2017-07-26 16:03:00

Hekima ya Mungu ni dira na mwongozo katika kufikiri na kutenda mema!


Hekima ni hali ya mtu kuutambua ukweli juu ya binadamu, vitu , matukio na mzingira mbalimbali na hivyo kuchagua vizuri jambo la kufanya. Hivyo hekima na ukweli huambatana daima. Hekima ni ile hali ya kuona lile ambalo kwa macho au hisi za kawaida ni vigumu kuonekana au kueleweka. Anayetenda katika hekima huwa anasimama katika ukweli na haki. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inatufundisha kwamba: “Mwanadamu anashiriki hekima na wema wa Mwumba anayempa mamlaka juu ya matendo yake na uwezo wa kujitawala kuhusu kweli na mema”. Hivyo hekima ni paji kutoka kwa Mungu, ambalo kwalo mwanadamu anatenda katika ukweli na wema. Hekima hujenga uwiano wa viumbe vyote na wote huingia katika ukaminilifu.

Hekima ni kitu cha thamani na cha kwanza kuhangaikiwa katika maisha ya mwanadamu. Elimu na ujuzi wote utakosa maana na msukumo kama havitasimama katika ukweli Hekima inapaswa kufananishwa na hazina iliyofichika au lulu nzuri anayoiona mfanyabiashara. Hii ni kwa sababu tunapojaliwa hekima ya kimungu hata vile tunavyojaliwa kuvimiliki vinatupatia furaha na fanaka ya kweli. Mantiki yake inaelezeka hapo juu kwani hekima inafunua ukweli na kuelekeza katika kuchagua vema. Kristo anaufananisha utawala wa ufalme wa Mungu na hicho kilicho cha thamani ambacho kwa nafasi ya kwanza kinapaswa kutafutwa kwa gharama yoyote. Mungu anapotawala ukweli ustawi na hivyo vyote vitaendeshwa kwa kadiri ya neno lake.

Mfano wa Mfalme Sulemani ni changamoto kwa watawala na wenye uwezo na mamlaka wa dunia yetu ya leo. Mfalme Sulemani anaomba kilicho cha thamani kuliko vyote: “nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya”. Hili kwake ndilo la msingi na si kitu kingine chochote. Madaraka au mali havitamfaidia kitu kama atapungukiwa na hekima hiyo itokayo juu. Sulemani anauunganisha ufalme wake katika ufalme wa Mungu. Hekima yake ndiyo inakaribishwa kutawala ili kuwa na uadilifu na kuyatofautisha mema na mabaya. Sulemani anaomba hekima ya kuwaongoza watu kadiri ya matakwa ya Mungu tofauti na hekima ya kidunia inayojikita katika uzoefu na mang’amuzi ya kawaida yaliyojikita katika elimu na tafiti. Anakuwa kweli changamoto kwa wenye kuchuchumilia madaraka leo hii si katika hekima ya Mungu bali kwa kuhonga, kudhulumu na hata ushirikina ili kujihakikishia nafasi fulani fulani ndani ya jamii.

Matokeo ya hawa wanaotafuta hekima za kibinadamu huwa ni mabaya. Viongozi wa namna hii huangaikia maslahi yao na hawatoruhusu neno la Mungu kupenyeza katika mamlaka yao. Viongozi wa namna hii hugeuka kuwa wanyonyaji, wanyanyasaji na wale wasiowajali watu walio chini yao. Zipo jamii nyingi zinazoangamia kwa watu wake kukosa maarifa haya ya kimbingu. Tuchukulie mathalani, leo hii jamii inapokumbwa na janga la UKIMWI majawabu yanayotafutwa si ya kimungu bali ni ya kibinadamu. Ni majawabu ambayo yanaudhalilisha utu wa mtu kwa kugeuzwa tu chombo cha starehe, yanachochea uasherati na kusambaratika kwa familia, ni majawabu ambayo yanaendelea kujaza mifuko ya watu. Mwanadamu haoni thamani ya kuwa na Mungu, kwake Mungu ni wa kuweka kauzibe na hivyo anapaswa kukaa pembeni katika mambo yangu.

