2017-07-26 14:39:00

Miaka 50 ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene ndani ya Kanisa!


Mwenyeheri Paulo VI, katika maisha na utume wake, alijipambanua zaidi kuwa ni mjumbe na chombo cha amani ambalo ni jina jipya la maendeleo endelevu ya binadamu; kiongozi aliyejikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili kuweza kuunganisha yale yaliyowagawa Wakristo kunako mwaka 1054, tayari kuanza kuandika ukurasa mpya wa majadiliano ya kiekumene unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha ya sala na huduma kwa watu wa Mungu. Alikuwa ni kiongozi shupavu na jasiri aliyethubutu kurejea tena mjini Costantinopoli, baada ya kuyoyoma karne kumi na mbili! Hapa si haba! Yataka ushupavu wa kiinjili ulioshuhudiwa kati ya tarehe 26 – 27 Julai 1967.

Patriaki Athenagora wa Kanisa la Costantinopoli kunako tarehe 25 – 26 Oktoba, 1967 “akatinga timu” mjini Roma na kusali kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Huo ukawa ni mwanzo wa mchakato wa mwendelezo wa majadiliano ya kiekumene, uiobuniwa na kuasisiwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ukavaliwa njuga kwa namna ya pekee na Mwenyeheri Paulo VI. Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake anaendelea kukazia umuhimu wa uekumene unaofumbatwa katika: Sala na maisha ya kiroho; katika huduma na ushuhuda wa damu, kielelezo cha imani kwa Kristo na Kanisa lake.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Costantinopoli katika tahariri yake kwenye Gazeti la L’Osservatore Romano, kama sehemu ya kumbu kumbu ya miaka 50 tangu Patriaki Athenagora wa Kanisa la Costantinopoli alipotembelea kwa mara ya kwanza na kusali kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa mwaliko wa Mwenyeheri Paulo VI,  anasema viongozi hawa kwa pamoja walipania kuanzisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili kuweza kuunganisha tena yale yaliyowatenganisha kunako mwaka 1054.

Juu ya lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kuna maneno ya kilatini ambayo pengine kutokana na haraka za mahujaji kuingia Kanisani humo hawayatilii maanani sana! Kumeandikwa hivi “Kwa ajili ya upatanisho na umoja kamili kati ya Kanisa la Kiorthodox na Kanisa Katoliki, ndani ya Kanisa hili, Patriaki Athenagora na Mwenyeheri Paulo VI walikutana na kusali pamoja tarehe 26 Oktoba 1967”. Hii ni changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kusali kwa ajili ya umoja wa Kanisa, ili Wakristo wote waweze kuwa chini ya Kristo mchungaji mwema!

Lakini, ikumbukwe kwamba, tukio hili la kihistoria lilitanguliwa kwa viongozi hawa wawili wa Makanisa kukutana na kusali pamoja mjini Phanar, mwezi, Julai 1967. Mwenyeheri Paulo VI akiwa kwenye Kanisa la Mtakatifu Gregory, alisikika akisema, kwa mwanga wa upendo wao kwa Kristo Yesu; na upendo wa kidugu walionao wao kwa wao; wanaendelea kutambua kitovu cha imani yao na kwamba, mambo yanayowagawa na kuwatenganisha, hayawezi kamwe kuzuia mang’amuzi haya ya umoja wa Wakristo!

Patriaki Athenagora kwa uapande wake, alikazia kuhusu dhamana ya viongozi wa Makanisa kuunganisha kile kinachowatenganisha, kwa kuhimiza kazi za kikanisa pale inapowezekana; kwa kujikita katika kanuni ya imani na uongozi wa Kanisa, ili kutoa dira na mwongozo kwa wanataalimungu kuanza mchakato wa ujenzi wa Jumuiya ya Kikristo iliyo thabiti zaidi; inayosimikwa katika kanuni ya imani, uhuru wa mawazo ya kitaalimungu yanayobubujika kutoka katika amana na urithi wa Mababa wa Kanisa; hazina inayohifadhiwa kwenye Makanisa ya Kikristo!

Mchakato wa majadiliano ya kiekumene anasema Baba Mtakatifu Francisko unaendelezwa na kudumishwa kwa njia ya watu kukutana na kuzungumza kwa pamoja; kukutana na kusali na kuombeana; kwa kujenga madaraja ya huduma na ushuhuda wa Kikristo unaofikia utimilifu wake kwa kumwaga damu, lakini zaidi kwa njia ya upendo kwa Mungu na jirani! Patriaki Athenagora na Mwenyeheri Paulo VI walikutana kwa mara ya kwanza kabisa tarehe 5-6 Januari, 1964 tangu mpasuko wa Kanisa kutokea mwaka 1054. Ni viongozi waliokuwa na maono ya roho wa nguvu katika mambo ya mwisho.

Kama kawaida, tukio hili halikuwa na mvuto sana kwa vyombo vya habari kwa nyakati zile, lakini katika maisha na utume wa Kanisa, hili ni tukio kubwa sana la majadiliano ya kiekumene, msingi wa ujenzi wa Ukristo duniani. Kile ambacho kilionekana kuwa ni hatua ndogo kabisa katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, kinaendelea kuzaa matunda makubwa katika maisha, utume na historia ya Kanisa. Hii ni sehemu ya mchakato muhimu sana katika kutibu na kuganga kashfa ya utengano wa Kanisa la Kristo. Kashfa ya utengano ilikuwa inalipekenya Kanisa kimya kimya kuanzia mwaka 1054 hadi mwaka 1964.

Kwa hakika, anasema Patriaki Bartolomeo wa kwanza, mkutano kati ya Patriaki Athenagora na Mwenyeheri Paulo VI ni tukio muhimu sana katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene unaofumbatwa katika nguvu ya upendo na majadiliano katika ukweli na uwazi, mfano bora wa kuigwa katika ulimwengu mamboleo unaogubikwa kwa ubinafsi, uchoyo, chuki, uhasama, ubaguzi na utengano kati ya watu. Lakini viongozi hawa wamekuwa ni nuru ya ulimwengu inayowaangazia wote kuendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na ustawi wa wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.