2017-07-21 07:00:00

WCC: Amani ya kweli inapatikana kwa njia ya majadiliano!


Baraza la Makanisa Ulimwenguni linasema, malumbano ya vitisho vya mashambulizi ya kijeshi yanayoendelea kusikika katika medani za kimataifa ni hatari sana kwa maendeleo, ustawi na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa. Daima ikumbukwe kwamba, vita ina madhara makubwa katika maisha ya binadamu, ni janga linalowagusa wahusika wa karibu na hata wale wasiohusika. Kumbe, busara inapaswa kutawala kwa kumaliza kinzani na migogoro ya Jumuiya Kimataifa katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi, daima utu na heshima ya binadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwa kushirikiana na Baraza la Makanisa Nchini Korea ya Kusini yanawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumkimbilia Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala ili kuepusha malumbano ya mashambulizi ya kivita kati ya Marekani na Korea ya Kaskazini yasigeuke kuwa kweli ni vita itakayosababisha madhara makubwa ndani na nje ya nchi husika! Dr. Olav Fykse Tveit anawaalika waamini kusali kwa ajili ya kuombea amani duniani pamoja na kuendelea kujikita katika majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi, ustawi na mafao ya wengi badala ya kutaka kuoneshana “ubabe wa kivita” kwa kutunishiana misuri.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linaendelea kusema kwamba, lengo lake msingi ni kuhakikisha kwamba, linasaidia mchakato wa haki, amani, upatanisho na mafungamano ya wananchi wa Korea zote mbili, ili siku moja, ziweze kuungana na kuwa ni nchi moja kama ilivyokuwa hapo awali! Kwa muda wa miaka thelathini, Baraza la Makanisa Ulimwenguni limekuwa likiendesha mchakato wa majadiliano kati ya Wakristo Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini. Lakini kwa siku za hivi karibuni kutokana na homa ya malumbano ya mashambulizi ya kijeshi kati ya Marekani na Korea ya Kaskazini kuendelea kupamba moto, majadiliano ya waamini wa nchi hizi mbili za Korea yameshindikana.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linakaza kusema, kamwe vita si suluhu ya kinzani na changamoto zinazoendelea kumwandama binadamu bali ni kielelezo cha udhaifu wa binadamu ambaye ameshindwa kutumia fursa na nyenzo mbali mbali kukuza na kudumisha majadiliano, ili kweli amani iweze kupatikana katika akili na nyoyo za watu! Amani ya kweli kamwe haiwezi kupatikana kwa njia ya mashambulizi ya mabomu, kwani madhara yake ni makubwa na yatachukua muda mrefu kuweza kutibiwa! Amani ya kweli inapatikana kwa njia ya majadiliano na utashi wa kisiasa unaopania mafao ya wengi.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwa kushirikiana na Baraza la Makanisa nchini Korea ya Kusini, yameendesha sala ya pamoja katika kipindi cha maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka kwa ajili ya kuombea haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hii imekuwa pia ni nafasi ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa Jimbo kuu la Seoul kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka tisini tangu kuanzishwa kwake. Kardinali Andrew Yeom Soojung, wa Jimbo kuu la Seoul ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, kwa kuwaombea Wakristo wa nchi hizi mbili ambao kwa njia ya maisha yao wameendelea kuwa ni mashuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake, licha ya hali ngumu ya uhuru wa kuabudu wanayokabiliana nayo! Hawa ni mashuhuda wa imani ya Kikristo katika Karne ya 21 kama anavyokaza kusema, Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake wakati wa Ibada ya Liturujia ya Neno la Mungu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaenzi mashuhuda wa imani walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake katika karne ya ya 20 na 21!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.