2017-07-24 10:53:00

Alessandro Manzi, C.PP.S apewa Daraja Takatifu ya Upadre!


Katika hija ya maisha na wito wa Kipadre, Yesu anaendelea kumuuliza kila Padre, ikiwa kama anampenda kuliko wengine wote, swali msingi alilomuuliza Mtakatifu Petro mara tatu, kiasi cha kumfanya mtu mzima: kuangua kilio na kusema, “Bwana wewe wajua kuwa ninakupenda”. Hapo Yesu, akamkabidhi dhamana na jukumu la kuwachunga kondoo wake! Yesu alimkumbusha Petro taabu na mahangaiko ya maisha na utume wake, kiasi cha kumkana mara tatu, lakini Yesu bado anaendelea kuwa mwaminifu katika ahadi zake na anataka kumwimarisha, ili hatimaye, aweze kuwa chombo cha utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu, kiasi hata cha kuyamimina maisha yake kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake!

Askofu Douglas Regattieri wa Jimbo Katoliki Ceserna-Sarsina ameyasema hayo, Jumamosi, tarehe 22 Julai 2017, wakati wa Ibada ya Misa Takatifu na Upadrisho wa Shemasi Alessandro Manzi, C.PP.S. wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Italia. Ibada iliyoadhimishwa kwenye Parokia ya “Corpo e Sangue di Cristo”, Jimbo kuu la Roma na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu wanaoshiriki katika kongamano la kimataifa kuhusu changamoto za maisha ya Kijumuiya, bila kuwasahau watanzania wanaoishi Roma ambao kwao Padre Alessandro Manzi anaona daima chimbuko la wito wake wa kitawa na Kipadre kwa kuguswa na kilio cha damu pamoja na ukarimu wa familia ya Mungu nchini Tanzania!

Askofu Douglas Regattieri katika mahubiri yake amegusia changamoto na fursa mbali mbali ambazo Kristo Yesu amezitumia kwa ajili ya kufafanua kuhusu mambo msingi ambayo wafuasi wake wanapaswa kuyazingatia licha ya changamoto na patashika nguo kuchanika katika safari yao ya ufuasi wao. Amegusia kuhusu mpanzi wa mbegu njema, magugu na shetani anayetaka kuharibu kazi njema iliyoanzishwa na mpanzi ambaye ni Kristo Yesu mwenyewe kama anavyofafanua katika Injili ya Jumapili ya XVI ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa. Hata pale mitume walipokuwa wamekata tama ya maisha na kurejea tena katika kazi yao ya uvuvi wakateseka usiku kucha lakini wakaambulia patupu! Yesu anawatokea na kuwatia shime kwa kupata samaki wengi zaidi. Yesu anawaimarisha mitume wake kutokana na udhaifu wao na kuwakumbusha Mapadre kwamba, wito na maisha yao yanahifadhiwa katika chombo cha udongo!

Huu ni udhaifu wa mwili unaopaswa kuimarishwa kwa joto la imani, matumaini na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Hili ni joto linalotolewa na Roho Mtakatifu ili kuweza kuwaimarisha mitume katika maisha na wito wao. Itakumbukwa kwamba, Petro alimkana Yesu pale walipokuwa wanaota moto, lakini kwa bahati mbaya moyo wake ulikuwa umegubikwa na ubaridi kiasi kwamba akashindwa kumshuhudia Kristo Yesu na matokeo yake akamkana mara tatu mbele ya watu! Yesu akawatokea tena wafuasi wake wakiwa wanaota moto baada ya kuvua usiku na  mchana bila kupata samaki, akawaonjesha ule moto wa imani, matumaini na mapendo; walioupoteza wakati wa Kashfa ya Msalaba. Ni moto uliowasaidia mitume kung’amua mapungufu yao ya kibinadamu, ilikuambata nguvu ya Roho Mtakatifu inayowaimarisha katika maisha na utume wao kwa Kristo na Kanisa lake kwa kujikita katika huruma, uvumilivu na udumifu, daima wakitambua kwamba, wao ni ngano safi inayozungukwa na magugu, yaani nguvu ya dhambi! Lakini, wakivumilia na kushikamana na Kristo Yesu, wataweza kupata furaha na maisha ya uzima wa milele!

