2017-07-25 07:56:00

Tuzungumzie tunu msingi za kifamilia, ili tujenge familia imara!


Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia” anagusia kwa namna ya pekee, furaha ya upendo ndani ya familia, changamoto na kinzani zinazoendelea kuiandama familia ya binadamu katika ulimwengu mamboleo. Hii ni changamoto ya waamini kujikita katika toba, wongofu wa ndani, msamaha na upatanisho, ili kweli familia iweze kutekeleza dhamana na wajibu wake ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo. Wosia huu ni habari njema kwa familia hususan familia zenye madonda na makovu ya maisha ya ndoa na zile ambazo kwa kweli zinanyanyasika na kudhalilishwa kutokana na sababu mbali mbali.

Ni wosia unaojikita katika Neno la Mungu linalomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu ndoa na familia: upendo ndani ya familia unaogeuka kuwa ni chemchemi ya maisha mapya. Baba Mtakatifu anapenda kutoa maelekezo ya sera na mikakati ya shughuli za kichungaji ili kujenga na kuimarisha familia mintarafu mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.

Baba Mtakatifu anatoa mchango wake juu ya umuhimu wa elimu na makuzi kwa watoto; umuhimu wa familia kujikita katika huruma ya Mungu na mang’amuzi sahihi kwa familia ambazo haziendani na mafundisho ya Kristo kwa waja wake, mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha wosia wake wa Furaha ya Upendo ndani ya familia kwa kutoa mwongozo wa tasaufi ya familia.

Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anasema, Baba Mtakatifu anachota utajiri wa mafundisho ya Mababa wa Kanisa, wanataalimungu mahiri pamoja na waandishi maarufu wa nyakati hizi, bila kusahau nyaraka za Mababa wa Kanisa, Katekesi kuhusu: familia, upendo wa binadamu; Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki; Mungu ni Upendo, Injili ya furaha pamoja na kuchota utajiri unaofumbatwa kutoka katika nyaraka mbali mbali za Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia. Kuna mwelekeo chanya wa uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia, kwani kila tendo la upendo ni utenzi wa sifa na shukrani kwa Mwenyezi Mungu, mwaliko kwa wanandoa kukuza na kudumisha fadhila ya upendo ambao kimsingi ni ushuhuda wa imani tendaji! Maaskofu wanahamasishwa kuwa ni kielelezo na mfano wa Kristo mchungaji mwema anayejitaabisha kufunga, kuganga na kuponya madonda ya waja wake, anawatambua wanakondoo wake na anawaita kwa majina.

Baba Mtakatifu katika Wosia wake huu anakazia kwamba, Kanisa liwe ni mahali pa kuwahusisha watu wote na wala si kuwatenga. Mapadre wawasaidie waamini wanaoogelea katika shida za maisha ya ndoa na familia, ili kuweza kupata mang’amuzi mapana zaidi kwa njia ya tafakari, toba na wongofu wa ndani. Ushuhuda wa waamini waliotalakiana na kuamua kuoa au kuolewa tena unapaswa kufanywa kwa uangalifu mkubwa ili kuona ikiwa kama kumekuwepo na jitihada za upatanisho, mahusiano yaliyopo kati ya waamini hawa na Jumuiya ya Kikristo na ni mfano gani ambao vijana wanaojiandaa kwa maisha ya ndoa na familia wanaweza kuuona kutoka kwao! Huu ni mchakato wa majadiliano unaojikita katika kiti cha huruma, majiundo makini na hatimaye, ushiriki mkamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Wosia huu unatoa mkazo wa pekee kwa maandalizi ya wanandoa watarajiwa, ili Kanisa liweze kuwapatia majiundo kamili kuhusu Sakramenti ya Ndoa ili waweze kuanza mchakato wa ujenzi wa msingi wa ndoa imara na thabiti. Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu ndoa na familia; utajiri wa maisha, mang’amuzi na mifano hai ya wanandoa iwasaidie wanandoa watarajiwa kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya familia.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland limeanzisha kampeni kamambe ya Siku ya Familia Duniani itakayoadhimishwa kuanzia tarehe 21 hadi tarehe 26 Agosti 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Injili ya familia, furaha ya ulimwengu”. Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua uzito wa tukio hili amemwandikia ujumbe Kardinali Kevin Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha akikumbusha juu ya maadhimisho ya Siku ya VIII ya Familia Duniani iliyoadhimishwa Jimbo kuu la Philadelphia, nchini Marekani na kwamba, maadhimisho kwa Mwaka 2018 yatafanyika Jimbo kuu la Dublin.

