2017-07-22 08:42:00

Iweni na huruma na msamaha kama Baba yenu wa mbinguni!


Ndugu msikilizaji  wa Radio Vatican, nakukaribisha katika tafakari ya Neno la Mungu Dominika hii ya 16 ya Mwaka A wa Kanisa. Katika dunia yetu ya leo na katika jamii zetu mbali mbali, tunashuhudia ongezeko kubwa la uhalifu, mauaji, dhuluma, ufisaidi, uvunjifu wa haki na amani pamoja na mambo mengi yasiyompendeza Mungu. Mbele ya matukio yote hayo pengine tunajiuliza, kwanini Mungu anawaacha waovu waendelee kusitawi katika jamii zetu? Katika tafakari ya Neno la Mungu leo hii, Bwana wetu Yesu Kristo anatuonyesha jinsi Mungu alivyo mwingi wa subira na rehema akiwaalika wenye dhambi wote waweze kutubu. Tafakari yetu leo hii inaongozwa na  masomo matatu. Somo la kwanza linatoka katika kitabu cha Hekima ya Sulemani Sura ya 12 aya ya 13 na aya ya 16 hadi 19. Somo la pili linatoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi Sura ya 8 aya ya 26 hadi ya 27 na somo la tatu linatoka katika Injili ya Mathayo Sura ya 13, aya ya 24 hadi ya 43.

Katika Injili tuliyoisikia, Bwana wetu Yesu Kristo anaufananisha Ufalme wa mbinguni na shamba ambamo mbegu nzuri na magugu hukua pamoja. Mbegu nzuri inayopandwa na mwenye shamba ni mfano wa Yesu mwenyewe anayepanda mbegu ya Neno lake katika moyo wa mwanadamu. Neno hili ndiyo Hekima ya Mungu na msingi unaomwezesha mtu kutenda yale yote yaliyo mema yenye kumpendeza Mungu. Hili ndilo Neno la uzima liletalo furaha na amani kwa yule anayelishika na kwa wale wote wanaomzunguka. Ndilo Neno lenye kuokoa na kumpatia mtu uzima wa milele. Nyuma ya Yesu huja adui mwovu na kupanda ndani ya mioyo wa mwanadamu chuki, kiburi, tamaa mbaya na ubinafsi ambavyo humwelekeza mtu katika kutenda maovu mbele za Mungu na mbele ya jamii. Kutokana na hila za mwovu, ndani ya kila Mkristu na ndani ya kila mwanadamu kuna mvutano wa nguvu mbili, nguvu ya Roho wa Mungu inayotusukuma kutenda mapenzi ya Mungu na nguvu ya yule mwovu itusukumayo kutenda uovu na kutupeleka mbali na Mungu. 

Kiini cha fundisho la Yesu katika mfano wa Injili ya leo ni pale ambapo mwenye shamba anawakataza watumishi wasiende kuyang’oa magugu shambani na badala yake wayaache yakue pamoja na mbegu nzuri. Anawaamuru wasubiri wakati wa mavuno ndipo watenganishe magugu na mazao wakiyaondoa magugu hayo na kuyachoma moto. Jibu la mwenye shamba halikuwashangaza tu watumishi wake bali latushangaza sisi pia kwa kuwa ni kawaida yetu sisi tulio wakulima kufanya palizi na kuondoa magugu yote ili mbegu nzuri ziweze kukua vizuri na kuzaa matunda bora. Kukubali kuyaacha magugu yakue pamoja na mbegu ni sawa na kukubali kucheka na nyani shambani kwani waswahili husema, “Ukicheka na nyani utavuna mabua.”

