2017-07-20 14:42:00

Changamoto mamboleo: haki na amani; maskini na mazingira!


Umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kudumisha haki na amani; upendeleo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kutetea haki msingi za binadamu pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni kati ya changamoto zinazotolewa leo hii na Mtakatifu Francisko wa Assisi, ambaye, Baba Mtakatifu Francisko ameamua kumteuwa kuwa ni msimamizi katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Mtakatifu Francisko katika ujana wake aliponda sana mali, lakini hatimaye, akagundua utajiri wa maisha ya kiroho uliokuwa umefichika katika ufukara, hivyo akaamua  kuyavua malimwengu, changamoto kwa walimwengu wenyewe walau kujitahidi kumwilisha sehemu ya ujumbe wa Mtakatifu Francisko, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi! Hii ni changamoto inayotolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Bwana Orazio La Rocca, kwa ajili ya Jarida la “Sanfrancesco” linalomilikiwa na kuchapishwa na Konventi ya Assisi, nchini Italia. 

Itakumbukwa kwamba, mwezi Mei, 2017, Kardinali Pietro Parolin, aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuzindua “Madhabahu Mapya ya Kuvulia Nguo” huko Assisi, kama kumbukumbu ya ushujaa ulioneshwa na Mtakatifu Francisko kwa kuvua malimwengu yote na kubaki mtupu! Hili ni tukio ambalo hata leo hii bado linawafikirisha sana watu. Baba Mtakatifu Francisko kwa upande wake anakazia umuhimu wa kazi kama sehemu ya utimilifu wa utu na heshima ya binadamu. Waajiri wanapaswa kukumbuka na kutambua thamani ya binadamu badala ya kuangalia tu idadi ya wafanyakazi na faida wanayoweza kupata katika vitega uchumi vyao.

Kardinali Parolin anaendelea kufafanua kwamba, kuna uhusiano mkubwa kati ya Mtakatifu Francisko wa Assisi na binadamu mamboleo, changamoto ni kwa watu wa nyakati hizi kusikiliza kwa makini sauti na changamoto inayotolewa na Mtakatifu Francisko wa Assisi kwa kukazia kwanza kabisa amani. Kwa njia ya amani, vita itatoweka na watu watapata maendeleo zaidi kwa kuendelea kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Itakumbukwa kwamba, vita ni mama wa maafa mengi yanayomsibu mwanadamu. Kwa kudumisha amani, madhara yote ya vita yataweza kudhibitiwa kikamilifu sanjari na kukomesha biashara haramu ya silaha na mabomu ya kutegwa ardhini ambayo yameendelea kupandikiza mbegu ya hofu na kifo miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa. Kulinda, kutunza na kudumisha mazingira nyumba ya wote,  afya na maisha ya watu wengi zaidi yangeweza kuboreka; watu wangekuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kupambana na baa la umaskini.

Jambo la kusitikisha ni kuona kwamba, utajiri mkubwa na rasilimali za dunia ziko miokononi mwa watu wachache wanaozimili na kuzitumia, wakati ambapo kuna mamilioni ya watu wanaoteseka na kufa kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha; umaskini na magonjwa. Hili ni kundi ambalo limepokwa utajiri na rasilimali ya dunia. Kardinali Pietro Parolin anakaza kusema, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha upendo na mshikamano kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa kuwawezesha kiuchumi na kijamii kama alivyofanya Mtakatifu Francisko wa Assisi kwa watu na maskini wa nyakati zake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.