2017-07-19 15:06:00

Wananchi wa Ukraine watakiwa kuwa na ujasiri na matumaini thabiti


Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki amehitimisha safari yake ya kikazi nchini Ukraine aliyoianza tarehe 11 hadi 17 Julai 2017 kwa kuitaka familia ya Mungu nchini Ukraine kuwa na ujasiri kwa wakati huu na matumaini kwa siku za usoni. Amewafikishia: baraka, salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko anayewapenda na kuwahimiza kuendelea kutembea katika mwanga wa Kristo wa Kristo Mfufuka unaoangaza hata katika giza la maisha ya kiroho.

Kardinali Leonardo Sandri amewahakikishia uwepo wa karibu wa Baba Mtakatifu Francisko katika hija ya maisha yao ya kila siku na kwamba, anawakumbuka na kuwaombea. Amekazia kwa namna ya pekee kabisa, umuhimu wa kujenga na kudumisha haki, amani, msamaha na upatanisho wa kweli, ili kuimarisha umoja wa kitaifa! Amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, ili kupata ulinzi na tunza yake ya kibaba sanjari na kuhakikisha kwamba, familia zinakuwa ni mahali pa haki, upatanisho na amani ya kudumu.

Hija ya Kardinali Sandri katika Madhabahu ya Bikira Maria wa Zarvanytsia, ilianza Jumamosi jioni, tarehe 15 Julai 2017: kwa kutembelea Seminari, mahali ambapo majandokasisi wanafundwa kwa ajili ya kujisadaka na kujitoa kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake katika maisha na utume wa Kipadre. Akabariki Jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa hospitali itakayowahudumia wananchi wote pasi na ubaguzi na hatimaye, akashiriki katika mkesha wa Jubilei ya Miaka 150 tangu Bikira Maria wa Zarvanytsia alipovikwa taji la dhahabu. Amepata nafasi ya kukutana, kusali na kuzungumza na vijana wa kizazi kipya waliokuwa wamefurika madhabahuni hapo utadhani “umande wa asubuhi”.

Kardinali Leonardo Sandri amewataka vijana kujenga imani, matumaini na mapendo, bila kukata wala kukatishwa tamaa kutokana na changamoto pamoja na matatizo wanayokutana nayo! Amewataka kujizatiti katika masomo, ili hatimaye, waweze kupata fursa ya kazi kwa siku za usoni. Anatambua hali ngumu ya maisha na imani waliyokutana nayo katika miaka ya hivi karibuni, lakini bado wamebaki kuwa imara kama “chuma cha pua”.

Katika safari ya maisha, wasiwe ni watu wenye uchu wa mali na madaraka; watu wanaotaka kupata mafanikio kwa haraka haraka, kwani mwelekeo wa namna hii ni hatari kabisa unaweza kuwatumbukiza katika mmong’onyoko wa kanuni maadili na utu wema; hali ambayo inaweza kuwakatisha tamaa ya maisha! Vijana wasimamie: haki na amani; ukweli, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, daima wakiwa na mwelekeo sahihi wa maisha unaofumbatwa katika matumaini; upendo, ukarimu na mshikamano. Waendelee kuwa waaminifu kwa imani na utambulisho wao, ili kuwa kweli ni mashuhuda yaani chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa.

Vijana watambue kwamba, wanayo nguvu ndani mwao, yakuweza kuleta mabadiliko ya kweli katika ustawi na maendeleo ya watu. Washinde kishawishi cha rushwa na ufisadi, kwa kujikita katika uaminifu, kwa Mungu, Kanisa na binadamu wenzao. Vijana wasimame kidete kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba. Wasikubali kutekwa na wajanga wachache wanaotaka kutumia umaskini wao wa hali na kipato kuwatumbukiza katika mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo.

Kardinali Leonardo Sandri anasema, pale ambapo vijana hawa wamekengeuka na kupotoka, wawe na miguu miyepesi kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Amewataka vijana wa kizazi kipya kujiandaa kikamilifu katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana inayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito” itakayofanyika mwezi Oktoba, 2018 sanjari na maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 yatakayofanyik nchini Panama kuanzia tarehe 22- 27 Januari 2019, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Tazama mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema”. Matukio yote haya yawapatia vijana nafasi ya kutafakari dhamana na wito wao katika maisha na utume wa Kanisa.

Kardinali Leonardo Sandri alijumuika na vijana kwa ajili ya maandamano, mkesha na sala na kuwataka vijana wa kizazi kipya kuwa kweli ni mwanga wa mataifa; faraja kwa watu wanaoteseka na kusumbuka kutokana na sababu mbali mbali, hasa madhara ya vita; vijana wasiokuwa na fursa za ajira; watoto yatima; walemavu pamoja na wale wote wanaoogelea katika dimbwi na hali ya kukata tamaa ya maisha, wote hawa wamekumbukwa na kuombewa. Haya ndiyo matunda na madhara ya ubinafsi, uchoyo na dhambi! Vijana wasimame kidete katika misingi ya haki, amani na maridhiano kwa kuondokana na kishawishi cha kutaka kulipizana kisasi; bali wao wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa watu wake.

Kardinali Leonardo Sandri ambaye Jumatatu, tarehe 17 Julai 2017 amerejea tena mjini Vatican amewaambia vijana kwamba, anahitimisha safari ya kikazi, huku taa ya moyo wake ikiwa inawashwa na mafuta ya imani, matumaini na mapendo yao. Amewataka kujenga na kudumisha uekumene katika sala, maisha ya kiroho, huduma na ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Mwishoni, ametembelea kijiji alikozaliwa Kardinali Josyf Slipyj.

Na Padre Richard A, Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.