2017-07-25 07:00:00

Mchakato wa maboresho ya huduma ya Hospitali ya Mt. Gaspar, Itigi!


Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, Manyoni, Singida, Tanzania, inayomilikiwa na kuendeshwa na Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu ilifunguliwa rasmi kunako mwaka 1987 na Rais Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hospitali hii inaongozwa na kauli mbiu: tibu, fariji na elimisha. Tangu kuanzishwa kwake, vongozi wamekuwa wakisoma alama za nyakati na hivyo kendelea kuwa na mbinu mkakati ambao umeisaidia hospitali kuzidi kukua na kupanuka mwaka hadi mwaka. Ilipoanza kutoa huduma kulikuwa na wodi moja ya tiba tu (Medical ward). Mwaka 1990 hospitali ilianzisha wodi ya watoto (Pediatric ward), Mwaka 1993 iliongeza wodi mbili: yaani wodi ya wazazi na Upasuaji (Obstetric & Gynecology ward and Surgical Ward).

Hospitali ilipoanza ilikuwa inatoa huduma kwa wagonjwa wa Wilaya ya Manyoni zaidi, lakini ilivyozidi kupanuka na kutoa huduma nzuri na bora zaidi kwa kuzingatia mahitaji ya kiroho na kimwili, ilianza kupokea wagonjwa wengi kutoka mikoa yote ya Tanzania na hata nje ya Tanzania. Hii haikutokana na kupanuka kwa miundo mbinu tu bali pia kwa huduma inayotolewa na madaktari bingwa huku pembezoni mwa jamii, kama sehemu ya tasaufi ya Shirika ya kusikiliza na kujibu kilio cha damu. Hospitali iliendelea kupata vifaa vya kisasa na kuzidi kutoa tiba, faraja na elimu nzuri na bora kwa wagonjwa, ikawa ni kweli ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu, kivutio kwa watu kutoka ndani na nje ya mkoa wa Singida!

Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, ilipofuguliwa (1987) ilikuwa ina uwezo wa kulaza wagonjwa 80 tu. Lakini kwa sasa inauwezo wa kulaza wagonjwa 323. Ongezeko hili la vitanda linatokana na hitaji lililopo. Mwaka 2000 uongozi wa Shirika la Wamisionari wa Damu Takatifu uliamua kupanua wodi ya watoto iliyokuwa na vitanda 45 na kufikisha vitanda 150. Hii ilitokana na ukweli kwamba, kuanzia mwezi Januari hadi mwezi Juni ya kila mwaka kutokana na ugonjwa wa malaria na upungufu wa damu, Hospitali ya Mtakatifu Gaspar Hospital hupokea watoto wagonjwa wengi sana. Hivyo hitaji hili lilipelekea kujenga wodi hii mpya ambayo ilifunguliwa rasmi tarehe 23.11.2003 na Mheshimiwa Benjamini Mkapa, Rais wa  awamu ya tatu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa sasa hospitali ina wodi kubwa nne: Wodi ya Tiba, Wazazi, Upasuaji na Watoto. Sambamba na wodi hizi kuna Vyumba vikubwa vitatu vya Upasuaji mkubwa (Operation Rooms) na kati ya hivyo kimeja kimetengwa kwa ajili ya upasuaji wa watoto. Kwa upasuaji mdogo vipo vyumba vitatu (Minor Theatre), Kuna idara ya Macho na Meno pamoja na Idara ya Mazoezi (Physiotherapy), „Mionzi, CT Scan na Ultra Sound”. Kutokana na kukua kwa hospitali hii katika huduma zake mwaka 2010 Seikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliamua kuipandisha hadhi na kuwa Hospitali ya Rufaa.

Kwa kusoma alama za nyakati, ili kukabiliana na changamaoto ya huduma bora na nzuri zaidi kwa familia ya Mungu nchini Tanzania, Padre Terenzio Pastore, C.PP.S Mkuu wa Kanda ya Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Italia kwa kushirikiana na Padre Chesco Peter Msaga, C.PP.S Mkuu wa Shirika la Wamissionari wa damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania, wameamua kumteua Padre Alessandro Manzi, C.PP.S, aliyepewa Daraja Takatifu ya Upadre, tarehe 23 Julai 2017, Mhandisi katika taaluma na missionari katika maisha na utume, kushughulikia kwa karibu zaidi mchakato wa maboresho ya huduma inayotolewa na Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, Manyoni, Singida, Tanzania kwa ajili ya sifa na utukufu wa familia ya Mungu nchini Tanzania na kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Padre Cesco Peter Msaga anampongeza Padre Alessandro Manzi, C.PP.S, kwa kufikia Daraja takatifu ya Upadre itakayomsaidia kuelekea kwenye utimilifu wa maisha; anampongeza kwa sadaka na majitoleo yake kwa ajili ya kusikiliza na kujibu kilio cha damu, kama sehemu ya tasaufi ya Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu. Anamkaribisha kwa mikono miwili nchini Tanzania ili kutekeleza dhamana na majukumu aliyokabidhiwa kwa sasa na Shirika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.