika amani, ustawi na mafao ya wengi


Kanisa limekuwa mstari wa mbele kuangalia haki msingi, utu na heshima ya binadamu Ulaya ya Mashariki; Diplomasia inayotekelezwa na Kanisa inajikita katika haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi! Kanisa linapenda kutangaza Injili ya amani katika maeneo yenye: vita, ghasia na mipasuko ya kijamii na kwamba, Vatican bado inaendelea kufuatilia kwa karibu sana machafuko ya kisiasa nchini Venezuela, ili amani na utulivu viweze kurejea tena na hivyo kutoa nafasi kwa wananchi kuendelea na ujenzi wa nchi yao. Majadiliano kati ya Vatican na China pamoja na Vietnam yanazidi kupamba moto!

Haya ni kati ya mambo msingi yaliyojitokeza kwenye mahojiano maalum kati ya Kardinali  Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na Bwana Gianfranco Brunelli, mwandishi wa habari wa “Jarida la Legno”. Kardinali Parolin amekwisha kutembelea Bielorussia, Ukraine na sasa anajiandaa kwenda nchini Russia, ili kuimarisha uhusiano kati ya Ulaya Mashariki na Magharibi, kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Katika historia haya ni maeneo ambayo yamewahi kutembelewa na Papa Gregori XVI pamoja na Papa PIO IX. Mwelekeo wa sasa unaonekana kuitenga Russia kana kwamba, iko katika sayari nyingine kabisa.

Hapa mkazo ni kudumisha mchakato wa haki, amani na ushirikiano wa kimataifa na hivyo kuondokana na mtazamo wa sasa unaoendelea kuitenga Russia kutokana na utaifa usiokuwa na mashiko, hali ambayo inaweza kuhatarisha amani, usalama na mafungamano ya kijamii kimataifa! Mahusiano tenge yanayoendelea kujionesha kati ya Marekani na Russia ni hatari sana kwa usalama wa Jumuiya ya Kimataifa, hasa ukizingatia hali ya sasa ambako kuna Vita Kuu ya Tatu, inaendelea kupiganwa vipande vipande kwa kukolezwa na biashara haramu ya silaha duniani pamoja na masilahi ya nchi husika.

Matokeo yake ni wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu milioni 65 wanaotafuta hifadhi ya kisiasa na kati yao walau asilimia 10% wanataka kupata hifadhi Barani Ulaya. Umaskini kusini mwa Jangwa la Sahara katika kipindi cha miaka thelathini iliyopita umeongezeka maradufu kutoka watu milioni 200 hadi kufikia milioni 400 hali inaonesha kwamba, katika mazingira kama haya ni nadra sana kupata amani na utulivu, ustawi na maendeleo ya wengi. Hapa kunahitajika majadiliano, umoja na mshikamano wa kimataifa unaongozwa na kanuni auni.

Kardinali Parolin anasema, ni mapema mno kumtupia “madongo” Rais Donald Trump wa Marekani anayehitaji muda wa kuweza kujipanga vyema katika kuamua na kutekeleza sera na mikakati ya maendeleo kwa ajili ya watu wake. Ni matumaini ya Vatican kwamba, Marekani pamoja na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa katika ujumla wake, wataendelea kutekeleza sera na mikakati ya Jumuiya ya Kimataifa pamoja na kukabiliana na changamoto mamboleo yaani: utekelezaji wa mpango mkakati wa kupunguza hewa ya ukaa kwa ajili ya kulinda mazingira nyumba ya wote; mapambano ya umaskini duniani pamoja na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya binadamu ifikapo mwaka 2030. Kanisa kwa upande wake, linapenda kujielekeza zaidi katika kuchochea misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu kwa njia ya diplomasia ya amani. Kanisa halitafuti “ujiko” wa kisiasa, kiuchumi wala kiitikadi. Kanisa linapania kudumisha uhuru wa kuabudu, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa njia ya mshikamano wa huruma na upendo, Kanisa linataka kujielekeza zaidi kwa ajili ya kuwahudumia waathirika wa vita, ghasia na mipasuko ya kijamii sehemu mbali mbali za dunia.

Kardinali Parolin anasema, hivi karibuni Chancellor mstaafu wa Ujerumani Helmut Kohl amefariki dunia, lakini ameacha urithi mkubwa sana katika historia ya Umoja wa Ulaya. Ni muasisi wa kuanguka kwa Ukuta wa Berlin na mwanzo wa mchakato wa kuunganisha Ujerumani Mashariki na Magharibi, iliyokuwa imesambaratishwa kutokana na itikadi za kisiasa. Changamoto kwa wakati huu ni kuendeleza umoja na mshikamano miongoni mwa Umoja wa Ulaya. Kinzani za kitamaduni, kidini na kimaadili na kiutu; athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa; utaifa usiokuwa na mashiko zisiwe ni visingizio vya kutaka kuvunjilia mbali Umoja wa Ulaya.

Kardinali Parolin anasema, machafuko ya kisiasa nchini Venezuela hayajapata muafaka wa amani na kwamba, hali bado ni tete baada ya Rais Nicolàs Maduro kuitisha Bunge kwa ajili ya kura ya maoni ili kubadilisha Katiba ya nchi ambayo kimsingi ni sheria mama! Sasa hivi upinzani na sehemu kubwa ya wananchi wanapinga kura hii na tayari kuna maafa yanayoendelea kujitokeza huko nchini Venezuela. Kanisa linaendelea kufuatilia machafuko haya kwa karibu zaidi, ili kusaidia mchakato wa haki, amani na maridhiano kati ya wananchi wa Venezuela.

Kanisa kwa jicho la kichungaji, linapenda kujielekeza zaidi huko China na Vietnam ili kutangaza na kushuhudia Injili ya amani kwa kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana: kitamaduni, kiuchumi na katika maisha ya kiroho, kwa Kanisa kumpeleka Mwenyezi Mungu kwa watu na watu kwa Mwenyezi Mungu. Kanisa linataka uhuru wa kuabudu na wala si upendeleo wa aina yoyote ile, ili kujenga na kudumisha haki, amani na usawa kati ya watu. Kanisa linataka kushiriki katika mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu. Huu ndio mwelekeo wa diplomasia ya Kanisa inayotekelezwa kwa kufanya majadiliano na viongozi wa serikali mbali mbali duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.