Askofu Douglas Regattieri amerejea tena katika msingi ule wa swali la Yesu kuhusu upendo wa Mapadre kwake binafsi na kwa Kanisa lake unaofumbatwa katika maisha ya Sala; Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na sadaka ya maisha kwa ajili ya wokovu wa walimwengu. Dhamana ya Padre mpya itakuwa ni kushiriki katika maisha na utume ambao Kristo Yesu amewakabidhi mitume na waandamizi wao; utume ambao Mapadre wanaushiriki kwa namna ya pekee kabisa kwa kuwa wahudumu mambo matakatifu miongoni mwa watu wa Mungu. Mapadre wanachangamotiushwa kuwa waaminifu na wadumifu katika maisha na utume wao.

Mapadre kimsingi ni wahudumu wa Neno la Mungu, wanalopaswa kulisoma, kulitafakari, kulifundisha na kulishuhudia kwa njia ya maisha yao yenye mvuto na mashiko. Ni wajibu na dhamana yao kujibidisha kufundisha na kushuhudia mafundisho tangu ya Kanisa Katoliki na wala si vinginevyo! Mapadre ni wahudumu wa Sakramenti za huruma ya Mungu na kwa namna ya pekee kabisa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ni wahudumu wa Sakramenti ya Upatanisho unaowakirimiwa waamini huruma na kuwaonjesha upendo wa Baba wa milele, ambaye daima anawasubiri katika kiti cha huruma kama alivyofanya Baba mwenye huruma kwa mwana mpotevu!

Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa ni kwa ajili ya sifa na utukufu kwa Mwenyezi Mungu sanjari na utakatifu na wokovu wa watu wa Mungu. Mapadre daima wakumbuke kwamba, wao ni vyombo vya Sala kwa ajili ya kuwaombea watu wa Mungu huruma, upendo, faraja na matumaini. Kwa njia ya sala, sadaka na huduma makini, Mapadre wanakuwa karibu zaidi na Kristo, Kuhani mkuu aliyejisadaka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Hii ni changamoto kwa Mapadre kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya wokovu wa watu wa Mungu.

Askofu Douglas Regattieri wa Jimbo Katoliki Ceserna-Sarsina, kwa namna ya pekee kabisa amekazia umuhimu wa sala katika maisha na utume wa Mapadre kwani sala inaimarisha utashi katika kuamua na kutenda. Ikumbukwe kwamba, Mwenyezi Mungu anaendeleza kazi ya ukombozi kwa kuwaita na kuwateua watu kushiriki katika kazi shambani mwake! Anawateuwa watu wa kawaida wasiokuwa na makuu kama alivyofanya kwa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto VXI, akikukumbusha maneno yake kwamba, Makardinali waliamua kumchagua kuwa mtumishi katika shamba la Bwana.

Damu Azizi ya Kristo iliyomwagika kwa ajili ya kuwakomboa watu, iwatie shime  Mapadre kutenda katika maisha yao, daima wakijitahidi kuifuata ile Njia ya Msalaba. Ubavu wa Yesu uliochomwa kwa mkuki na humo ikatoka damu na maji, iwakumbushe Mapadre umuhimu wa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu katika maisha ya watu na Sakramenti ya Upatanisho inayowakirimia waamini huruma na upendo wa Mungu. Kila mara Mapadre wanapoadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu wakumbuke maneno ya Yesu: “Fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi”. Ekaristi Takatifu ni Fumbo kuu la Imani na zawadi ya uwepo endelevu wa Kristo miongoni mwa watu wake. Mapadre wajitahidi kufanana na Kristo Yesu katika maisha na utume wao. Wanaposhiriki Mwili na Damu Azizi ya Kristo, wajitahidi kuwa sadaka safi isiyokuwa na mawaa; sadaka inayompendeza Mungu. Damu Azizi ya Kristo iwe ni msaada katika maisha na utume wao. Bikira Maria, Mama wa Damu Azizi ya Yesu awasimamie, awaongoze na kuwapatia tunza yake ya kimama!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.