2017-07-27 14:57:00

Wazazi na walezi warithisheni watoto wenu imani, maadili na utu wema!


Parokia ya Mtakatifu Anna, iliyoko ndani ya Vatican, Jumatano, tarehe 26 Julai 2017 imeadhimisha kumbu kumbu ya Watakatifu Yoakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria kwa kusali kwa ajili ya kuombea maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, yatakayotimua vumbi kuanzia mwezi Oktoba, 2018 hapa mjini Vatican kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”. Waamini wamesali pia kwa ajili ya kuombea maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 yatakayoadhimishwa nchini Panama kuanzia tarehe 22- 27 Januari 2019 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Tazama mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema”.

Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu, ameongoza Ibada ya Misa Takatifu Parokiani hapo majira ya jioni! Wakati wa Ibada ya Misa ya Asubuhi, Kardinali Angelo Comastri, Mwakilishi wa Baba Mtakatifu kwa mji wa Vatican, katika mahubiri yake alikazia umuhimu wa wazazi kutekeleza dhamana na wajibu wao wa malezi makini pamoja na kusaidisa mchakato wa kurithisha imani, maadili na utu wema kwa watoto wao, changamoto kubwa kwa malezi ya vijana wa kizazi kipya, wanaotaka uhuru usiokuwa na mipaka wala nidhamu.

Bikira Maria aliyazamisha maisha yake katika sala, tafakari na umwilishaji wa Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yake kama inavyojidhihirisha kwenye utenzi wake wa “Magnificat”. Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa ni matunda ya malezi makini yaliyofanywa na wazazi wake Mtakatifu Yoakim na Anna, waliomsaidia katika maisha yake, kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu na upendo kwa jirani.

Kumbe, familia ni kitalu cha imani na miito mbali mbali ndani ya Kanisa; ni kitovu cha uinjilishaji na urithishaji wa imani kwa vijana wa kizazi kipya. Huu ni mwaliko kwa vijana kuwa wepesi kutimiza mapenzi ya Mungu katika maisha yao, kama alivyofanya Bikira Maria kwa kutoa jibu la uhakika; tazama mimi ni mtumishi wa Bwana nitendewe kama unavyosema! Kardinali Angelo Comastri amekumbusha kwamba, tarehe 26 Julai 2017, Kanisa limeadhimisha kumbu kumbu ya miaka 25 tangu Mama Theresa wa Calcutta alipofariki dunia.

Kwa upande wake, Kardinali Lorenzo Baldisseri alikazia zaidi dhamana na nafasi ya wazazi katika kujenga na kudumisha utakatifu wa maisha unaofumbatwa katika ushuhuda makini, kielelezo cha imani tendaji. Jina Anna maana yake ni “neema” inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ndiyo maana Mtakatifu Anna ni msimamizi wa wanawake wajawazito wanaosubiri kujifungua; lakini pia ni faraja kwa wanawake ambao hawakubahatika kupata watoto katika maisha yao. Watakatifu Yoakim na Anna walikuwa ni wachamungu, mfano bora wa familia hata kwa watu wa nyakati hizi.

Katika umaskini, ukimya na huduma kwa Mungu na jirani, wakabahatika kupokea zawadi ya Mungu na kuwa ni wazazi wake Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Kwa njia hii wakashiriki katika mpango mzima wa kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Mwenyezi Mungu. Wazazi na walezi wanakumbushwa dhamana na wajibu wao wa kuhakikisha kwamba wanarithisha imani, mila, desturi na tamaduni njema kwa vijana wa kizazi kipya. Wahenga ni watu muhimu sana kwani wanakumbatia hekima, busara na tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu; mambo wanayopaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya ili waweze kuwajibika barabara!

Lakini, kwa bahati mbaya, ulimwengu mamboleo unaonekana kana kwamba, hauna nafasi kwa wazee kwani umuhimu wa mtu unapimwa kwa kile anachochangia katika mchakato wa uzalishaji na utoaji wa huduma! Matokeo yake ni wazee, kusukumizwa pembezoni mwa jamii, hali ambayo inawafanya vijana wengi kujikuta hawana utambulisho makini katika maisha yao! Hawa ni vijana ambao ni sawa na “daladala” iliyokatika usukani, kiasi cha kukosa mwelekeo sahihi barabarani!

Si haba kuona kwamba, Mama Kanisa anawahimiza watu kuwajali, kuwathamini na kuwaenzi wazee ambao ni hazina ya jamii. Kinachotiliwa mkazo hapa ni utu na heshima ya binadamu; ili kukaza na kudumisha umoja, mshikamano na mafungamano ya kidugu na kijamii. Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa kutoka kifua mbele ili kwenda kuinjilisha pembezoni mwa maisha ya watu kwa kukazia mambo msingi ya maisha; amana ya imani; mafundisho ya Kanisa, Amri za Mungu na maisha ya sala, ili kuzima utupu unaojitokeza kutokana na kelele nyingi na uchafuzi wa mazingira mambo yanayohatarisha amani na utulivu wa watu wengi duniani.

Kardinali Lorenzo Baldisseri anakaza kusema, watu lazima watangaziwe na kushuhudiwa Habari Njema ya Wokovu, kwa lugha rahisi inayopenya masikio na kukita katika akili na nyoyo za watu sanjari na kuhakikisha kwamba, vyombo vya mawasiliano ya jamii ambavyo daima viko katika mchakato wa mageuzi na mabadiliko makubwa vinatumika kufikishia watu ujumbe wa Neno la Mungu. Kinachotakiwa ni ukweli, uhakika na mambo msingi kwani watu hawana nafasi ya kupiga michapo! Wana haraka zao kama yale Mabasi ya mwendo kasi, Bongo! Watu wanataka kusikiliza Habari Njema ya Wokovu, Injili ya Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu na wala si “vijembe, kejeli na matusi”.

Kardinali Lorenzo Baldisseri anaendelea kufafanua kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anatoa kipaumbele cha pekee kwa wazee na wahenga kama mashuhuda na vyombo makini katika mchakato mzima wa malezi na urithishaji wa imani, maadili na utu wema kwa vijana wa kizazi kipya. Wahenga wanayo nafasi ya pekee katika malezi kwa wajukuu wao, kwani wao kwa hakika ni nguzo imara za familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.