2017-07-24 10:12:00

Papa Francisko: Iweni na kiasi na dumisheni majadiliano Yerusalemu


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Tafakari na Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili, tarehe 23 Julai 2017 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amesikitika kusema, kwamba, anafuatilia kwa wasi wasi mkubwa matukio mbali mbali yanayoendelea kujiri mjini Yerusalemu! Anasikia ndani mwake, wajibu wa kuwaalika wahusika wote kujikita katika kiasi na majadiliano. Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuungana naye kwa njia ya sala na sadaka zao, kwa ajili ya kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia mawazo ya upatanisho na amani.

Katika siku za hizi karibuni kumekuwepo na hali tete ya ulinzi na usalama kiasi hata cha kuifanya Serikali ya Israeli kuimarisha mikakati ya ulinzi na usalama kuzunguka maeneo ya misikiti, baada ya kijana mmoja kutoka Palestina alipojitoa mhanga na kufanya mauaji ya askari wawili wa Israeli. Waziri mkuu wa Israeli Bwana Benjamin Netanyahu anaangalia uwezekano wa kuimarisha zaidi ulinzi na usalama katika eneo hili, hali ambayo imezua wasi wasi mkubwa kwa wananchi wa Palestina.

Rais wa Palestina Mahmoud Abbas amekata mawasiliano na Serikali ya Israeli inayotaka kuhatarisha uhuru wa Wapalestina ambao umekuwepo bila kuingiliwa tangu mwaka 1967. Vikosi vya ulinzi na usalama nchini Israeli vinaendelea kuwatia mbaroni wananchi wa Palestina na kwamba, hadi sasa kuna watu kadhaa ambao wamepoteza maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.