2017-07-21 15:13:00

Papa Francisko atoa msaada kwa waaathirika wa njaa Afrika Mashariki


Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya familia ya Mungu Afrika Mashariki iliyoathirika kwa ukame wa kutisha pamoja na baa la njaa, ameamua kuchangia kiasi cha Euro 25, 000 ili kusaidia mchakato wa upatikanaji wa chakula cha msaada. Baba Mtakatifu anasema, mchango huu ni alama hai kwa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO kwa ajili ya kuunga mkono juhudi zake ili kutoa mbegu na pembejeo za kilimo kwa familia za wakulima vijijini ambazo zimeathirika na vita pamoja na ukame wa kutisha!

Msisitizo huu umo kwenye barua ya Baba Mtakatifu Francisko aliyomwandikia Professa Josè Graziano da Silva kupitia kwa Monsinyo Fernando Chica Arellano, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Kilimo na Chakula za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Roma. Mchango huu ni sehemu ya utekelezaji wa ombi la Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mkutano mkuu wa FAO, uliofanyika tarehe 3 Julai 2017 alipowaalika wakuu wa Serikali na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake, kuhakikisha wanatekeleza dhamana na wajibu wao katika kusaidia kupambana na baa la njaa duniani na hasa zaidi huko Sudan ya Kusini ambako kuna zaidi ya watu milioni 6 wanakabiliwa na baa la njaa.

Takwimu zinaonesha kwamba, idadi ya watu wanaohitaji chakula cha msaada inazidi kuongezeka maradufu katika nchi za Afrika Mashariki hasa: Somalia, Ethiopia, Kenya, Uganda na Tanzania, ambako kuna zaidi ya watu milioni 16 wanaotishiwa na baa la njaa ambalo limeongezeka kwa asilimia 30 tangu mwaka 2016. Baba Mtakatifu katika maisha na utume wake anapenda kukazia umoja na mshikamano katika huduma kwa maskini kama sehemu muhimu sana ya maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Tarehe 16 Oktoba 2017 katika maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kutembelea na kuzungumza na wajumbe wa FAO. Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Chakula kwa Mwaka 2017 ni “Kubadili mwelekeo wa wahamiaji”: Wekeza katika usalama wa chakula na maendeleo vijijini”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 
All the contents on this site are copyrighted ©.