Mungu ndiye asili ya ukweli wote. Kujishikamanisha naye ndiyo hekima ya kweli. Sisi wanadamu tupaswa kuitafakari sheria yake kwa ajili ya kusimama daima katika ukweli wake. Mwenyezi Mungu anamfahamu mwanadamu tangu mwanzo na heri yetu ipo katika kuungana naye daima. Balaa kwa mwanadamu huanza pale tu anapodiriki kuuweka ukweli wa Mungu pembeni. Matokeo yake ni uhuria wa kimaadili, mgawanyiko wa mawazo na hivyo kujenga jamii ambayo inakosa misingi ya umoja kimaadili. Kujishikamanisha kwake kunajionesha katika paji la imani na kubaki waaminifu katika neno lake. Hivyo ni wito kwetu kujiimarisha katika imani yetu kwa Mungu ili ufalme wake ustawi ndani mwetu na hivyo kujazwa na hekima ya Mungu.

Mtume Paulo anatuonesha jinsi ambavyo Mungu anatenda pamoja na sisi kwa namna mbalimbali ili kukamilishana. Hekima yake inamwita kila mmoja tangu awali kwa ajili ya kutimiza wajibu fulani ili kuleta uwiano wa kijamii. Mwitikio wetu kwa wito wake ni kudhihirisha upendo na shukrani zetu kwake. “Maana wale aliowajua tangu asili, aliowachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi”. Hivyo wito wake kwetu ni mwendelezo wa wito mkubwa wa Mwana wake ambao umenuia katika ukombozi wa mwanadamu. Mungu amekupatia nafasi uliyonayo kwa makusudi maalum. Juhudi zetu zijikite katika kukitafuta na kukihifadhi kilicho cha thamani kubwa ndani ya wito wangu ambacho kwacho hekima ya Mungu itatamalaki. Kuitikia wito huu kunatuunganisha sote na kuwa ndugu pamoja na ndugu yetu mkubwa Kristo Yesu na hivyo kuufanya ufalme wa Mungu kuenea kweli.

 Utajiri wa kweli ambao tunaweza kuuachia ulimwengu kama urithi wetu si wingi wa vitu au ugunduzi na maarifa mengi ya kidunia. Utajiri wa kweli ni ule ambao unawagusa kila mtu mmoja mmoja katika nafsi yake. Utajiri wa kweli na wenye thamani kubwa ni kumpeleka Kristo kwa binadamu wote. Wapo wanaojikinai kwamba wameuachia ulimwengu urithi pengine kwa majumba mengi yanayotoa huduma mbalimbali za kijamii, mfano mahospitali, mashule nk. Hayo ni majengo tu ambayo pia yana umuhimu na nafasi yake. Lakini urithi wa kweli ni kuugusa ubinadamu. Haya ni matokeo ya kuukumbatia ukweli. Kuishi katika ukweli kunakoongozwa na hekima ya Mungu ndiyo njia sahihi ya kutufikisha katika kuungana na wenzetu kiroho na kuwaachia urithi wao stahiki. Hii ndiyo hekima ambayo Mwenyezi Mungu amemkirimia kila mmoja wetu kwa nafasi yake akinuia kila mmoja kuicheza vema nafasi yake kwa ajili ya fanaka kwa watu wote.

Kitu cha thamani katika maisha ya mwanadamu, kile ambacho kinapaswa kutafutwa au kutunzwa kwa gharama yoyote ni uwepo wa Mungu ndani yake. Mmoja anapokuwa na Mungu amepata yote kwani Yeye ni muweza wa yote. Uwepo wa Mungu ndani ya mwanadamu ni uwepo wa ukweli wote na hekima yake itatamalaki. Mtu huyu atatenda kadiri ya mapenzi ya Mungu na daima atayatafuta mapenzi yake na kuyatimiza. Kinyume chake ni yule ambaye hana Mungu ndani mwake. Huyu atajikinai katika kuweza yote kwa juhudi binafsi. Mwanadamu anajisahau ukomo wa uwezo wake; mwanadamu anajisahau kutokuweza kwake katika kutenda yote. Huyu atajidai kuweza na kujua yote na matokeo yake huwa ni kushindwa kudumu katika mengi anayonuia kuyatenda. Leo tuiombe hiyo hekima ya Mungu kusudi tuweze kuutambua ukweli ambao ni Mungu mwenyewe, tuukumbatie huo ukweli na kutenda katika kweli. Roho Mtakatifu atuangaze na kuona umuhimu wa kuungana na Mungu daima kusudi uwepo wake wa daima ndani mwetu uwe ni taa ya kutuongoza katika njia sahihi.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.
All the contents on this site are copyrighted ©.