2017-07-27 15:14:00

Uekumene wa sala na maisha ya kiroho una mashiko zaidi!


Mwendelezo wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene miongoni mwa Wakristo ni kujibu changamoto ya Kristo Yesu, kwa wafuasi wake, ili wote wawe wamoja, ili kweli Injili iweze kuwa na nguvu zaidi inaposhuhudiwa na Wakristo wote pasi na migawanyiko; kwa kuondokana na wasi wasi pamoja na mashaka ambayo wakati mwingine yanagumisha majadiliano ya kiekumene. Ni wajibu kwa wakristo waote kujikita katika majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika sala na maisha ya kiroho; katika ushuhuda wa damu na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Wakristo kwa pamoja wanatafuta amani ing’aayo uso wa Mungu; kwa kuwa wapatanishi; watangazaji na mashuhuda wa Injili ya Kristo na Kanisa lake.

Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo pamoja na ujumbe wake, Jumatano, tarehe 26 Julai 2017 wameondoka kuelekea mjini St. Petersburg, Russia kwa ajili ya kushiriki katika mapokezi ya Masalia ya Mtakatifu Nicola wa Bari, anayeheshimiwa na waamini zaidi ya milioni mbili sehemu mbali mbali za dunia. Huu ni ushuhuda wa uekumene wa watakatifu, unaofumbatwa katika ibada kwa watakatifu wa Mungu, fursa makini kwa Makanisa kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene miongoni mwa waamini katika uhalisia wa maisha yao ya kawaida. Inapendeza kuona viongozi wakuu wa Makanisa wakikutana na kusali pamoja, lakini ina mvuto wa pekee kabisa katika maisha na utume wa Kanisa, kuona waamini wa Makanisa mbali mbali wakikutana na kusali pamoja.

Masalia ya Mtakatifu Nicola wa Bari yatarejeshwa nchini Italia, Ijumaa tarehe 28 Julai 2017 na kupelekwa moja kwa moja kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la Bari-Bitonto kwa maandamano makubwa. Baadaye kutafutiwa na Ibada ya Misa Takatifu na hapo, tukio hili la kihistoria, litaandikwa kisheria kwamba, Masalia ya Mtakatifu Nicola wa Bari, yamerejeshwa nchini Italia, tarehe 28 Julai 2017. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Nicola wa Bari anaheshimiwa na Wakristo wa madhehebu mbali mbali ya Kikristo kama mlinzi wa maskini na wale wote wanaonyanyaswa; mlinzi na mtetezi wa watoto na mabaharia. Ibada kwa mtakatifu huyu, imekuwa ni daraja kati ya Makanisa ya Mashariki na Makanisa ya Magharibi.

Masalia ya Mtakatifu Nicola wa Bari yanarejeshwa baada ya mazungumzo ya kiekumene kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Cyril wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Russia nzima, yaliyofanyika nchini Cuba kunako mwaka 2016, kama alama ya udugu na urafiki katika Kristo, ili kwa maombezi ya Mtakatifu Nicola wa Bari, Makanisa haya mawili yaendeleze mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili siku moja, yote mawili yaweze kuwa chini ya Kristo mchungaji mkuu. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Nicola wa Bari anafungamanishwa sana na historia ya Russia na kwamba, sehemu kubwa ya Makanisa nchini humo yako chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu huyu, ambaye pia ni kimbilio la familia nyingi. Ni mshauri wa mambo mazito katika maisha.

Askofu mkuu Francesco Caccuci, wa Jimbo kuu la Bari-Bitonto ambaye pia yuko kwenye msafara huu anasema, tarehe 21 Mei 2017 kulikuwa na bahari ya watu waliojipanga kutoa heshima zao kwa Masalia ya Mtakatifu Nicola wa Bari tangu yalipoanza safari Jimbo kuu la Barti-Bitonto hadi yalipofika  mjini St. Petersburg, nchini, Russia. Hii inaonesha kwamba, licha ya mipasuko ya kitaalimungu, lakini waamini wanaishi katika uekumene wa sala na maisha ya kiroho; mambo msingi yanayotiliwa mkazo na Baba Mtakatifu Francisko mintarafu majadiliano ya kiekumene. Hija hii ya maisha ya kiroho inalenga pia kuimarisha majadiliano ya kiekumene miongoni mwa waamini na Makanisa katika ujumla wake. Kardinali Kurt Koch, pamoja na ujumbe wake wanakutana na viongozi wakuu wa Kanisa la Kiorthodox, Moscow na Russia katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.