2017-07-25 07:00:00

Kuna uhusiano mkubwa kati ya wahamiaji na maendeleo endelevu!


Padre Michael Czerny, Katibu mkuu msaidizi, Idara ya wahamiaji na wakimbizi, Baraza la Kipapa la Maendeleo Endelevu ya binadamu akichangia katika kikao cha Umoja wa Mataifa kinachojadili kuhusu “Mkataba wa Kimataifa juu ya usalama wa Wahamiaji 2018” mjini New York, kuanzia tarehe 24-25 Julai 2017 anakazia kuhusu uhusiano uliopo kati wahamiaji na maendeleo.

Itakumbukwa kwamba, “Mkataba wa Kimataifa juu ya usalama wa Wahamiaji 2018”Unalenga kuratibu na kuboresha mchakato wa wahamiaji na wakimbizi duniani, ili kulinda na kudumisha haki msingi, utu na heshima yao kama binadamu. Unakazia umuhimu wa Jamii kusikiliza na kujibu kilio cha wakimbizi na wahamiaji duniani; kwa kukusanya maoni; kwa kupunguza gharama za kuwahudumia wahamiaji sanjari na kudumisha usalama na maisha bora zaidi. Ni mkataba unaopania kuboresha: ulinzi na usalama; haki msingi za binadamu pamoja na kupatiwa huduma ya msaada wa kisheria pale haki zao zinapovunjwa.

Padre Michael Czerny anasikitika kuona kwamba, watu wanashindwa kuoanisha kuhusu maendeleo endelevu ya binadamu na sababu msingi zinazoyafanya makundi ya watu kuzihama nchi zao: baa la umaskini na njaa; vita na ghasia; ukosefu wa fursa za ajira; athari za mabadiliko ya tabianchi; ukame wa kutisha; rushwa na ufisadi wa mali ya umma; mambo ambayo yamebainishwa kinagaubaga kwenye Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu ifikapo mwaka 2030.

Ni haki ya kila mtu kubaki nchini mwake ili kudumisha utu na heshima yake, amani na usalama. Asiwepo mtu anayelazimika kuikimbia nchi yake kutokana na ukosefu wa fursa za ajira na maendeleo. Lakini, ukweli wa mambo unaonesha kwamba gharama za kiuchumi na kitamaduni zimechangia watu kuzikimbia na kuzihama nchi zao. Ikiwa kama vigezo vyote vilivyotajwa hapo awali vitazuingatiwa na kuheshimiwa, basi, uhamiaji unakuwa ni chaguo la mtu na wala si shuruti.  Umaskini na ukosefu wa matumaini katika mchakato wa maendeleo endelevu umepelekea watu wengi kuzihama nchi zao, kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao huko kwenye Bahari ya Mediterrania.

Wahamiaji ni watu wanaotaka kuboresha utu na maisha yao na hatimaye, kuchangia katika ustawi wa familia na mahali wanapotoka; ukuaji na maendeleo ya uchumi kwa nchi wahisani. Lakini yote haya anasema Baba Mtakatifu Francisko yanategemea jinsi ambavyo wahamiaji: watakaribishwa, watalindwa, kuendelezwa na hatimaye, kushirikishwa katika jamii hisani. Hii ni changamoto inayopania kukuza na kuboresha karama, mapaji, elimu, ujuzi na maarifa ya wahamiaji, ili kuchangia katika ustawi na maendeleo ya jamii.

Padre Michael Czerny anakaza kusema, wahamiaji wanapaswa kukaribishwa, kuheshimiwa pamoja na haki zao msingi kulindwa na kudumishwa kisheria. Wapewe msaada wa hali na mali, kadiri ya uwezo wa jamii inayowakirimia; kwa kuhakikisha kwamba, serikali inatoa ruzuku kwa jumuiya zinazotoa hifadhi kwa wakimbizi. Wahamiaji washirikishwe kuchangia utajiri, karama na rasilimali zao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Wawe mstari wa mbele kuhakikisha kwamba, wanaheshimu tunu msingi za jamii inayowazunguka; kwa kuzingatia mapokeo, mila na desturi za jamii husika. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi ni fursa ya kukuza na kudumisha utu wa binadamu; kujenga na kuimarisha madaraja ya watu kukutana na kusaidiana; tamaduni kujadiliana ili kudumisha amani na udugu kati ya watu! Udugu na mshikamano vinasaidia kuimarisa amani ndani ya jamii sanjari na kukoleza maendeleo endelevu ambayo Jumuiya ya Kimataifa kwa sasa inayavalia njuga!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.