2017-07-21 07:11:00

Haki ya Mungu ni huruma yake!


Leo hii tunasikia tena Neno la Mungu masikioni mwetu na mioyoni mwetu. Dominika iliyopita tulisikia habari ya mpanzi na mbegu na tuliona kuwa mbegu ni Neno la Mungu, Kristo ni mpanzi na mavuno ni wale waliolisikia hilo neno. Changamoto iliyowekwa mbele yetu ni kuwa je sisi tuko eneo gani kati ya maeneo yaliyotajwa katika maisha yetu ya kumtumikia Mungu. Je, katika udongo wa njiani, katika miiba, katika mwamba au katika udongo mzuri? Wito wetu na majibu yetu kwa Mungu ni kutoa mavuno mema.

Katika Jumapili hii, Yesu Kristo anaelezea hali ya Kanisa ulimwenguni katika mifano mitatu – mbegu ya haradali – akielezea ukuaji wa ufalme wa Mungu hapa duniani, mfano wa chachu – akielezea ukuaji wa ufalme lakini siyo kieneo bali akionesha nguvu ya Neno na uwezo wake wa kubadilisha hali. Mifano hii miwili inaeleweka kwa urahisi na mitume. Ule mfano wa tatu anautolea maelezo ya kina. Mpanzi ni yeye mwenyewe, mbegu nzuri ni wana wa Mungu, mbegu mbaya ni wana wa yule  mwovu na mavuno ni mwisho wa ulimwengu.

Ndugu zangu, katika mahangaiko ya mwanadamu kuishi neno la Mungu na katika jitihada za kuushuhudia huo ufalme wa Mungu tunaweza pia hata kupoteza lengo la uwepo wa ufalme wa Mungu na hata pia kupoteza maana ya uwepo wetu. Swali ambalo watu waweze jiuliza ni hili. Kwa nini ukristo umehubiriwa miaka yote lakini bado watu wengi hawajaongoka? Mtaalamu mmoja wa maswala ya dini, G. K. Chesterten  anasema, ukristo haujashindwa bali watu hawajaishi vyema hiyo habari njema. Mwinjili Matayo katika 5:7… anaongea juu ya heri ambao ni mwongozo mzima wa kufika mbinguni. Wanaoamini wanajua hili lakini pengine changamoto inakuwa ni kwa kiasi gani wanaoamini wanaishi neno hilo.

Tuangalie mifano michache iliyojitokeza katika historia ya kanisa juu ya uelewa huu na jinsi ilivyosababisha migongano mbalimbali. Wa Donati – waliokuwa na namna yao ya kuelewa maana ya Kanisa – walipoteza mwelekeo kabisa – waliishi kanisa la kufikirika, la wazuri na wabaya wa ulimwengu wa wenye dhambi. Tunatambua pia maisha ya Mt. Paulo aliyelidhulumu kanisa akiwa na mtazamo mbaya wa ukristo. Benjamin Smith – wa Kanisa la “White supremacist World Church of the Creator” – aliyekuwa na chuki hata ya kifo dhidi ya Wayahudi, Weusi na Waasia.  Mtakatifu Agustino, Askofu na mwalimu wa Kanisa anatukumbusha kuwa hili shamba ni kweli liko ulimwenguni lakini pia ni Kanisa  mahalia ambapo wema na wabaya wanaishi pamoja, lakini penye nafasi ya kukua na kuongoka. Walio wabaya wanapata nafasi ya kuongoka au kwa sababu ya uwepo wao, wengine wanaweza kuishi uvumilivu.

Ndugu zangu, hatuna budi kukumbuka kuwa kanisa limewekwa kwa ajili ya wanadamu na kwa ajili ya wokovu wao. Siyo kwa ajili ya watakatifu. Yapo magugu pia ndani yetu na kati yetu na miongoni mwetu. Jambo jema ni kwamba Mwengyezi Mungu ametupa nafasi ya kumwendea yeye. Ametupatia nafasi ya kushiriki katika kueneza na kujenga huo ufalme. Martin Luther alimkemea Erasmus wa Rotterdam kwa kuendelea kubaki ndani ya Kanisa Katoliki pamoja na madhambi yaliyopo. Erasmus alimjibu akimwambia, ninabaki nikiamini kuwa siku moja litakuwa bora zaidi, lakini pia linapaswa kunivumilia likiamini kuwa siku moja nami nitakuwa bora zaidi. Jibu la Yesu ni kwa nini kuacha magugu na ngano mpaka mwisho ni tofauti kabisa na mawazo ya Luther. Na hapo ndipo tofauti ya jibu la Yesu na mawazo ya mwanadamu inapopata changamoto. Hakika Yesu hasemi au kuunga mkono uwepo wa magugu, bali anasema tuchukue muda na anasema wazi ni lini yatolowe.

Lengo kubwa la mfano huu wa ngano na magugu katika Injili ya leo ni kuonesha huruma kuu ya Mungu. Angalia somo la kwanza, mwandika neno hili anausifu uvumilivu na huruma ya Mungu ambayo si tu inasubiri saa ya mwisho bali huwepo daima kwa ajili ya mwanadamu amtafutaye Mungu. Huwaangazia jua wema na wabaya n.k., lakini hutoa hukumu siku ya mwisho. Ndicho tuonacho katika injili kwamba muda wa mavuno ni mwaliko wa kuuweka mtazamo wetu katika ukweli, kuona mambo katika mwanga wake Mungu. Muda wa kuishi hapa duniani ni kipindi cha kutenda ili kile kilichopandwa kitoe mavuno. Lakini katika kutenda huko ni lazima tuongozwe na roho wake Mungu. Somo la pili linatuangalisha sana. Peke yetu hatutaweza kumtumikia Mungu ipasavyo. Tunapaswa kuongozwa na roho wake daima.

Sote tunaalikwa kulinda mbegu ya Neno lake ambalo amepanda katika mioyo yetu na kuwa waangalifu dhidi ya nguvu za yule mwovu. Neno la Mungu ni uhai na uzima lakini shetani atafuta kuliharibu. Tujaribu kufikiria thamani ya ukombozi alioleta Kristo kwa kumwaga damu yake msalabani. Sisi tumeshakombolewa. Lakini pia tunajua wazi kuwa tunamsubiri Bwana atakayekuja mara ya pili kwa hukumu. Uhakika tulio nao ni kwamba Mungu ni Bwana wa haki na hukumu yake si kama yetu sisi. Lakini inakuja. Ni hukumu juu ya kile tulichopanda na kuvuna katika maisha yetu. Atatenganisha dhambi na wema. Ile mifano miwili ya mwisho katika Injili ya leo itufikirishe sana – punje ya haradali na chachu.

Mtu mmoja aitwaye Charles Read anasema – panda tendo na utavuna mazoea, panda mazoea na utavuna tabia na panda tabia na utavuna mwisho mwema. Katika 2 Kor. 4, 7 tunasoma hivi: lakini tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu. Nimalizie tafakari hii nikimkumbuka Mt. Paulo anayekiri kuwa nguvu zake peke yake hazitoshi katika kutimiza kazi zake za utume. Anakiri kwa unyenyekevu udhaifu wake. Lakini anasadiki pia kuwa Mungu aweza kuendesha maisha yake na kumkamilisha katika yote kwa kutumia watu dhaifu. Baada ya tafakari kama hiyo na ujumbe mzuri kama huo, tunajiuliza Je, sisi ni ngano au magugu?

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S








All the contents on this site are copyrighted ©.