2017-07-20 14:12:00

Ujenzi wa hospitali ya watoto waanza huko Bangui, Afrika!


Baba Mtakatifu Francisko anasema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni tukio endelevu linalopaswa kutangazwa, kushuhudiwa na kuwazamisha watu katika huruma ya Mungu. Kanisa linahamasishwa kuwa ni shuhuda mwaminifu wa huruma ya Mungu, kiini cha ufunuo wa Kristo Yesu unaopata chimbuko lake kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Huruma ya Mungu iguseu na kuwaonjesha waamini umuhimu wa kusamehe, kutegemeza, kusaidia na kudumisha upendo hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Ziara ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika kunako mwaka 2016 na kwa namna ya pekee, nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati inaendelea kuzaa matunda ya huduma makini, licha ya kwamba, ilikuwa ni nchi ya kwanza kuadhimisha Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mahangaiko ya watoto wadogo nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, aliamua kusaidia mchakato wa huduma kwa watoto hawa na sasa tayari jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya watoto wadogo mjini Bangui, limewekwa.

Tukio hili limehudhuriwa na Rais Faustin Archange Touadera wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati kwa niaba ya Serikali yake na Vatican imewakilishwa na Dr. Mariella Enoc, Rais wa Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican pamoja na maafisa wa ubalozi wa Vatican nchini humo. Ujenzi wa kitengo cha watoto wagonjwa wa utapiamlo, licha ya kupewa tiba na lishe bora, lakini pia wanawake watafundwa namna ya kuwahudumia watoto wao wanaokabiliwa na utapiamlo wa kutisha.

Vatican pia imeanza kulipa mishahara kwa madaktari na wafanyakazi wa hospitali ya watoto wadogo sanjari na ukarabati mkubwa wa miundo mbinu ili kuweza kutoa huduma bora zaidi kwa watoto wagonjwa kama alivyokazia Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume Barani Afrika. Dalili za mafanikio zinaanza kuonekana kwa vifo vya watoto wadogo wenye umri chini ya miaka 5 kuanza kupungua kutokana na maboresho ya huduma kwa watoto hawa. Mwezi Septemba 2017, kuna baadhi ya wafanyakazi wataanza kupata mafunzo ya tiba kwa ajili ya watoto wadogo yatakayotolewa na Hospitali ya Bambino Gesù ili kwamba, watakapohitimu masomo yao, waweze kurejea nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, ili kutoa huduma bora zaidi kwa watoto wagonjwa. Yote haya yanawezekana kutokana na moyo wa ukarimu na upendo unaoshuhudiwa na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na wafadhili mbali mbali ndani na nje ya Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.