2017-07-27 14:36:00

Papa Francisko kuzindua kampeni ya upendo na mshikamano na wahamiaji


Baba Mtakatifu Francisko tarehe 27 Septemba 2017, anatarajiwa kuzindua kampeni ya mshikamano na wahamiaji pamoja na wakimbizi wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Kampeni hii inaratibiwa na Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis kwa kuongozwa na kauli mbiu “Shiriki safari hii” “Share the Journey”. Kardinali Luis Antonio G. Tagle, Rais wa Caritas Internationalis anasema, ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana unasaidia kukuza mchakato wa amani.

Hili ni hitimisho la barua ambayo ameyandikia Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki kitaifa na kimataifa, kushiriki kikamilifu katika kampeni hii itakayozinduliwa kwenye kumbu kumbu ya Siku kuu ya Mtakatifu Vincent wa Paolo, Baba wa maskini sanjari na maadhimisho ya Jubilei ya miaka 400  ya Shirikisho la Vyama vya Upendo Kimataifa, lililoanzishwa na Mtakatifu Vincent wa Paulo. Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kujisadaka zaidi kwa ajili ya kuwasaidia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kuwajengea uwezo na kuwapatia matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Lengo kuu la kampeni hii anasema, Kardinali Luis Antonio G. Tagle ni kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana, ili kufahamiana na hatimaye, kusaidiana kwa hali na mali. Ni kampeni inayofumbata mchakato mzima wa safari ya wahamiaji na wakimbizi kutoka katika nchi zao za asili; wanapokuwa njiani na hatima ya safari yao ya matumaini. Ni vyema waamini na watu wote wenye mapenzi mema wakawa na ufahamu mpana wa mambo msingi yanayopelekea makundi ya watu kuhama nchi zao. Ni wakati kwa mashirika 165 ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa kuunganisha mikono na nyoyo zao ili kuwasaidia wahitaji zaidi.

Shirikisho la Vyama vya Upendo Kimataifa ni matunda ya wema na huruma unaobubujika kutoka katika sakafu ya moyo wa Mtakatifu Vincent wa Paulo aliyejisadaka kwa ajili ya maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa njia hii, Mtakatifu Vincenti wa Paulo alitaka kuutafakari wema na huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu, kwani kwake maskini walikuwa kama wawakilishi wa Yesu na sehemu ya Fumbo la mwili wake, yaani Kanisa. Alitambua kwamba, maskini ni amana na utajiri mkubwa wa Kanisa, hata wao pia wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Kanisa kwa kulisaidia kumwongokea Mwenyezi Mungu.

Mambo yote haya anasema Baba Mtakatifu Francisko ni sehemu ya utashi wa Mungu kwa mwanadamu, yaani ni upendo unaopaswa kumwilishwa katika maisha ya binadamu, ili kumletea maendeleo endelevu: kiroho na kimwili. Maisha yanayofumbatwa katika imani kwa Kristo na Kanisa lake, yawasaidie waamini kutambua uhalisia wa maisha, utu na heshima ya binadamu; matatizo na changamoto anazokabiliana nazo: kijamii, kisiasa na kiuchumi na kumthamini kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Waamini wanakumbushwa kwamba, wanawajibika kuwasaidia na kuwahudumia jirani zao, changamoto inayobubujika kutoka katika Fumbo la Umwilisho! Hapa, Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai aliyejinyenyekesha katika mambo yote na kuwa sawa na binadamu, isipokuwa hakutenda dhambi. Aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili aweze kuwainua maskini na wanyonge kutoka mavumbini, matendo makuu ya Mungu, mwaliko kwa Mama Kanisa kuyaendeleza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu. Ukombozi wa mwanadamu na maendeleo endelevu ni sehemu muhimu sana ya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili sanjari na kujizatiti katika kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu, kiini cha wito na muungano wake na Mwenyezi Mungu.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu imekuwa ni fursa kwa Mama Kanisa kuwaendea walimwengu ili kuwapelekea wema, huruma na upole wa Mungu, changamoto kwa waamini kuendeleza mchakato huu anasema Baba Mtakatifu Francisko. Uaminifu wa Kanisa unafumbatwa kwa namna ya pekee, katika upendo wenye huruma unaowafunuliwa watu matumaini. Ni uaminifu unaofumbatwa katika ushuhuda wa mtu binafsi kwa kukutana na Kristo Yesu pamoja na kuwapatia maskini nafasi ya kumwona Kristo katika maisha yao. Kwa kukita mizizi ya maisha ya kiroho kwa Kristo Yesu, waamini wanaweza kusaidia mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa huruma unaopyaisha mioyo ya watu kutoka katika undani wao na kuwawezesha kuwa na mang’amuzi mapya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.