Desturi yetu ya kuondoa magugu yote shambani inafanana kabisa na hamu tuliyonayo ya kukomesha uovu wote katika jamii zetu. Tunapoyaangalia maovu mbalimbali yanayotokea katika jamii mfano wizi, ufisadi, ubakaji, uuaji, na matendo mengi mengine kama hayo, tunajiuliza, kwa nini Mungu anawaacha waovu waendelee kustawi katika jamii zetu? Sisi wenyewe tungependa kutoa hukumu na adhabu kali kwa wahalifu wote ili kukomesha uovu katika jumuiya zetu. Mara ngapi tumesikia hata katika mabunge yetu mapendekezo ya kuwafutilia mbali wale wanaofanya maovu katika jumuiya zetu. Mfano tumeshuhudia mara kadhaa baadhi wakitoa mapendekezo kwamba mafisaidi wote wanyongwe au wabakaji wote wahasiwe, n.k. Mara kadhaa imetokea wananchi kujichukulia sheria mkononi mwao kwa kuwachoma moto wahalifu mbalimbali au kuwaua vikongwe wakiwatuhumu kuwa ni wachawi. Hatua kama hizo ni kinyume kabisa cha mafundisho ya Yesu.

Katika Injili ya leo Yesu anatuonesha jinsi ambavyo haki ya Mungu ni tofauti na haki yetu wanadamu. Mungu anawahukumu wakosefu kwa Moyo wa huruma na subira. Mungu hawapendi walio wema tu bali huwapenda hata wenye wadhambi japo anayachukia maovu yao. Katika somo la kwanza tumesikia kuwa Mungu anawaangalia watu wote bila ubaguzi. Pamoja na nguvu na uwezo alionao Mungu huwatawala na kuwahukumu watu kwa upole na kwa uvumilivu mwingi. Ndiyo maana Yesu akiwa hapa duniani hakuwabagua watu, hakuwatenga wadhambi bali aliwasogelea, akiwapa muda waweze kutubu naye akawasamehe wote waliotubu.

Nilipata nafasi ya kutoa huduma ya kiroho katika gereza fulani lenye ulinzi wa pekee na wa hali ya juu. Wafungwa waliopo katika gereza hili ni wale waliotenda uhalifu mkubwa katika jamii. Mambo mabaya waliyokuwa wakiyafanya ikiwepo kujihusisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya iliwapelekea hata kuua watu kadhaa wasiokuwa na hatia. Kitu cha pekee kwa wafungwa wa gereza hili maalumu ni kwamba wanatambua na kukiri ubaya na uchungu mkubwa waliousababisha kwa jamii na hasa kwa familiya mbalimbali zilizowapoteza ndugu zao. Kwa sababu hiyo wako tayari kubadilika na kushirikiana na serikali kuondoa mtandao wa maovu katika jamii. Kwakuwa nao karibu niliweza kutambua neema na nafasi ambayo Mungu anampa kila mmoja wetu aliyepotoka ili abadilike kwa kuiacha njia mbaya na kutenda mema. Nilipokuwa nikiongea na mtu fulani juu ya mang’amuzi hayo, yeye alikuwa na mtazamo tofauti akidai kuwa wafungwa kama hao wanastahili wapate hukumu inayoendana na matendo yao.

Ujumbe wa Neno la Mungu leo hii unatualika sote kutumia vema nafasi anayotupa Mungu tuweze kutubu dhambi zetu. Hakuna dhambi yeyote iliyokubwa kuliko huruma ya Mungu. Hata hivyo, endapo hatutachukua hatua kufanya hivyo, hakika tutahukumiwa na kuchomwa moto kama magugu. Mungu anapenda pia tubadili mtazamo wetu mbele ya wenzetu wakosefu. Yeye hataki tubaki bila kufanya chochote katika kukabiliana na uovu bali katika kuchukua hatua yeyote lazima tuige mfano wake wa kuwahukumu wengine daima kwa huruma na upole. Tusisahau kuwa kila mwanadamu mbali na hali yake ya dhambi, ana thamani kubwa mbele ya macho ya Mungu. Kwa sababu hiyo Yesu alimwaga Damu yake kwa ajili ya wote ili yeyote anayemwamini aweze kuokoka. Tumwombe Roho Mtakatifu atusaidie ili tuweze kuisikiliza daima sauti yake tupate kumpendeza Mungu daima katika maisha yetu.

Na Padre Walter Milandu, C.PP.S.
All the contents on this site are copyrighted ©.