2017-07-26 16:41:00

Jitahidini kutafuta hazina na lulu iliyofichika: Ufalme wa Mungu!


Baada ya kutafakari Injili juu ya ngano na magugu Dominika iliyopita, Injili ya leo inatualika tutafute ilipo hazina na lulu ya kweli. Hapa Yesu Kristo anatamka mwenyewe juu yake na ujio wake ulimwenguni. Hivi tunaalikwa tutumie nafasi hii njema ya wokovu. Ni muda wa kuamua. Katika mfano huu Yesu anaweka wazi kuwa yeye ndiye Bwana wa historia na anasema wazi kuwa ufalme wa Mungu uko kati yetu. Hazina, yaani Kristo, yupo. Tusipoteze nafasi hiyo. Hii mifano miwili hazina na lulu ni mwaliko wa kuutafuta huo ufalme. Yesu anasema wazi kuwa wokovu uko mikononi mwenu na bila gharama yo yote. Ni juu yetu kuchangamkia hiyo fursa. Fanya uamuzi sasa. Ni muda wa kuamua. 

Padre Raniero Cantalamessa anafananisha muda huu wa Bwana na muda wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia ilipomalizika. Anasema kuwa mara tu baada ya majeshi ya Wajerumani kuondoka katika maeneo walioyateka, watu walivamia maduka na maeneo waliyoishi askari ili kupata baadhi ya vitu muhimu vilivyowafaa kwa mahitaji yao kama vyakula vizuri, nguo, mablanketi n.k. Walitumia hiyo nafasi kupata mahitaji yao muhimu. Ndivyo ilivyo katika Injili hii ya leo. Sote tunaalikwa kutumia hii nafasi adhimu tuliyopewa na Bwana.

Tungeweza kujiuliza mara moja, Je, sisi tunatafuta nini au tumewekeza wapi? Katika maisha ya kawaida twaona kuwa tumewekeza sana katika mambo mengi kwa mfano  kwenye bima ya maisha, bima ya afya nk. Ni sawa na sahihi kabisa. Lakini tunasahau kuwa bima hizi huwa ni kwa ajili ya kulinda maisha ya kawaida ya mtu awapo duniani lakini siyo bima dhidi ya kifo. Tena kinachotokea katika aina hizi za bima ni kuwa baada ya kifo wale walioandikishiwa urithi wa hiyo bima ndio wanaofaidi zaidi ya yule aliyeweka hiyo bima.

Tutafakarishwe na mfano huu; bibi mmoja aliyekuwa tajiri, alipofariki alipata nafasi ya kufika mbinguni. Akapata sehemu ndogo ya kukaa ila pembezoni kabisa mwa mbingu. Akamlalamikia malaika aliyemwongoza kwenda sehemu hiyo. Unanileta mahali hapa? Mbona mimi huko duniani nilikuwa na kila kitu na nilikaa mahali pazuri na kwa fahari kubwa? Malaika kwa unyenyekevu akamjibu – tafadhali ridhika na ulichopata. Vile vifaa vya ujenzi ulivyotuma huku mbinguni vilitosha tu kutengeneza kiti hiki kidogo ambapo ndipo mahali pako pa kujisetiri milele. Ridhika na ulichotoa. Malaika akaenda zake.

Ndugu zangu, leo hii tunaalikwa tuwekeze kwenye bima ya ufalme wa mbinguni. Tukumbuke kuwa ufalme wa mbinguni ni bima dhidi ya kifo na mauti ya milele. Yesu atuambia waziwazi, aniaminiye hata kama akifa, ataishi milele. Hivyo twaelewa vizuri mwaliko wake – uza vyote na kuutafuta kwanza ufalme. Kuwa tayari kutoa sadaka yo yote kwa ajili ya huo ufalme wake.

Leo tunaulizwa – katika yote ninayotamani katika maisha – ni kipi natamani zaidi au nahitaji zaidi? Injili inaweka wazi – kwanza ufalme wa mbinguni – Mt. 6:33 – basi, kwanza utafuteni ufalme wa Mungu na uadilifu wake, na hayo yote mtaongezewa. Ufalme wa Mungu ni utawala wa Mungu mioyoni mwetu, katika maisha yetu, nyumbani kwetu, katika jamii na katika ulimwengu wetu. Anayepata ufalme wa Mungu amepata yote. Ndiyo maana inalinganishwa na hazina bora iliyopatikana shambani au lulu ya thamani kubwa. Hata hivyo, hatuna budi kukumbuka vizuri kuwa msisitizo hauko katika kutafuta kwanza ufalme wa Mungu pamoja na mengine yanayoambatana nayo bali msisitizo uko katika kutafuta tu ufalme huo.

Somo la kwanza litupe changamoto tena leo. Tunaona kuwa Sulemani akiwa mfalme kijana mbichi kabisa alikuwa na mahitaji mengi sana. Alihitaji utajiri, jeshi kubwa na imara, umaarufu, usalama, ustawi, maisha marefu, furaha n.k. Lakini katika nafasi aliyopewa na Mungu ya kuomba – aliomba hekima. Alifahamu fika akiwa na hekima ya kimungu mengine yote yatawezekana. Na Mungu anamhakikishia hilo - 1 Waf. 3: 11-13 – Mungu akamwambia, kwa kuwa umeomba jambo hili – wala hukujitakia maisha marefu, wala hukujitakia utajiri, wala hukuomba roho za adui zako, bali umeomba hekima ya kujua kuhukumu, basi, tazama ninatenda kama ulivyosema. Ninakupa  moyo wa hekima na akili, hata kabla yako hakupatikana mtu kama wewe, na wala baada yako hatainuka mtu kama wewe,. Hata mambo yale usiyoyaomba nimekupatia: utajiri, heshima na utukufu kushinda wafalme wengine wote.

Sijui leo tungepata nafasi kama ya mfalme Sulemani tungeomba nini. Utajiri, mafanikio katika biashara, ushindi dhidi yaw engine, furaha? Maisha mema na ya upendo thabiti? Je tungekuwa na hekima ya Sulemani kuomba hekima katika maisha yetu ya kila siku? Ni ipi nafasi ya ufalme wa Mungu katika maisha yako? Tusisahau kuwa ufalme wa Mungu si moja kati ya mambo tuyatamaniyo ila ndicho pekee tunachohitaji. Mengine ni ziada.

TUMSIFU YESU KRISTO.

Padre REGINALD MROSSO, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.