2017-07-22 14:45:00

Viongozi wa kidini wanayo dhamana ya kuzuia mauaji ya kimbari


Umoja wa Mataifa unasema, umefika wakati kwa viongozi wa kidini duniani kuhusishwa kikamilifu katika mchakato wa kuzuia uwezekano wa kuibuka tena mauaji ya kimbari ambayo yamesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao katika historia ya miaka ya hivi karibuni! Hizi ni juhudi za miaka mitatu ya mpangokazi wa Umoja wa mataifa unaowashirikisha wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanasaidia kugaribisha umuhimu wa kuzia mauaji ya kimbari, vitendo vya jinai wakati wa vita; mauaji ya kikabila pamoja na vitendo vyote vinavyokwenda kinyume cha heshima na utu wa binadamu.

Askofu mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, hivi karibuni akichangia kuhusu mada hii, alisema kwamba, Vatican, kimsingi inaunga mkono mpango kazi wa Umoja wa Mataifa, kwa kuutaka kuwajibika kulinda. Kwanza kabisa, hii ni dhamana inayopaswa kutekelezwa na Serikali husika, wakati ambapo Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kusaidia Serikali kutekeleza vyema wajibu wake bila kuchochea vurugu wala ghasia. Viongozi wa kidini wanaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kuzuia mauaji ya kimbari, lakini, ikumbukwe kwamba, Serikali ndiyo inayomiliki vyombo vya ulinzi na usalama wa raia na mali zao pamoja na Mahakama, mahali ambapo sheria inaweza kuchukua mkondo wake na haki ikatendeka. Viongozi wa kidini wakishirikishwa kikamilifu wanaweza kusaidia mchakato mzima wa kuzuia mauaji ya kimbari, kwani wao wana uwezo mkubwa wa kutekeleza dhamana hii kadiri ya tabia na imani za watu. Lakini, inasikitisha kuona kwamba, kuna wakati ambao hata viongozi wa kidini wamehusisha pia na mauaji ya kimbari sehemu mbali mbali za dunia.

Haya ni matumizi mabaya ya uongozi wao kidini yanayoendelea hata leo hii kujionesha kwa watu kubambikizwa kesi za kufuru za kidini au kutumia dini kwa ajili ya kufanya vitendo vya kigaidi vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu kwa kisingizio cha imani kali! Kumbe, ni wajibu na dhamana ya viongozi wa kidini na waamini wao kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete kulinda jamii dhidi ya mauaji ya kimbari; kwa kujizatiti katika kulinda na kudumisha utu, heshima, ustawi na maendeleo ya binadamu wote; kwa kukuza majadiliano ya kidini na kiekumene katika ukweli na uwazi;  kwa kudumisha: umoja, upendo, udugu na maridhiano kati ya waamini wa dini mbali mbali.

 Viongozi hawa wasimamie na kudumisha ukweli, haki na amani mambo msingi yanayofumbatwa katika Vitabu vitakatifu. Viongozi wa kidini wapandikize mbegu ya haki na amani na kung’olea mbali ndago za vita, ghasia na mipasuko ya kijamii. Wawe watekelezaji muhimu wa Uhuru wa kidini na kukataa kujihusisha kabisa na vitendo vya kigaidi pamoja na misimamo mikali ya kidini. Wawaelimishe waamini wao mambo msingi ya imani, maadili na utu wema; upendo na mshikamano kati ya watu wa Mataifa, kwa kutambua kwamba, dini kimsingi si tatizo bali ni suluhu ya changamoto zinazomwandama mwanadamu.

Vijana waelimishwe na kufundwa kuhusu umuhimu wa kuzingatia haki, heshima na utu wa binadamu. Uhuru wa kuabudu ni msingi wa haki zote za binadamu anasema Baba Mtakatifu Francisko. Vita na ghasia zinahatarisha sana utakatifu wa maisha ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kumbe, ni wajibu wa viongozi wa kidini kupinga kwa nguvu zote vita, vurugu na ghasia; chuki na uhasama pamoja na kufuru mbaya ya kutumia Jina la Mwenyezi Mungu kutenda ubaya. Majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi ni msingi thabiti wa amani duniani.

Ni fursa ya kuweza kuthamini tofauti katika umoja; kwa kuheshimiana na kuthaminiana; kwa kutembea pamoja katika amani, daima kwa kutafuta mafao ya wengi! Kuna haja ya kujenga na kudumisha uchaji wa Mungu na moyo wa ibada miongoni mwa watu; kwa kushughulikia changamoto za kijamii zinazoweza kusababisha vita, ghasia na machafuko ya kijamii; kwa kuwapatia vijana fursa za ajira: kwa kuendeleza mchakato wa haki, amani, maridhiano na msamaha wa kweli. Ni fursa kwa waamini wa dini mbali mbali kushikamana katika kutenda matendo ya huruma: kiroho na kimwili sanjari na kujikita katika ujenzi wa utamaduni wa haki na amani. Dhamana na wajibu wa viongozi wa kidini; majadiliano ya kidini na kiekumene; uchaji wa Mungu; haki na amani ni mambo msingi yanayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa si tu kwa kuzia mauaji ya kimbari, bali kwa kuwajengea watu fadhila, kanuni maadili, utu wema, upendo na mshikamano ili watu waweze kutambua kutoka katika undani wa maisha yao kwamba, mauaji ni kitendo kinachokwenda kinyume cha utu na heshima ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.