2017-07-27 15:34:00

Ushuhuda wa Injili miongoni mwa ulimwengu wa wafanyakazi!


Utu wa mwanadamu ndicho kipimo cha heshima ya kazi na kwamba kazi ni kwa ajili ya mwanadamu na wala si mwanadamu kwa ajili ya kazi. Hii ni changamoto ya kufanya kazi kwa ushirikiano, kwani kazi pia ni wajibu unaopaswa kutekelezwa na binadamu kama sehemu ya ushiriki wake katika mchakato wa kazi ya uumbaji. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa wajumbe wa Chama cha Wafanyakazi Wakristo Duniani (MMTC, WBCA, WMCW) wakati wa mkutano wake huko Avila, Hispania kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Mkutano umeongozwa na kauli mbiu “ Ardhi, Makazi na Ajira kwa ajili ya maisha yenye utu” na kuhudhuriwa na wajumbe 120 kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Mkutano umehitimishwa kwa kutoa Waraka unaowahimiza wafanyakazi Wakristo kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya Kristo katika ulimwengu wa wafanyakazi! Wajumbe wamesikitishwa sana kwa uwepo wa kiwango cha hali ya juu kabisa cha ukosefu wa fursa za ajira hususan miongoni mwa vijana wa kizazi kipya; ukosefu wa kazi zinazoheshimu utu wa binadamu; mahusiano tenge kati ya wafanyakazi na waajiri wao pamoja na wafanyakazi wengi kukosa matumaini ya maisha bora kwa sasa na kwa siku za usoni.

Yote haya yanapelekea wafanyakazi wengi kujikuta wanatumbukia katika magonjwa ya sonona, afya ya akili, mfadhaiko na hatimaye kujikatia tamaa ya maisha. Wajumbe wamefanya upembuzi yakinifu kuhusu mwenendo wa uchumi kimataifa na changamoto ya ukosefu wa fursa za ajira katika ulimwengu mamboleo. Chama cha Wafanyakazi Wakristo Duniani kinasema, dhamana na wajibu wake ni kuendelea kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu katika ulimwengu wa wafanyakazi; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya wafanyakazi, wanaoshiriki katika mpango wa kazi ya uumbaji, ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi binadamu kuiendeleza. Utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ni jambo linalovaliwa njuga na Chama hiki katika sera na mikakati yake ya maisha.

Chama cha Wafanyakazi Wakristo Duniani kinasema, kinapania kuendeleza mchakato wa elimu makini kwa wafanyakazi pamoja na uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa umoja, udugu na mshikamano kwa hali na mali. Imani kwa Kristo na Kanisa lake, Mafundisho Jamii ya Kanisa na Injili ya Kristo ni nyenzo msingi zinazotumiwa na Chama hiki katika kutekeleza sera na mikakati yake katika ulimwengu wa wafanyakazi. Wajumbe wametumia fursa hii kuonesha mshikamano wao wa dhati na wafanyakazi ambao ajira zao ziko mashakani; wale wasiokuwa na fursa za ajira kutokana na athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa; wazee wanaokula pensheni zao bila kuwasahau wafanyakazi wa majumbani, ambao wanatekeleza dhamana kubwa sana katika ustawi na maendeleo ya jamii ya binadamu.

Wafanyakazi Wakristo Duniani wanahamasishwa kujiunga pamoja ili kuweza kukabiliana na changamoto zote hizi kwa imani na matumaini, ili hatimaye, kujenga jamii inayosimikwa katika umoja, udugu, upendo na mshikamano wa dhati! Imekuwa ni fursa pia ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kutimiza Miaka 50 tangu Chama hiki kilipoanzishwa na wakati wote huu, kimeendelea kuwa bega kwa bega na wafanyakazi sehemu mbali mbali za dunia. Wanahamasishwa sasa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Kristo miongoni mwa wafanyakazi sehemu mbali mbali za dunia, ili sauti ya Kanisa iendelee kusikika hata ndani ya ulimwengu wa wafanyakazi. Lengo ni kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Chama Cha Wafanyakazi Wakristo Duniani kitaendelea kujikita katika ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika haki, mshikamano na maendeleo endelevu! Kinataka kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wafanyakazi Wakristo duniani, kama sehemu ya mchakato wa dhamana na utume wake katika uinjilishaji mpya. Wafanyakazi Wakristo wanahamasishwa kuwa kweli ni mashuhuda wa ima ni yao kwa Kristo na Kanisa lake sehemu za kazi. Wawe mstari wa mbele kuhakikisha kwamba, wanamwilisha kwa dhati kabisa Mafundisho Jamii ya Kanisa pamoja na kushirikiana na vyama vingine vya wafanyakazi kwa ajili ya kulinda na kutetea haki msingi za wafanyakazi. Wafanyakazi Wakristo Duniani Wawe mstari wa mbele kupambana na ukosefu wa haki msingi za binadamu, lakini pia watekeleze dhamana na wajibu wao vyema kwa kuzingatia kanuni, sheria na maadili ya kazi. Usawa sehemu ya kazi, utu na heshima ya wafanyakazi ni mambo muhimu sana yanayopaswa kuvaliwa njuga na wajumbe wote mahali popote pale walipo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.