Baba Mtakatifu anapenda kutoa mwongozo makini ambao unapaswa kufuatwa kama sehemu ya tafakari ya Wosia wa Kitume, "Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Swali la msingi hapa ni kujiuliza ikiwa kama Injili inaendelea kuwa ni sababu ya furaha kwa ulimwengu? Je, Familia bado inaendelea kuwa ni Habari Njema kwa ulimwengu mamboleo? Baba Mtakatifu anakiri kwa kusema kwamba, ni kweli familia inaendelea kuwa ni sababu ya furaha na Habari Njema kwa walimwengu, kwani uhakika huu unafumbatwa katika mpango wa Mungu kwa mwanadamu; upendo ambao unapaswa kupewa jibu la “Ndiyo” na binadamu wote kwani hiki ni kiini cha moyo wa binadamu.

Hii ni “Ndiyo” inayowaunganisha bwana na bibi tayari kushiriki katika mchakato wa kuhudumia uhai katika hatua zake zote! Hii ni “Ndiyo” ya Mungu inayodhihirisha ile dhamana yake kwa binadamu aliyejeruhiwa, anayetendewa vibaya na kutawaliwa na ukosefu wa upendo. Familia kimsingi ni “Ndiyo” ya upendo wa Mungu. Upendo ni chimbuko ambalo linaiwezesha familia kushuhudia sanjari na kuzalisha upendo wa Mungu duniani. Bila upendo huu, si rahisi sana kuweza kuishi kama watoto wa Mungu, watu wa ndoa, wazazi na hata kama ndugu.

Baba Mtakatifu anapenda kuhimiza umuhimu wa familia kuishi kwa kujikita katika upendo kwa ajili ya upendo na ndani ya upendo wenyewe. Hii ina maana kwamba, wanandoa wanapaswa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusameheana, kuvumiliana na kuheshimiana. Baba Mtakatifu anawaalika wanafamilia kumwilisha ndani mwao maneno makuu matatu: “Hodi, samahani na asante”. Mama Kanisa kila wakati anapata mang’amuzi ya udhaifu wa binadamu, ndiyo maana watu wote, familia pamoja na viongozi wa Kanisa wanapaswa kujenga unyenyekevu unaopyaishwa, unaotamani kufundwa vyema; kuelimishwa ili uweze kuelimisha; kusaidiwa ili uweze kusaidia; kusindikiza, kung’amua na kuwaingiza na hatimaye, kuwashirikisha watu wote wenye mapenzi mema.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland linakaza kusema, maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani kwa Mwaka 2018 ni wakati muafaka wa kutangaza na kushuhudia: uzuri, wema na utakatifu wa Injili ya familia unaofumbatwa pia katika udhaifu na mapungufu ya binadamu yanayopaswa kugangwa kwa mafuta ya faraja na divai ya huruma kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Familia kutoka sehemu mbali mbali za dunia zinahamasishwa kushiriki kwa wingi tukio hili muhimu katika maisha na utume wa familia ndani ya Kanisa. Ireland ni nchi yenye mvuto wa maisha na utume wa kimissionari! Hii ni nchi ambayo, wamissionari wengi walijisaka na kujitosa kwenda sehemu mbali mbali za dunia ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili.

Tarehe 21 Agosti 2017, Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland litaanza maadhimisho haya yatakatodumu kwa kipindi cha mwaka mzima, ili kuwahamasisha waamini kutambua na kuthamini Injili ya familia inayopaswa kushuhudiwa na wengi. Katika Madhabahu ya Bikira Maria wa Knock, kila jimbo litatoa wanandoa wawakilishi, watakaojadili kuhusu familia, ili waweze kuwa ni sehemu ya familia! Hii ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho haya. Picha ya Sanamu ya Familia Takatifu itaanza kuzunguka katika Majimbo yote nchini Ireland na kilele chake ni wakati wa maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani kwa Mwaka 2018. Familia mbali mbali nchini Ireland zinahamasishwa na Maaskofu kuonesha upendo na ukarimu, kwa kutoa hifadhi kwa familia mbali mbali zitakazohudhuria tukio hili la kihistoria.

Kwa habari zaidi unaweza kukodolea macho kwenye anuani ya tovuti ifuatayo:

www.worldmeeting2018.ie

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.