2017-07-21 17:14:00

Wito: viongozi wa kidini wanapaswa kushikamana na kuwajibika


Viongozi wa dini mbali mbali duniani wanapaswa kushikamana na kuwajibika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kujiunga na mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato duniani; kwa kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu pamoja na kujikita kikamilifu katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Mchango wa viongozi wa kidini unapaswa kusimikwa hasa katika kanuni maadili na utu wema, ili kuhakikisha kwamba, kweli Jumuiya ya Kimataifa inashikamana dhidi ya umaskini, magonjwa na baa la njaa duniani; daima utu na heshima ya binadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza. Yote haya yakizingatiwa kwa ukamilifu, haki na amani vitaweza kutawala duniani!

Hii ni sehemu ya mchango uliotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican wakati wa majadiliano kwenye Jukwaa la Kisiasa kwenye Umoja wa Mataifa. Anasema, mchakato wa Maendeleo Endelevu kuanzia sasa hadi ufikapo mwaka 2030 unahitaji kwa namna ya pekee, Jumuiya za kidini kujenga mshikamano na uwajibikaji wa pamoja, ili kudumisha mafao ya wengi, kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, mambo msingi katika mchakato mzima wa maendeleo endelevu. Bila kuzingatia mambo haya, Malengo ya Maendeleo Endelevu yatajikita zaidi katika masuala ya: uchumi, mazingira na jamii na hivyo kuwasahau maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kanuni maadili, utu wema, upendo kwa Mungu na jirani ni mambo muhimu sana yanayoweza kuisaidia Jumuiya ya Kimataifa kushikamana na kuwajibikiana kama ndugu anasema Askofu mkuu Bernardito Auza. Viongozi wa kidini wasiposimamia misingi ya haki na amani; umoja, upendo na mshikamano wa dhati, matokeo yake ni baadhi ya watu kuibuka wakiwa na misimamo mikali ya kidini na kiimani, ambayo imepelekea mauaji ya kimbari sehemu mbali mbali za dunia; ubaguzi wa kidini; kuenea kwa jangwa pamoja na kukumbatia utamaduni wa kifo.

Viongozi wa kidini wakihamasika na kushikamana kwa dhati wanaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya binadamu; huku binadamu na mahitaji yake msingi akipewa kipaumbele cha kwanza. Viongozi hawa wanapaswa kuwa ni mihimili ya kanuni maadili na maisha ya kiroho, ili kuweza kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili. Dini zimekuwa na mchango mkubwa sana katika huduma ya maendeleo endelevu kwa kuzingatia kwamba, zinatoa huduma muhimu sana katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya wengi. Wamejitahidi kuwa mstari wa mbele kulinda na kutetea uhai wa binadamu, utu na heshima yake; wamewajengea maskini uwezo wa kujiamini na hatimaye, wakaweza kupambana na changamoto za maisha ya kila siku.

Wengi wa viongozi hawa wamekuwa ni chachu ya majadiliano katika ukweli na uwazi kwa kutambua kwamba, amani ya kweli ni kikolezo kikuu cha maendeleo endelevu ya binadamu. Athari za mabadiliko ya tabianchi kama zinavyofafanuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” zinawagusa watu wote, lakini waathirika wakuu ni wananchi wanaoishi katika nchi maskini zaidi duniani na matokeo yake ni kutoweka kwa amani, ambalo ni jina jipya la maendeleo kama anavyosema Mwenyeheri Paulo VI.

Askofu mkuu Bernardito Auza anasema, amani na maendeleo ya kweli yanaweza kupatikana ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itashikamana kwa dhati kupambana na umaskini, magonjwa na baa la njaa; kwa kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu, sanjari na kutunza mazingira nyumba ya wote! Mifumo yote ya ubaguzi, ubinafsi na uchoyo; uchu wa mali na madaraka ni mambo ambayo yanaendelea kuwatumbukiza watu wengi katika utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Matokeo yake ni kufilisika kwa maisha ya kiroho, watu kuanza kukengeuka na kutopea katika imani. Yote haya yanaonesha umuhimu wa viongozi wa kidini kujizatiti katika mshikamano na uwajibikaji wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya binadamu. Kigezo kikuu cha ufanisi wa utekelezaji wa Malengo haya kiwe ni ubora unaofumbatwa katika kanuni maadili na utu wema; kwa kuwaunda na kuwafunda watu kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote; kwa kushikamana na kupendana kama ndugu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mshikamano na uwajibikaji ni muhimu sana katika mchakato wa kuiwezesha ekolojia kuwa jambo halisi kabisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.